Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Chaumma sasa kuzindua ziara ya 'chopa' Juni 3

Naibu Katibu Mkuu wa Chaumma, Benson Kigaila akizungumza na Waandishi wa habari jijini Mwanza. Picha na Peter Saramba.

Muktasari:

  • Chaumma kimejizolea umaarufu kwenye uwanja wa siasa nchini Tanzania baada ya kupokea wanachama wapya ambao baadhi walikuwa viongozi wa juu wa Chadema walilkuwa kwenye kundi la G55 ambao baadhi sasa ni viongozi wakuu wa Chaumma.

Mwanza. Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma) kimesogeza mbele uzinduzi wa mikutano yake ya siku 16 ya kujitambulisha na kupokea wanachama wapya kutoka Juni Mosi, 2025 hadi Juni 3, 2025 baada ya kukosa vibali vya kurusha 'chopa' na uwanja wa mkutano wa uzinduzi.

Akizungumza na Waandishi wa habari jijini Mwanza leo Mei 29, 2025, Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho (Bara), Benson Kigaila amesema hadi leo, vibali vya kurusha chopa na matumizi ya uwanja wa Furahisha jijini Mwanza  havijapatikana kutoka mamlaka husika.

"Tulitangaza kufanya ziara ya siku 16 katika mikoa yote ya Tanzania kwa kuanza na uzinduzi uliopangwa kufanyika jijini Mwanza Juni Mosi, 2025, lakini tumesogeza mbele tarehe ya uzinduzi kutokana na sababu kuu mbili; kwanza hatujapata kibali cha kurusha chopa na pili ni upatikanaji wa viwanja kwa sababu hadi leo hatujapata majibu ya kibali cha kurusha chopa na kutumia uwanja wa Furahisha tunayotarajia kufanya mkutano wetu wa uzinduzi," amesema Kigaila

Amesema wakati wakiendelea kufuatilia  kibali cha kuruka kwa chopa, uongozi wa chama hicho unafanya tathmini ya viwanja vingine vinavyofaa kwa mkutano wa uzinduzi iwapo uwanja wa Furahisha hautapatikana.

"Baada ya mkutano wa uzinduzi jijini Mwanza, Juni 4, 2025, viongozi wote wa kitaifa wa chama hicho akiwemo Mwenyekiti, Hashim Rungwe watatawanyika kwa ajili ya ziara ya kukitambulisha chama na kupokea wanachama wapya katika mikoa ya Simiyu, Mara, Manyara Dodoma na Singida.

Mikutano mingine ya chama hicho kilichopata umaarufu baada ya  kupokee makada wapya kutoka Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) itafanyika katika mikoa ya Tabora, Shinyanga,  Geita, Kagera, Kigoma, Rukwa, Katavi, Songwe,  Mbeya, Njombe, Tanga,  Morogoro, Kilimanjaro na Arusha watakapohitimishia ziara Juni 16, mwaka huu.

"Tunatoa wito kwa wananchi wafike kwenye mikutano yetu kusikiliza sera na ajenda yetu  ambayo ni kusimama na umma kwa kuwasemea kuhusu shida zao na kuwaunganisha bila kujali tofauti zao kiitikadi ili kupambana na Chama Cha Mapinduzi (CCM) kudai maisha na huduma bora za kijamii," amesema Kigaila.

Naibu Katibu Mkuu huyo ametoa mfano wa kukosekana kwa huduma ya uhakika ya majisafi na salama kwa wakazi wa Jiji la Mwanza kuwa miongoni mwa hoja zitakazotumiwa na Chaumma kuhamasisha umma kukiondoa madarakani CCM.

"Jiji la Mwanza iko pembezoni mwa Ziwa Victoria, lakini huduma ya majisafi na salama bado ni tatizo chini ya miaka 64 ya Uhuru chini ya uongozi wa Serikali ya CCM. Hoteli niliyofikia hakuna maji tangu juzi, jana na hata leo," amesema kiongozi huyo aliyewahi kuwa Naibu Katibu Mkuu (Bara) wa Chadema.

Akizungumzia ujio wa Chaumma katika uwanja wa siasa nchini Tanzania, Halima Abdulkarim, mkazi wa Mtaa wa Nyabulogoya jijini Mwanza amesema japo umma unajiuliza nguvu na ushawishi wa ghafla wa chama hicho, ujio huo una manufaa kwa sababu unaongeza idadi ya vyama vitakavyotoa ushindani kwa CCM zaidi ya Chadema iliyozoeleka kuwa ndicho chama kikuu cha upinzani.

"Binafsi sikuifahamu sana Chaumma zaidi ya yule kiongozi wake (Mwenyekiti Hashim Rungwe) aliyejizolea umaarufu kwa sera yake ya ubwabwa; lakini sasa kimekuwa maarufu na ni jambo jema kwa maendeleo na ustawi wa siasa," amesema Halima.

Amesema umma una haki ya kuhoji ulikopata ukwasi wa kufanya mikutano nchi nzima tofauti na miaka ya nyuma, lakini siyo jambo baya Taifa kuwa na vyama vya upinzani zaidi viwili vyenye nguvu kukichagiza CCM iliyozoea kupata ushindani kutoka kwa Chadema pekee.


'No reforms, No election'

Akijibu swali la yeye na wenzake waliohamia Chaumma wakitoka  Chadema kubadili msimamo kuhusu kudai mabadiliko ya sheria na mfumo wa uchaguzi, Kigaila amesema bado wanaamini katika mapambano ya kuunganisha nguvu ya umma kudai madadiliko kwa kushiriki uchaguzi, kushinda nafasi za kisiasa na tumia majukwaa rasmi ikiwemo Bunge kudai na kufanya mabadiliko.

"Ni kweli kabla ya Chaumma nilikuwa Chadema na nilinadi ajenda ya 'No reforms, No election' ambayo ililenga kuchagiza na kushinikiza mabadiliko, kwa mujibu wa Kamati Kuu ya Chadema. Lakini dhana ya kaulimbiu hiyo haikuwa kuzuia uchaguzi kama wanavyosema Chadema kwa sababu tukiwa Chadema, tumeshiriki uchaguzi mkuu wa 2020 na uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2024," amesema Kigaila.

Akifafanua, kiongozi huyo amesema japo ni kweli kunahitajika mabadiliko ya Katiba  kwa kuwa iliyop ina mfumo wa chama kimoja kwa sababu ilitungwa mwaka 1977 wakati mfumo wa vyama vingi umerejea mwaka 1992, siyo chaguo sahihi wala busara vyama vya uoinzani kususia uchaguzi kutokana na ukweli kwamba vineshiriki na kupata madiwani na wabunge kupitia katiba hiyo huyo tangu chaguzi za vyana vingi vilipoanza mwaka 1995.

"Timu ya Soka isiyopeleka timu uwanjani haiwezi kushinda mechi wala kupata kikombe, sisi Chaumma tunapeleka timu uwanjani.”

Bila kukitaja Chadema, Kigaila amewataka wanaotangaza kuzuia uchaguzi hadi mabadiliko yafanyike kuueleza mikakati itakayotumika kufanikisha lengo hilo ili umma uwaamini na kuwaunga mkono.

Kuwalipa fedha wanaohudhuria mikutano

"Mtu yeyote mwenye kompyuta yake anaweza kuandaa na kusambaza fomu mitandaoni kuanza propaganda kuwa Chaumma inawalipa fedha watu ili wahudhurie mikutano yetu; watu wachunguze na kuthibitisha iwapo watakutana na hizo fomu za malipo huko mitaani," amesema.

Kigaila na wenzake kadhaa ambao awali walikuwa makada wa Chadema wamehamia Chaumma ambako pia wameteuliwa kushika nyadhifa za Kitaifa.

Wakati Kigaila akiukwaa nafasi ya Naibu Katibu Mkuu (Bara), Salum Mwalimu yeye amekuwa Katibu Mkuu huku Devotha Minja akikaimishwa nafasi ya Makamu Mwenyekiti (Bara).