Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Waumini wa Askofu Gwajima wasali nyumbani, ndoa na ubatizo zaahirishwa

Muktasari:

  • Juni 2, 2025, Msajili wa Jumuiya za Kiraia, Emmanuel Kihampa alitangaza kulifuta Kanisa la Ufufuo na Uzima kwa kile alichokieleza limekiuka Sheria ya Jumuiya Sura ya 337, kwa kutoa mahubiri yenye mwelekeo wa kisiasa.

Dar es Salaam. Kufuatia kufutwa usajili wa Kanisa la Ufufuo na Uzima linaloongozwa na Askofu Josephat Gwajima, uongozi wa kanisa hilo umetangaza mabadiliko ya ibada ikitaka zifanyike nyumbani huku ikiahirisha ndoa na ubatizo.

Uongozi wa kanisa hilo umetoa taarifa hiyo baada ya Serikali kupitia kwa Msajili wa Jumuiya za Kiraia, Emmanuel Kihampa kutangaza kulifuta kanisa hilo kwa kile alichoeleza limekiuka Sheria ya Jumuiya Sura ya 337, kwa kutoa mahubiri yenye mwelekeo wa kisiasa na nia ya kuichonganisha Serikali na wananchi.

Kihampa alitangaza kuchukua hatua hiyo Juni 2, 2025 siku chache tangu Askofu Gwajima kukutana na waandishi wa habari kuzungumzia matukio ya kutoweka na kutekwa kwa watu, huku akitoa mfano wa hali ingekuwaje iwapo matukio hayo yangewakuta watoto wa viongozi akiwemo yeye mwenyewe.

Askofu Gwajima alifafanua maelezo yake ambayo yaliibua mijadala ndani na nje ya Bunge. Awamu hii ilikuwa Juni 1, 2025 katika ibada ya Jumapili akidai matukio hayo yapo na yanasikitisha jamii na hatua zinapaswa kuchukuliwa.

Leo Jumapili, Juni 8, 2025, Mwananchi limefika katika Kanisa la Ufufuo na Uzima lililopo Ubungo jijini Dar es Salaam na kukuta ulinzi ukiwa unaendelea kuimarishwa na Jeshi la Polisi ili kuhakikisha hakuna anayeingia wala kutoka.

Gari la washawasha limeegeshwa katika lango kuu. Pilikapilika zile ambazo huwa zinaonekana eneo hilo hususan siku za Jumapili ni tofauti. Ukimya umetanda huku utepe wa kuzuia watu kuingia ukiendelea kuwapo tangu ulivyowekwa siku ya kwanza.

Baadhi ya waumini wa kanisa hilo wamezungumza na Mwananchi wamesema wameshapewa maelekezo kupitia makundi sogozi (WhatsApp) kuendelea na ibada katika maeneo yao.

Kelvin Mndemi, mkazi wa Ubungo Kibo amesema walishapewa mwongozo tangu Ijumaa hivyo wameendelea na ibada zao kama kawaida na Jumapili ya leo wamekutana huko.

"Baada ya kukatazwa kuingia kanisani tuliwauliza viongozi wanaotusimama kuhusu hatima yetu na wao walisema wanasubiri mwongozo kutoka kwa viongozi wakuu na Ijumaa tuliambiwa tusali nyumbani na vituoni kwetu tukisubiri uamuzi sahihi," amesema Mndemi.

Amesema kwa wale waliokuwa wanahitaji kufunga ndoa na kubatizwa wameambiwa wasubiri viongozi watakuja na uamuzi utakaowasaidia kutimiza takwa la Mungu.

Mwingine ni kiongozi ambaye hakutaka kutajwa jina lake amesema wamekutana katika vituo vyao lakini mwitikio umekuwa mdogo tofauti na awali kutokana na wengi wao kuamini, kuwepo kanisani kuna kitu wanapokea tofauti na nyumbani.

"Kanisani kuna maana yake na nyumbani vivyo hivyo mazoea ya kuwepo kiongozi mkuu kwenye ibada inaleta nguvu ndani ya waumini leo kusali nje ya kanisa inatupa ugumu kidogo," amesema.

Jana Jumamosi, Juni 7, 2025 Katibu wa kanisa hilo, Dk Eric Shoo kupitia mitandaoni alirusha taarifa za kinachoendelea baada ya kanisa lao kufutwa akitoa maelekezo kwa maaskofu, wachungaji na waumini.

"Siku ya kesho (leo) Jumapili Juni 8, 2025 hapatakuwa na ibada katika makanisa yetu yote ya Glory Christ Tanzania kwa hiyo kila mshirika wa kanisa letu afanyie ibada nyumbani kwake," amesema.

Amesema anafahamu ratiba ya kanisa lao kuna mambo mengi yalitakiwa kufanyika leo kama kufunga ndoa, ubatizo, ibada za meza ya bwana na kubariki watoto na mambo mengine: “Matukio yote haya yameahirishwa mpaka tutakapowafahamisha tena.”

Amewaagiza maaskofu wa majimbo makuu yote manane ya Tanzania na maaskofu wote wa majimbo 33, waangalizi wa divisheni, makuhani wa sehemu, waamuzi wa maeneo na walawi wa vituo wa Tanzania kutekeleza maelekezo hayo kwa bidii.

Pia, amemuagiza mkuu wa utawala wa fedha kuwafahamisha wakurugenzi wa fedha wa majimbo yote na wakuu wa idara kusimamia utekelezaji wa shughuli hii kwa bidii kwenye majimbo yao yote.

"Maelekezo haya yanahusu makanisa yetu yaliyopo Tanzania, yaliyopo nje ya nchi yaendelee na taratibu kama zilivyopangwa," amesema Dk Shoo.

Katibu Mkuu huyo amehitimisha taarifa yake akiwaomba waumini wa kanisa hilo kusoma Wakoronti 15:58 akinukuu ‘Kwa hiyo ndugu zangu, simameni imara. Msitikisike. Mzidi sana kujitoa kwa ajili ya kazi ya Bwana, kwa maana mnajua ya kuwa, juhudi yenu si bure katika Bwana.”

Aidha, kufutwa kwa kanisa hilo kumeacha kilio kwa wafanyabiashara jirani na kanisa hususan wa chakula, waendesha bodaboda, wauza vinywaji baridi na madaftari wakisema ibada za kila siku na za mwisho wa wiki zilihudhuriwa na waumini wengi ambao walikuwa wateja wao.

Asha Mtemi, mama lishe mwenye banda jirani na kanisa hilo akizungumza na Mwananchi jana Jumamosi alisema siku za Jumapili alikuwa na uhakika wa biashara kuanzia asubuhi hadi jioni na alikuwa akipata faida hadi SH120,000 akitoa mtaji na siku za kawaida Sh70,000 na kwa sasa hali imekuwa ngumu.