Maaskofu 500 wa kanisa la Gwajima watinga mahakamani

Muktasari:
- Maaskofu wengi kutoka maeneo mbalimbali nchini ambako Kanisa la Glory of Christ Tanzania Church lina matawi, wameathiriwa na hatua ya Serikali kulifunga kanisa hilo, hatua iliyozua mjadala kuhusu uhuru wa kuabudu na uhalali wa uamuzi huo wa kiserikali.
Dodoma. Kanisa la Glory of Christ Tanzania Church, maarufu kama Kanisa la Ufufuo na Uzima, limefungua kesi Mahakama Kuu, Kanda ya Dodoma, likiomba amri ya muda ya kuondoa zuio lililowekwa na Serikali dhidi ya kuendelea kwa shughuli zake za kidini, huku ikiripotiwa takribani maaskofu 500 wamefika kusikiliza kesi hiyo.
Kesi hiyo inalenga kulinda hadhi ya usajili wa kanisa hilo huku rufaa dhidi ya zuio hilo ikiendelea kusikilizwa.
Kanisa hilo linaongozwa na Askofu Josephat Gwajima, ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Kawe kupitia CCM.

Baadhi ya maaskofu wa Kanisa la Glory of Christ Tanzania, wakiwa katika Mahakama Kuu Kanda ya Dodoma kwenye kesi ya kupinga kufutwa kwa kanisa hilo.
Hivi karibuni, mamlaka za Serikali zilifunga kanisa hilo kwa madai kwamba linaendesha shughuli kinyume na masharti ya leseni ya usajili wake.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa mamlaka, baadhi ya shughuli zinazofanyika ndani ya kanisa hilo zimeelezwa kuwa ni za ‘kisasa kupita kiasi’, na hazilingani na malengo ya asili ya taasisi hiyo kama ilivyosajiliwa.
Kupitia kwa wakili wake, Peter Kibatala, kanisa hilo limewasilisha shauri namba 13189 la mwaka 2025 dhidi ya Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Mwanasheria Mkuu wa Serikali, na Msajili wa Taasisi za Kiraia.

Mawakili wa Kanisa la Glory of Christ Tanzania, Peter Kibatala na Gloria Ulomi wakiwa katika Mahakama Kuu Kanda ya Dodoma kwenye kesi ya kupinga kufutwa kwa kanisa hilo.
Katika shauri hilo, Glory of Christ Tanzania Church inaiomba mahakama kutoa amri ya muda itakayoruhusu kuendelea kwa ibada na shughuli nyingine za kidini, hadi pale rufaa iliyowasilishwa kupinga hatua ya serikali kufungia kanisa hilo itakaposikilizwa na kuamuliwa rasmi.
Wakili Kibatala akiwa amenongza na viongozi wa kanisa hilo amesema kuwa lengo la ombi hilo ni kuhakikisha kuwa haki za msingi za waumini wa kanisa hilo, ikiwemo uhuru wa kuabudu kama ulivyoainishwa katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, zinazingatiwa huku mchakato wa kisheria ukiendelea.
Hatua ya kufunga kanisa hilo imeibua mjadala mpana katika jamii, hasa miongoni mwa waumini na wafuasi wa Askofu Gwajima, ambapo baadhi yao wameitaka Serikali kutoa maelezo ya kina kuhusu sababu za hatua hiyo na kuwataka viongozi wa dini kupewa nafasi ya kujitetea kupitia taratibu za kisheria.