Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kufungwa kanisa la Gwajima wafanyabiashara walia ukata

Viti vikiwa vimepangwa ndani ya Kanisa la Askofu Gwajima, lililopo eneo la soko la Maimoria, Manispaa ya Moshi Mkoani Kilimanjaro.

Muktasari:

  • Msajili wa Jumuiya za Kiraia, Emmanuel Kihampa Juni 2, 2025 alitangaza kulifuta Kanisa la Ufufuo na Uzima akieleza limekiuka Sheria ya Jumuiya Sura ya 337.

Dar es Salaam. Baada ya Serikali kufuta usajili wa Kanisa la Ufufuo na Uzima linaloongozwa na Askofu Josephat Gwajima, baadhi ya wafanyabiashara jirani na kanisa lililopo Ubungo, Dar es Salaam wanakuna vichwa, wakieleza biashara zao zimeyumba.

Msajili wa Jumuiya za Kiraia, Emmmanuel Kihampa Juni 2, 2025 alitangaza kulifuta kanisa hilo akieleza limekiuka Sheria ya Jumuiya Sura ya 337: “Kwa kutoa mahubiri yenye mwelekeo wa kisiasa na nia ya kuichonganisha Serikali na wananchi,” amesema.

Baadhi ya wafanyabiashara wa vinywaji baridi, madaftari, kalamu, chakula, wamiliki wa saluni na waendesha bodaboda waliozungumza na Mwananchi leo Juni 6,  wanasema ibada za kila siku na za mwisho wa wiki zilihudhuriwa na waumini wengi waliokuwa wateja wa bidhaa na huduma zao.

Asha Mtemi, mama lishe mwenye banda jirani na kanisa hilo amesema: “Jumapili nilikuwa na uhakika wa biashara kuanzia asubuhi maana waumini wanaanza misa saa mbili asubuhi, nilikuwa napata hadi Sh120,000 nikitoa mtaji, siku za kawaida nilikuwa na uhakika wa kupata Sh70,000,” amesema.

Amesema kwa sasa hakuna waumini hivyo wateja wanaokwenda kwake ni mafundi wa magari na waunga vyuma ambao wengine amesema huwa wakimkopa na kulipa baadaye.

Asha amesema amelazimika kupunguza kipimo cha chakula asubuhi na mchana kutokana na wateja kupungua.

Wachuuzi wa madaftari, kalamu na pipi nje ya geti la kanisa hilo pia wanalalamika kukwama kwa biashara.

“Siwezi kusema sana inabidi nikae kimya tangu siku ya kwanza nilivyoona hali hii niliwaza hatima ya biashara yangu ambayo imekuwa ikiniingizia kipato, lakini hali ni mbaya na tofauti na ilivyokuwa awali,” amesema mfanyabiashara ambaye hakutaka kutajwa jina akieleza uwepo wa askari polisi eneo hilo pia unawapa woga.

Madereva wa bodaboda kwa upande wao wanasema wamepoteza wateja waliokuwa wakilipa Sh1,000 kwenda kanisani hapo.

Dereva wa bodaboda Salim Jabir anasema: “Kukosekana kwa huduma hapa kumetuathiri na si sisi wa kijiwe hiki hata wengine ambao walikuwa wanaleta waumini kutoka maeneo mbalimbali.”

Amesema baadhi yao wamehamia kwenye vituo vya daladala vya Kibo na Ubungo Maji baada ya Jeshi la Polisi kuwaeleza hawapaswi kuwapo jirani na kanisa hilo.

Wenye saluni za kike nao wanaeleza kukosa wateja waliokuwa wakiwahudumia jirani na kanisa hilo.

Wauzaji wa soda, maji na juisi wanasema Jumapili na siku za mikutano ya maombezi walikuwa wakipata mapato zaidi.

“Tulikuwa tunauza soda na maji kila siku kutokana na uwepo wa ibada za maombezi na mikesha, hata miamala ya pesa ilikuwa inaonekana kwa sasa hali ni mbaya wateja ni wa kuvizia,” amesema Anneth Leo.