Dk Nchimbi kuanza ziara Ruvuma, mgeni rasmi mkutano wa wahariri

Muktasari:
- Mtendaji Mkuu wa chama tawala nchini Tanzania- Chama cha Mapinduzi (CCM), Dk Emmanuel Nchimbi anaanza ziara ya kukagua utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya mwaka 2020/25 katika mkoa wa Ruvuma.
Masasi. Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Dk Emmanuel Nchimbi leo Jumatano, Aprili 2, 2025 anaanza ziara ya kikazi ya siku tano mkoani Ruvuma.
Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa na CCM imeeleza ziara hiyo ya kukagua utekelezaji wa ilani ya CCM 2020/25, mtendaji mkuu huyo wa chama hicho tawala atakagua miradi ya maendeleo na kuzungumza na wananchi na wanachama wa chama hicho.
Dk Nchimbi ataanza ziara hiyo leo Jumatano baada ya kuwasili kwa ndege katika Uwanja wa Ndege wa Masasi mkoani Mtwara akitokea jijini Dar es Salaam.
Ambapo pamoja na mambo mengine atazungumza na wananchi, wanachama na viongozi mbalimbali watakaokuwa wamejitokeza kumpokea. Kisha ataelekea Tunduru, mkoani Ruvuma ambapo atakagua miradi ya maendeleo na kufanya mkutano wa hadhara.
Katika siku ya pili ya ziara hiyo, kesho Alhamisi, Aprili 3, 2025 Dk Nchimbi ambaye pia ni mgombea mwenza mteule wa urais wa CCM atakuwa na mkutano Namtumbo.
Aprili 5, 2025, Dk Nchimbi mwenye miaka 53 atakuwa wilayani Nyasa na atahitimisha ziara yake Aprili 6, 2025 Songea Mjini ambapo atafanya mkutano wa hadhara.
Ziara hiyo ni mwendelezo wa viongozi waandamizi wa CCM maeneo mbalimbali. Ni hivi karibuni Makamu Mwenyekiti wake Bara, Stephen Wasira alihitimisha mkoani Simiyu baada ya kupita mikoa ya Songwe, Mbeya, Kagera na Shinyanga.
Aidha, Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Amos Makalla alifanya ziara mikoa mwili ya Mbeya na Iringa. Ziara zote zinalenga kukiandaa chama hicho kuelekea uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba 2025.
Ziara hii ya Dk Nchimbi ni ya kwanza tangu wajumbe wa mkutano mkuu wa CCM walipompitisha kuwa mgombea mwenza mteule wa urais Januari 19, 2025 jijini Dodoma.
Pia, wajumbe hao walianza kwa kuwateua Rais Samia Suluhu Hassan kuwa mgombea urais na Dk Hussein Mwinyi kutetea nafasi ya urais upande wa Zanzibar.
Siku hiyo, Mwenyekiti wa CCM, Rais Samia alisema Dk Nchimbi ataendelea na majukumu yake ya ukatibu mkuu licha ya kuwa ni mgombea mwenza mteule wa irais.
Mkutano wa wahariri
Pamoja na mambo mengine, Dk Nchimbi akiwa mkoani Ruvuma, atakuwa mgeni rasmi katika mkutano mkuu maalumu wa uchaguzi wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) unaoanza Alhamisi Aprili 4-5, 2025, Songea Mjini.
Katika uchaguzi huo, wajumbe wa TEF watawachagua mwenyekiti, makamu mwenyekiti pamoja na wajumbe wa kamati ya utendaji.
Deodatus Balile, ni mgombea pekee wa nafasi ya uenyekiti anayetetea kwa miaka minne mingine, sawia na Bakari Machumu anayetetea umakamu.
Shughuli kwenye uchaguzi huo unaotarajiwa kuwa kwenye nafasi za ujumbe wa kamati ya utendaji kwani waliojitosa ni 12 na wanaotakiwa ni saba. Wote hao kila mmoja anapambana kivyake kuhakikisha anaibua mshindi.
Wanaochuana kwenye kinyang'anyiro hicho ni, Reginald Miruko, Anna Mwasyoke, Tausi Mbowe, Angelina Akilimali, Jane Mihanji, Salim Said Salim, Bakari Kimwanga, Peter Nyanje, Yasin Sadiq, Stella Aron, Esther Zelamula na Joseph Kulangwa.