Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Dk Nchimbi atoa maagizo wizara ya Bashe, wakala wa mbegu

Muktasari:

  • Ziara ya Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Dk Emmanuel Nchimbi imeingia siku ya pili mkoani Ruvuma na kutoa maagizo mbalimbali yenye lengo la kuondoa changamoto za wakulima.

Namtumbo. Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk Emmanuel Nchimbi ameiagiza Wizara ya Kilimo kuongeza kasi ya utafiti na uzalishaji mbegu za alizeti ili wananchi na Taifa liondokane na uagizaji mafuta ya kupikia nje ya nchi.

Mtendaji mkuu huyo wa CCM ameutaka Wakala wa Mbegu za Kilimo Tanzania (ASA) kuhakikisha inafungua maduka maeneo mbalimbali nchini ili kuwapunguzia adha wakulima.

Amesema wakulima nchini wakipatiwa mbegu bora na zenye uhakika kwa bei nafuu, itachangia kuongeza tija ya uzalishaji wa mafuta ya kupikia na nchi itakuwa na uhakika wa upatikanaji bidhaa hiyo.

Dk Nchimbi ametoa maelekezo hayo leo Alhamisi, Aprili 3, 2025 alipokuwa wilayani Namtumbo, Mkoa wa Ruvuma kwa nyakati tofauti akiendelea na ziara ya siku tano mkoani humo.

Ameanza kutoa maagizo hayo wakati akikagua shamba la uzalishaji mbegu za mahindi na alizeti, linalisimamiwa na Wakala wa Mbegu za Kilimo Tanzania (ASA) kwa kushirikiana na Jumuiya ya Wazazi wa CCM.

Mgombea huyo mwenza mteule wa CCM akasisitiza maelekezo hayo wakati akihutubia mkutano mkubwa wa hadhara uliofanyikia Shule ya Msingi Namtumbo.

Baada ya kupokea maelezo ya Mtendaji Mkuu wa ASA, Leo Mavika juu ya wanachokifanya, Dk Nchimbi akaamua kutoa maagizo kwa Wizara ya Kilimo ambayo inaongozwa na Waziri, Hussein Bashe.

“Wizara iendelee kuongeza nguvu katika kuhakikisha uzalishaji mbegu unaimarishwa na wakulima wetu wapate mbegu kwa bei nafuu zenye ubora ili tija ipatikane na tuhakikishe kilimo cha alizeti kinapewa kipaumbele kuanzia uzalishaji mbegu hadi ukamuaji mafuta, ili nchi ijitegemee katika uzalishaji mafuta ya kupikia," amesema Dk Nchimbi

Dk Nchimbi amesisitiza: "Siyo heshima kabisa kwa nchi kutegemea kuagiza mafuta ya kula kutoka nje ya nchi wakati tunaweza kuimarisha kilimo cha alizeti kupitia upatikanaji mbegu kisha kuongeza tija katika uzalishaji mafuta ya kula.”

Amesema chama hicho kinahitaji mkulima afanikiwe kwa kupata mbegu bora zitakazosaidia kuongeza uzalishaji mazao na kupunguza gharama za uzalishaji shambani.

Katika mkutano wa hadhara, Dk Nchimbi amesema lengo la ziara hiyo ni kuangalia uhai wa chama na kama Serikali inatekeleza vyema maelezo ya chama hicho.

Amesema hivi karibuni alimtembelea Mama Maria, mjane wa baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere jijini Dar es Salaam na katika maelezo yake Mama Maria alisisitiza nchi kuendelea kujitosheleza kwa chakula.

"Mama Maria akasema, ni heshima ya nchi kujitosheleza katika chakula, Tanzania kwa miaka 10 mfululizo imejitosheleza kwa chakula na akasisitiza tuilinde heshima hii," amesema

Akijenga hoja, Dk Nchimbi amesema anaipongeza Wizara ya kilimo na ASA kwa kuongeza uzalishaji wa mbegu: "Huyo ni wakala wa Serikali ambaye anapunguza bei ya mbegu na Serikali ya CCM lazima irahisishe maisha ya wananchi."

"Nataka kutoa maelekezo, kwanza kutekeleza ahadi ya kufungua maduka ya mbegu maeneo mbalimbali nchini sawa na uzalishaji wa mbegu. Sisi kama chama tutaendelea kusimamia upatikanaji wa mbegu na masoko," amesema Dk Nchimbi.


Maelezo ya ASA

Mtendaji Mkuu wa ASA, Leo Mavika akitoa maelezo kwa Dk Nchimbi amesema wakala huo unazalisha mbegu za mazao 13 ambayo Wizara ya Kilimo imeyapa kipaumbele katika kusaidia nchi kujitosheleza kwa chakula na kibiashara.

Mavila amesema shamba hilo la Namtumbo linazalisha mbegu za mahindi na alizeti ambazo baada ya kuzalishwa zinauzwa kwa bei nafuu kwa wakulima.

Amesema kilo moja ya mbegu za mahindi wanauza Sh3,500 wakati wazalishaji binafsi wanauza kati ya Sh15,000 hadi Sh16,000. Amefafanua kuwa mbegu za alizeti kwa kilo moja wanauza  Sh6,000 wakati wazalishaji kawaida wanauza hadi Sh20,000.

 Mavika amesema shamba hilo lenye ukubwa wa hekta 6,850, hekta 19,000 zinafaa kwa uzalishaji mbegu, hata hivyo eneo linalotumika ni hekta 12,000.

 “Hekta 3,308 zimegawiwa kwa wananchi katika shughuli za mashamba na makazi. Tumebakiwa na hekta 3,500. Katika eneo hilo ASA tuna uwezo wa kuzalisha mbegu tani 4,402 katika msimu huu wa kilimo,” amesema.

 Amesema tayari wakala huo umenunua mtambo wa kuchakata mbegu utakaofungwa katika eneo hilo, hatua ambayo itasaidia kupunguza gharama za uzalishaji, kushusha bei ya mbegu na kuzalisha ajira kwa wananchi.

Mavika amesema watajenga eneo la kuhifadhi mbegu kupatikana unyevunyevu unaohitajika, kupanua ghala la kuhifadhi mbegu na kufunga mfumo wa umwagiliaji katika mashamba.


Alichokisema Vita Kawawa

Mbunge wa Namtumbo (CCM), Vita Kawawa akizungumza katika mkutano wa hadhara amesema jimbo hilo limepiga hatua kwenye sekta ya afya, elimu ikiwemo ujenzi wa shule tano za sekondari na madarasa 207 yamejengwa.

Kawawa amesema vifo vya mama na mtoto vimepungua (hakutaja takwimu) na hiyo ni jitihada za Serikali kuhakikisha huduma za afya kwa wananchi zinakuwa fanisi na bora.

"Kuna shida ya maji hapa Namtumbo na Mama (Rais Samia Suluhu Hassan) nilimuomba na nimepatiwa fedha na mkandarasi anaweza kupatikana kabla ya Mei 2025," amesema Kawawa.

Aidha, changamoto nyingine ni kukosekana kwa soko na stendi mambo ambayo amemwomba Dk Nchimbi kuyabeba na kwenda kuyatafutia ufumbuzi ili wananchi waweze kusogezewa huduma.

Akizungumza changamoto hizo, Dk Nchimbi amesema:"Niielekeze Serikali ifuatilie jambo hili na kujua wananchi wa Namtumbo wanataka kuwa soko na stendi na mimi nitakuwa nawaunga mkono katika hili. Kuhusu barabara tutaendelea kuzifanyia msukumo wa kipee hadi zipatikane."


Ujuvi wa Joram Nkumbi

Msaidizi wa Ofisi ya Katibu Mkuu wa CCM, Joran Nkumbi amesema wananchi wanahitaji huduma bora za afya, elimu, teknolojia na mambo mengine ya kwenda katika ulimwengu wa sayansi.

Nkumbi ambaye ni mjuvi wa lugha ya Kiswahili akizungumza huku akishangiliwa kutokana na uhodari wa matumizi ya lugha hiyo amesema mambo yote ya maendeleo yatafanyika na wananchi wanapaswa kukipa nafasi chama hicho:"Ili watupeleke kwenye nchi ya asali na maziwa."