Prime
Huu hapa mkakati wa kuisuka upya Chaumma

Dar es Salaam. Baada ya kufuru ya mikutano katika kumbi ghali na kupokea maelfu ya wanachama, mwelekeo wa Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma) kwa sasa ni kukisuka upya chama hicho, kifikie hadhi ya kuwa chama kikuu cha upinzani.
Kwa mujibu wa Naibu Katibu Mkuu Bara wa chama hicho, Benson Kigaila, ingawa Chaumma ina umri mdogo tangu kilipoanzishwa mwaka 2013, kina malengo, mifumo, itikadi na mafunzo yanayoonyesha ukomavu wake.
Chama hicho kimepokea wanachama wapya zaidi ya 1,000 waliotokana na wanamuungano wa G55 waliokihama Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).

Kigaila, aliyezungumza katika mahojiano maalumu na Mwananchi, anasema kitendo chao cha kuhamia Chaumma ni kama wameihamisha Chadema, ndiyo maana kaulimbiu yao ni ‘tunaendelea tulipoishia’.
Anasema muda uliobaki unatosha kufanya maandalizi ya kuingia katika Uchaguzi Mkuu wa baadaye mwaka huu na kuleta ushindani.
“Watu ni walewale, ndiyo maana nasema tumehamisha chama na kazi tuliyonayo ni watu kule chini kuingia kwenye mifumo ya chama kwa mujibu wa katiba ya Chaumma,” anasema.
Ni bahati nzuri kwa mujibu wa Kigaila, chama hicho kina wanachama wa kutosha na matarajio yao hadi kufikia Juni mwishoni baada ya kumaliza ziara ya C4C watakuwa wamekamilisha mchakato wa kuingia kwenye mifumo ya Katiba ya Chaumma.
“Tutawaunganisha na kuingia kwenye mfumo wa uchaguzi wa Chaumma na tukizunguka tutakuwa tumepata wagombea wote na tutaingia katika uchaguzi na utaona kazi itakayokuwepo,” anasema Kigaila.

Kigaila anasema kupitia ziara hiyo itakayozinduliwa Mwanza Juni Mosi, mwaka huu na kuzunguka mikoa yote Tanzania kwa usafiri wa chopa, watakuwa wanafanya mikutano ya kukusanya watu wao kwa kutumia mfumo wa kuteka na kujenga.
“Hiyo itakuwa mbinu yetu ya vita ya kupigana. Huwezi kupiga mabomu na kuondoka, tutatengeneza mfumo mzuri na tukimaliza uchaguzi, Chaumma kitakuwa chama kikubwa cha upinzani Tanzania,” anasema.
Kigaila anasema Chaumma ina nafuu kuliko Chadema aliyoikuta wakati anajiunga nayo mwaka 2004 akitokea chama cha UDP, anadai mifumo yake haikuwa mizuri, walilazimika kutumia muda mwingi kuunda upya.
Mipango ya kushinda uchaguzi
Ni matumaini ya chama hicho kushinda uchaguzi kwa mujibu wa Kigaila na kwamba wanafanya hivyo tofauti na Chadema, iliyosusa ili kuipa nafasi ya ushindi CCM.

“Kama CCM wametununua utaona moto wetu, tunaenda kusimamisha wagombea majimbo yote 264 na kuongeza mengine mapya yaliyoongezeka 272,” anasema.
Tumedhamiria kurusha chopa
Kigaila anasema chopa ndio usafiri utakaotumika katika ziara ya kampeni ya C4C, huku akihoji wanaowauliza wametoa wapi fedha za kutumia usafiri huo kwanini hawakuuliza ilivyofanyika wakiwa Chadema.
“Chadema tulikuwa tunarusha chopa hatukuwahi kuulizwa fedha tunatoa wapi? Tumehamisha chama tumeleta Chaumma tukirusha chopa unatuuliza tunarusha fedha tumetoa wapi?” anahoji.
Anasema gharama za kurusha Helikopya ni Sh1.5 milioni kwa saa, hivyo ni gharama nafuu zaidi ya kutumia magari.

Anasema mafuta ya ndege ni bei nafuu kuliko mafuta ya magari inatumia mafuta ya taa A1 na watatumia siku 16 mfululizo na watatengeneza ratiba nzima.
Kuhusu mgombea urais
Kigaila anasema bado hawajamuandaa, muda ukifika watakuwa na mtu mwenye sifa hizo za kushindana kwenye nafasi hiyo na kuibuka mshindi.
“Chama kikitangaza utaratibu wanachama watakuwa huru kutia nia, unajua mgombea si mtu mmoja anavyomuona, mgombea kwanza ni yeye kuamua anataka kutia nia alafu chama kitaamua kupitia vikao na katiba yake.
“Uhakika tulionao tutakuwa na mgombea urais wa kushinda uchaguzi, kwa wanachama tulionao awe atakuja awe hayupo, lakini mwisho wa siku tutapata mgombea wa kushinda urais,” anasema.
Awakaribisha kina Mdee
Kigaila anasema kama wabunge 19 wa viti maalumu waliopo bungeni walifukuzwa Chadema, milango iko wazi kujinga na Chaumma wala hawajawekewa mpaka.
“Hata Chadema ukifukuzwa kuna utaratibu wa kuomba kurudi, hakuna wanaofukuza milele, kwa hiyo Chaumma hatukuwafukuza, hatuwezi kukataa kujiunga nao kwa sababu hakuna kosa walilolifanya,” anasema Kigaila.

Anasema anayejisikia kujiunga na Chaumma anakaribishwa kwa mikono miwili kwa kuwa hawajawahi kutenda kosa lolote ndani ya chama hicho.
Ugumu wa Chadema
Kigaila, aliyekuwa na wadhifa kama wa sasa alipokuwa Chadema kwa miaka mitano, anasema ugumu aliokutana nao baada ya kujiunga na Chadema, kwanza iliingia akiwa amebakiwa na miezi michache waingie kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2005.
“Niliposoma Katiba ya chama muundo wake ulikuwa hauhimili uchaguzi kwa sababu ulikuwa na ngazi ya taifa, mkoa, wilaya, kata na ngazi ya tawi na haikuzingatia jiografia, ilikuwa wanachama 60 wanaweza kuunda tawi,” anasema.
Kulingana na mfumo huo, Kigaila anasema kwenye majimbo hakukuwa na muundo wa chama na ilikuwa ngumu kwao kuingia kwenye uchaguzi na kushinda.
“Hakukuwa na muundo kwenye kijiji, mtaa au kwenye kitongoji ambako kuna uchaguzi wa kiserikali kwa sababu tawi lilikuwa ni watu 60 pekee, maana yake hata kijiji kimoja kingeweza kuwa na matawi hata sita, sasa tukajiuliza ni tawi lipi linaweza kuteua mgombea,” anasema.

Anasema jambo hilo lilikuwa pasua kichwa, kwa kuwa walikuwa wanaingia kwenye uchaguzi bila uwezo wa kufanya maboresho ya kikatiba.
“Baada ya uchaguzi 2005 nilipendekeza mabadiliko ya muundo kwa chama na mabadiliko ya Katiba na tuliandika ili kukidhi matamanio na mapambano kwenye vitovu vya uchaguzi kwa kuwa na muundo imara kuanzia taifa, Kanda, Wilaya na tukageuza tawi liwe kijiji, kwa mjini ni mtaa,” anasema.
Alitoka UDP kuingia Chadema
Kigaila anasema Desemba 28, Mwaka 2004 alijunga na Chadema na kutunukiwa wadhifa wa Mkurugenzi wa Oganaizesheni aliyekuwa wa kwanza kukalia tangu kuanzishwa kwake.
Sababu za kukihama UDP na kujiunga Chadema, Kigaila anasema aliona hawawezi kupiga hatua kwenda mbele kwa hoja aliyodai kuwa, alitamani kuona kifanyike kile wanachokubaliana.
“Kulikuwa na ugumu wa kutekeleza na kwa kuwa niliingia kwenye siasa za mageuzi nikiwa na miaka 27, nikaamua kutoka,” anasema.
Anasema alijiunga na Chadema na alipokelewa siku moja na John Mnyika na wakati anahamia alikuwa na wanachama 73 wa UDP kutoka Ukonga. “Niliingia Chadema wakati huo Kurugenzi zikiwa zimeandikwa tu kwenye Katiba, lakini hakuna mtu amewahi kutumikia, ndipo nikaanza kuunda mfumo na kuanza kuufanyia kazi.

“Nimetengeza mifumo na nilishuka chini kijiji kwa kijiji hadi mwaka 2017 nilipoteuliwa kuwa Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama hadi 2019 nilipoteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu Tanzania Bara hadi wadhifa wangu ulipokoma Januari 21, 2025,” anasema Kigaila.
Baada ya kujiunga na Chadema…
Anasema ziara yake ya kwanza ya kujenga Chadema alitumwa kwenda kuandaa ziara ya Mwenyekiti wa wakati huo, Freeman Mbowe Mkoa wa Ruvuma na Iringa, ilikuwa Machi 2005.
“Ziara hiyo ilikuwa kwenye programu iliyopewa jina Chadema ni tawi, nilianzia Songea kwenda kufundisha semina dhana ya chama na sikuwa nimewahi kuhudhuria semina yeyote, ila nilikuwa na Katiba ya chama,” anasema.
Anasema Songea alitangulia kwa muda wa wiki mbili, alizunguka majimbo yote ya mkoa wa Ruvuma kufundisha Chadema ni tawi na kuandaa mazingira ya ujio wa Mwenyekiti.
“Amekuja Mwenyekiti naamka asubuhi natangaza mkutano kuanzia saa 11 alfajiri hadi saa tano Asubuhi, naenda kupaki eneo la mkutano Mbowe inabidi avae nguo watu wasimjue, anakuja kufunga vipaza sauti,” anasema.

Wakati Mbowe anaendelea kufunga, Kigaila alipanda jukwaani kuanza kuhutubia, watu wanakuja kukaa kuanzia saa 5 asubuhi hadi saa 9 alasiri mwenyekiti anapanda anahutubia.
“Tukimaliza tunaunda uongozi palepale, kuwapa kadi na kuondoka, ilikuwa kama siku hiyo hatuna hela tunaenda tunafika kulala kwenye magari, nakumbuka tulifika Iringa tulilala ndani ya gari,” anasema Kigaila.
Kulingana na Kigaila, walikuwa wanalala kwenye magari na Mbowe kwa sababu kwa wakati huo hawakuwa na fedha ya timu yote kwenda kulala nyumba za wageni.
“Na tulikuwa tunakunywa chai asubuhi na kula chakula jioni na tunakubaliana kama ni wali maharage basi ni hivyo na tulifanya kazi hiyo miezi miwili kuanzia Ruvuma, Mbeya hadi Iringa hupewi hata senti tano kupeleka nyumbani au mfukoni,” anasema.
Anasema mhasibu alichokuwa anakifanya, ni kutembea na fedha kwenye begi na wanapokula anakwenda kulipa na nyingine zinatumika kuweka mafuta kwenye magari wanayosafiria.
“Hela zenyewe ni zile tulizochangisha wenyewe, wabunge wamechangia tumeweka pale ili tufanye kazi ya ujenzi wa chama, ndivyo tulivyojenga Chadema,” anasema.
Kulingana na maelezo ya Kigaila, kitanda kimoja walikuwa wanalala wawili ili kuendana na gharama, huku akieleza hakuna kada yeyote wa Chadema anayeweza kufanya shughuli hiyo kwa sasa.
“Hiyo ziara alikuwa mwenyekiti Mbowe, Shaibu Akwilombe akiwa Naibu Katibu Mkuu, wakati ule nilikuwa mimi (Kigaila), mkurungenzi wa Organization, alikuwepo Grace Kihwelu akiwa mbunge wa viti maalumu,” anasema.
Anasema mfumo uliokuwa unatumika, wakurugenzi wote walikuwa wanapewa vitabu vidogo, kuchangisha watu na waliwekewa malengo wafikishe Sh300,000 kila mwezi. “Fedha zilikuwa zinakusanywa na zinaletwa kwenye chama tunalipwa Sh50,000,” anasema.
Kukikuza Chadema…
Kigaila anasema wakati huo Chadema kilikuwa cha sita kwa ukubwa, kikizidiwa na CCM, CUF, NCCR-Mageuzi, TLP na UDP, lakini walipambana hadi kufikia chama kikubwa cha upinzani nchini.
“Tulikikuta kina wabunge watano, lakini hadi 2015 tumekifanya kifikie wabunge 72, tulikuta kina madiwani 45 hadi tumefikisha madiwani 1,108, lakini ruzuku tulipandisha kutoka Sh5.6 hadi Sh360 milioni,” anasema.
Anasema wakati huo waliingia kwenye siasa si kwa sababu walikosa kazi, ingawa waliowengi wanajiunga na vyama baada ya kukosa shughuli za kufanya.
Anasema wakati anafanya uamuzi wa kujiunga na siasa alikuwa anajua machozi na damu, lakini kuna Watanzania wanahitaji kupiganiwa.
“Nikiwa nafundisha Tambaza inakombinesheni zote za sayansi, lakini tulikuwa watu wawili tu tunafundisha, wanafunzi walikuwa wengi, nikianza kufundisha wanafunzi wa kidato cha sita wote wanakuja,” anasema.
Anasema walikuwa wanakuja hadi wanafunzi wa shule jirani, Azania, Jangwani na Mzizima walikuwa wanakuja darasani kwake na alikuwa anafundishia kwenye bwalo la chakula.
“Mwalimu wetu mkuu alikuwa ananifuata siwezi kumaliza matatizo ya walimu, nilikuwa nafanya kazi kubwa lakini nikaona bora nitoke nikafundishe wazazi wao ili wabadilishe serikali ili walimu wapatikane,” anasema.
Anasema hiyo ilikuwa sababu kubwa ya kuacha kufundisha na wala hakuwa kilaza na hata matokeo yake ya kidato cha sita hayakuwa ya kusomea ualimu.
Anasema aliona aache kazi hiyo ili akafundishe wazazi wao wabadilishe Serikali waje na sera ya kuongeza walimu shule na walikuwa wanakosekana kwa sababu ya mfumo wa Serikali inayoongoza.