Prime
Mapya yaibuka mahakamani kufungwa Kanisa la Askofu Gwajima

Muktasari:
- Juni 2, 2025, Msajili wa Jumuiya za Kiraia, Emmanuel Kihampa alitangaza kulifuta Kanisa la Ufufuo na Uzima kwa kile alichokieleza limekiuka Sheria ya Jumuiya Sura ya 337, kwa kutoa mahubiri yenye mwelekeo wa kisiasa.
Dar es Salaam. Mvutano mkali wa kisheria, umeibuka kortini baada ya Serikali kuweka pingamizi la awali kupinga maombi yaliyofunguliwa na Bodi ya Wadhamini ya Kanisa la Glory of Christ Tanzania linalomilikiwa na Askofu Josephat Gwajima.
Hata hivyo, katika uamuzi wake alioutoa Juni 6, 2025 na kuwekwa katika tovuti ya mahakama, Jaji Juliana Masabo wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Kuu ya Dodoma, ametupilia mbali pingamizi lililowekwa na wajibu maombi.
Katika maombi hayo yaliyowasilishwa chini ya hati ya usikilizwaji wa dharura, Kanisa lilifungua maombi hayo dhidi ya Msajili wa Jumuiya za Kiraia, Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) na Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP).
Kupitia kwa wakili Peter Kibatala, kanisa hilo liliomba amri ya upande mmoja (Ex-Parte) kwamba barua ya msajili ya Juni 2, 2025 ya kulifunga Kanisa hilo, izuiwe kutekelezwa wakati wakisubiri kusikilizwa kwa maombi yao kwa pande zote na kutolewa uamuzi.
Lakini katika ombi mbadala, kanisa hilo limeiomba Mahakama ielekeze shughuli za Kanisa ziendelee kama kawaida (Status Quo Ante) wakati suala la usajili wa Kanisa likifanyiwa kazi kwa kuwa hakuna mawasiliano rasmi yamepelekwa kwao mpaka sasa.
Katika ombi la kusikilizwa pande zote (Inter parties), Bodi hiyo ya wadhamini inaiomba Mahakama itoe amri kwamba utekelezaji wa amri ya kufungwa kwa kanisa usimame kusubiri usikilizwaji wa rufaa yao kwa Waziri wa Mambo ya Ndani.
Kanisa limeeleza tayari wamewasilisha rufaa kupinga kufungwa kwa shughuli za kanisa hilo nchi nzima, kwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi ambaye ndiye mamlaka ya rufaa kulingana na kifungu cha 19 cha sheria ya Jumuiya za kiraia.
Pia wameomba Mahakama itoe amri maagizo ya Msajili wa Jumuiya za Kiraia ya kusitisha mara moja shughuli za kidini na kiimani na mikusanyiko ya kiroho katika kanisa hilo, yazuiwe au yasitishwe kutekelezwa hadi haki za kisheria za kanisa zitakapotekelezwa kikamilifu na msajili.
Halikadhalika wanaomba Mahakama imzuie IGP kuingilia shughuli za dini, imani na mikusanyiko katika kanisa hilo kwa kuegemea maelekezo ya Msajili, hadi rufaa yao itakaposikilizwa na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi na kutolewa uamuzi.
Maombi hayo yameambatanishwa na kiapo cha Bryson Lema ambaye amejitambulisha kama ofisa mkuu wa kanisa na mjumbe wa bodi ya wadhamini.
Pingamizi la Serikali
Katika shauri hilo, wajibu maombi ambao ni Msajili, AG na IGP waliwakilishwa na wakili wa Serikali mkuu, Vivian Method, akisaidiwa na wakili mwandamizi, Narindwa Sekimanga, Erigi Rumisha na Kumbukeni Kondo.
Mawakili hao waliwasilisha pingamizi la awali na kuiomba Mahakama ilisikilize kwanza na kulitolea uamuzi kwa kuwa linahusiana na uwezo wa mahakama hiyo kuweza kusikiliza maombi ya kanisa hilo linaloongozwa na Askofu Gwajima.
Wakili Method alisema msingi wa maombi hayo ni barua ya Juni 2, 2025 iliyoonyesha kama imetoka kwa Msajili ambaye ni mjibu maombi wa kwanza, ambayo ilibeba ujumbe wa kulifungia kanisa la Glory of Christ Church.
Kulingana na wakili huyo, jina hilo ni tofauti na la kanisa la mwombaji ambalo ni Glory of Christ Tanzania Church, hivyo kwa dosari hizo ina maana hakuna uamuzi wowote uliofanywa dhidi ya waleta maombi unaohitaji zuio.
Wakili wa Serikali Mkuu alisema kile kinachoitwa ni barua haina saini kama ambavyo mleta maombi amekiri kuwa hawajapata barua hiyo rasmi.
Kwa mujibu wa wakili huyo, alisema kulingana na kiapo cha mleta maombi, barua inayoelezwa ilipatikana kupitia mitandao ya kijamii hivyo mahakama haiwezi kufanyia kazi maombi hayo, labda kama kuna uhakika kuna maamuzi hayo.
Wakili huyo alisema kwa kuwa hakuna uhakika kama kuna uamuzi huo umefanywa na Msajili, maombi hayo yameegemea katika uvumi na yamefunguliwa kabla ya muda, hivyo kuyashughulikia ni kupoteza muda.
Hivyo wakaiomba Mahakama iyatupe maombi hayo kwani uamuzi wowote utakuwa ni batili na hauwezi kuwa na nguvu ya kisheria, hivyo Mahakama na muombaji ayafungue pindi atakapopokea rasmi barua ya Msajili.
Akijibu hoja hizo, wakili Kibatala alisema mawakili wa Serikali wamejielekeza vibaya katika pingamizi hilo kwa kuwa halihusiani na suala la mamlaka ya Mahakama na wametoka nje kabisa ya misingi ya pingamizi la awali.
Wakati Kibatala akikiri barua ya kufuta kanisa hilo iko kwa jina tofauti na la muombaji, haijasainiwa na wala muombaji hajapewa rasmi, alisema hoja hizo tatu ndizo ambazo zinapaswa kufanyiwa kazi na kutolewa uamuzi na waziri katika rufaa waliyoikata kwake.
Malalamiko ya msingi ya muombaji katika rufaa kwa waziri ni kwamba ingawa mlalamikaji siye anayetajwa katika anuani ya barua, utekelezaji wake umemwathiri moja kwa moja baada ya IGP kusimamia utekelezaji huo.
Kibadala alisema mjibu maombi wa tatu ambaye ni IGP amezuia shughuli za muombaji na kuwakamata na kuwaweka kizuizini baadhi ya waumini na kukiuka kabisa hali ya kikatiba ya waumini hao kuabudu.
Hivyo Kibatala alisema maombi ya zuio la waombaji ili wajibu maombi waache shughuli ziendelee kama kawaida ni muhimu katika hatua hiyo.
Uamuzi wa Jaji
Katika uamuzi wake, Jaji alisema amesikiliza hoja za kisheria za pande zote mbili na anaona kuwa hoja inayopaswa kuamuliwa na Mahakama yake ni kama mahakama hiyo ina uwezo wa kusikiliza na kuamua kuhusu maombi hayo.
Jaji alisema katika pingamizi hilo, Wakili Kibatala ameialika Mahakama kuona kuwa hoja zilizoibuliwa na wajibu maombi haihusiani na pingamizi la awali, kwa vile imebeba maelezo ambayo yanahitaji kutolewa ushahidi kisheria.
“Pingamizi lililoko mbele yangu linahusu mamlaka ya Mahakama hii. Nimepitia hoja zilizowasilishwa na wakili wa Serikali kuhusu pingamizi la awali, lakini hakunukuu sheria yoyote au msimamo wa kisheria kuunga mkono pingamizi.”
Alisema wasilisho lake linaonyesha Mahakama ina uwezo wa kusikiliza maombi kuhusu zuio la muda chini ya kifungu namba 2(3) cha sheria inayosimamia maombi ya aina hiyo.
Jaji Masabo amesema hata hivyo, kwa kuchambua hoja za wakili Methodi ameshindwa kuelewa ni kwa namna gani mamlaka ya Mahakama hii imeondolewa.
Amesema hoja kwamba barua ina jina tofauti na mwombaji, na kwamba haijawasilishwa rasmi, zinazohusu uwezo wa mwombaji kufungua shauri na kiini cha madai na si suala la mamlaka ya Mahakama.
"Kwa hayo yote, pingamizi la awali linatupwa bila gharama,” alisema Jaji Masabo.