Chaguzi CCM zinavyotoa mwelekeo wa siasa Tanzania

Muktasari:

Wakati Chaguzi za ndani za Chama cha Mapinduzi zikitoa sura mpya nyingi, wanasiasa na wachambuzi wa masuala kisiasa wanasema chama kinalenga kujisafisha, kujenga taswira mpya na kukiondoa chama katika dhana ya kubebwa na dola.

  

Dodoma. Wakati Chaguzi za ndani za Chama cha Mapinduzi zikitoa sura mpya nyingi, wanasiasa na wachambuzi wa masuala kisiasa wanasema chama kinalenga kujisafisha, kujenga taswira mpya na kukiondoa chama katika dhana ya kubebwa na dola.

Hata hivyo uchaguzi huo unatoa taswira kuwa safu za viongozi waliopatikana ndizo zitakaweza kukivusha kwenye chaguzi za Serikali ya Mitaa mwaka 2024 na Uchaguzi Mkuu wa 2025 ambao tayari Rais Samia Suluhu Hassan amekuwa akipigiwa chapuo.

Chaguzi hizo pia zimeibua hisia za makundi kati ya waliopata kutumika katika nyadhifa mbalimbali kwenye awamu ya tano chini ya Dk John Magufuli na utawala wa sasa chini ya Rais Samia na mzigo mkubwa walionao viongozi ni kuunganisha makundi hayo.

Siasa zinazofanywa na baadhi ya makada wake wakiwemo Dk Bashiru Ally, aliyekuwa Spika wa Bunge Job Ndugai na balozi wa Tanzania nchini Malawi, Humphrey zinatajwa kama mifano ya kuonyesha kuna msuguano wa chini kwa chini.

Dk Bashiru akiwa kwenye mkutano na na wawakilishi wa wakulima, alilitaka kundi hilo liwatishe watawala ili watekeleze mahitaji yao na wasipofanya hivyo hawakuwa tofauti na wanaowapamba na wakati mwingine kuwadanganya kwamba ‘wanaupiga mwingi.’

Kwa upande wake Balozi Polepole, alikuwa na shule yake ya uongozi kwenye mitandao ya kijamii iliyokuwa ikionekana kutokubaliana na hali ya mambo inavyokwenda huku akiusifia utawala wa awamu ya tano.

Kauli ya Rais Samia

Rais Samia Suluhu Hassan aliwahi kusema aliambiwa wanatakaomsumbua siyo vyama vya upinzani bali ni shati la kijani mwenzake.

Rais Samia alitoa kauli baada ya kukerwa na kile alichokisema Spika wa Bunge, Job Ndugai kuhusu Serikali kukopakopa badala ya kujiendesha kwa pesa za ndani.

Kauli hiyo Rais Samia aliitoa Januari 4, 2022 wakati akipokea ripoti ya matumizi ya Fedha za Maendeleo (Fedha za Uviko-19), Ikulu jijini Dar es Salaam.

“Mtu mmoja aliniambia, atakayekusumbua kwenye uongozi wako ni shati ya kijani mwenzio (yaani Mwana-CCM) na sio mpinzani, mpinzani atakutazama unafanya nini, ukimaliza hoja zao hawana maneno, anayetazama mbele 2025 huyu ndiyo atakayekusumbua ndicho kinachotokea.

Kauli ya kuwapo kwa makundi imekuwa ikitawala kila mara ndani na nje ya Bunge lakini viongozi wamekuwa wakitaka umoja ndani ya chama hicho.

Hata hivyo Katibu Mkuu wa CCM, Daniel Chongolo siku chache zilizopita aliwataka wanachama kuacha kuwatumikia watu bali wakitumikie chama.

Baadhi ya viongozi walioangushwa kwenye chaguzi hizo wamekuwa wakitajwa walishindwa kukabiliana na hoja za wapinzani walioonekana kudhibitiwa na kuzuiwa kufanya shughuli zao na waliodiriki kuzifanya walikumbana na mkono wa dola.

Baadhi ya wachumbuzi wa kisiasa waliozungumza na Mwananchi, walisema viongozi wapya watakuwa na jukumu zito la kukabiliana na rushwa ambayo ilisababisha baadhi ya chaguzi kufutwa na nyingine kuahirishwa.

Akizungumzia uchaguzi huo, Katibu Mkuu wa ADA-Tadea na mwanasiasa mkongwe aliyewahi kushika nafasi mbalimbali ndani ya CCM ikiwemo ubunge, John Shibuda, alisema uchafu na usafi wa mwenye nyumba anaoujua ni mwenye nyumba.

“Kitendo cha vigogo kudondoshwa au kutochagulika ni kielelezo cha kwamba wanaoujua usafi na uchafu wa ndani ya jumuiya ni wajumbe ama wanachama. Ndio wanaojua utumishi, faida na shida ya kila mgombea,”alisema.

Alisema waswahili wamekuwa wakisema uzuri wa mtu si sura bali ni matendo na hivyo umaarufu wa majina kama hayana virutubisho yamepauka kwa hiyo ni lazima wananchi wafanye mabadiliko.

Wakili wa kujitegemea, Elias Machibya alisema kiongozi yoyote hupimwa kulingana na utendaji wake katika nafasi aliyoaminiwa na hakuna mwenye hati miliki katika nafasi za uongozi.

“Baadhi ya watu wanajisahau hawawi wanyenyekevu tena, hawatekelezi majukumu yao vizuri tena. Sasa katika zama hizi mwamko ni mkubwa sana ndani ya chama na kwa wananchi kufuatilia utendaji wa viongozi na ndio maana mtu akikosea kidogo habari zinafika mbali sana katika mitandao ya kijamii,”alisema.

Alisema kushindwa kwa viongozi waliotetea nafasi zao kutoe funzo kwa wapya kufanya kazi kwa bidii ili kufikia matarajio ya wanachama na malengo ya chama.

Safu ya uongozi wa CCM inatajwa ndiyo itakuwa na jukumu kubwa la kukitangaza chama hicho na kuwashawishi wasio wanachama wajiunge nacho.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha St John, Dk Shadidu Ndossa, alisema kushindwa katika uchaguzi kwa majina makubwa na wengine kuambulia kura chache kunamaanisha kuwa ukomavu wa chama katika demokrasia.

“Chama kinaruhusu sura mpya kuingia katika uongozi ili kuleta fikra na chachu mpya katika chama. Pia, chama kinaendelea kuwa na mvuto kwa kuwa kuna watu wengi kila wakati wanaamua kuingia katika uongozi wa chama,”alisema.

Kwa mujibu wa katiba ya CCM, Wenyeviti wa Mikoa ni wajumbe wa Halmashauri Kuu Taifa (NEC) na pia wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Taifa.

Pia Wenyeviti wa jumuiya zote ngazi ya Taifa wa UVCCM, UWT na Wazazi ni wajumbe wa Kamati Kuu na NEC ambavyo ni vikao muhimu vya kupitisha maamuzi mazito ya chama.

UWT

Kauli ya Rais Samia kwenye hotuba yake ya ufunguzi wa mkutano wa uchaguzi wa UWT ya kutoshiriki kwa vitendo kutokomeza ukatili kwa watoto na kuhusu kaulimbiu yao, ni viashiria viongozi wa jumuiya hiyo hawakuwa wametekelez a majukumu yao ipasavyo.

Rais Samia pia alizungumzia UWT kushindwa kuingiza wanachama wapya wa jumuiya hiyo kwa kipindi chote walichokaa madarakani. Wanawake ndio wanaaminika kuwa washiriki wakuu kwenye upigaji kura na uhamasishaji kwenye kampeni.

Kupigwa mweleka

Hakuna ubishi mtu unaposhiriki uchaguzi kuna matokeo ya kushinda au kushindwa, ila kwa mtu anayeshiriki uchaguzi wa kutetea nafasi yake anakuwa anaangaliwa kwa jicho la ziada kwani wapiga kura wanakuwa wanajua utendaji wake.

Uchaguzi wa ndani wa CCM kuanzia ngazi ya shina, matawi, wilaya, mkoa hadi jumuiya zake za UVCCM, UWT na Wazazi kwa ngazi ya Taifa umetoa funzo kwa viongozi baada ya kutoa matokeo yanayoonyesha viongozi kadhaa wakipigwa mweleka mpaka wengine wakipata kura chache.

Mfano, waliotetea uenyekiti wa Taifa wa UWT na Wazazi walianguka kwa kupata chache na wengine waliambulia kura moja dhidi ya walioibuka washindi.

Hii si mara ya kwanza kwa vigogo kuangushwa ila tofauti ya kura wanazopigwa nazo ndio zinaweka maswali mbalimbali, je wapigakura wamemuona huyu mwingine ni bora zaidi, je wapiga kura walikuwa wamechoshwa na huyo kiongozi.

Maswali mengine ya kujiuliza je wapiga kura wanachotaka sasa ni mabadiliko tu na walikuwa wanangojea kwa hamu uchaguzi ufike ili wawaondoe waliokuwapo

Viongozi wa UWT

Katika uchaguzi wa Jumuiya ya Wanawake (UWT) Mary Chatanda aliibuka mshindi kwa kupata kura 527 kati ya kura halali 756 zilizopigwa katika uchaguzi huo huku aliyekuwa mwenyekiti wa jumuiya hiyo, Gaudentia Kabaka akipata kura 219.

Matokeo hayo yanafanya Chatanda ambaye aliwahi kushika nafasi mbalimbali ikiwemo ubunge, ukatibu wa CCM Mkoa wa Arusha kumshinda Kabaka kwa kura 308.

Katika uchaguzi huo uliowashirikisha wagombea wengine watatu walipitishwa na Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM (NEC) ulikuwa kati ya Kabaka na Chatanda ambapo hata kampeni zilizokuwa zikipigwa zilionekana kuelekezwa kwa wawili hao.

Uchaguzi huo, uliwaacha wagombea wengine watatu kuambulia ‘namba za viatu’ baada ya aliyekuwa Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam Kate Kamba aliyeambulia kura nane.

Kamba alitupa turufu yake ya mwisho kwenye uchaguzi huo baada ya kuangukia pua katika uchaguzi wa uenyekiti wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam ulimweka madarakani Abbas Mtemvu.

Wengine waliokuwa wakiwania kiti hicho cha UWT, ni Dk Wemael Chamshama, Mariam Lulida wao waliambulia kura moja moja kati ya kura 756 halali zilizopigwa.

Kwa upande wa Jumuiya ya Wazazi, Fadhil Maganya aliibuka kidedea kwa kura 578 kati ya 835 zilizopigwa huku aliyekuwa mwenyekiti wa jumuiya hiyo, Dk Edmund Mndolwa akiambulia kura 64 ikiwa ni karibu ya mara 10 ya kura alizopata mshindani wake.

Wagombea wengine na kura walizozipata kwenye mabano ni Bakari Kalembo (21), Said Mohamed Mohamed (43), Mwanamanga Mwaduga (61), Ally Maulid Othman (57), Ali Khamis Masoud (5), Zahara Hassan Haji (6).

Katika uchaguzi huo, vigogo akiwemo Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dk Angella Mabula na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Adamu Malima walipigwa chini kwenye ujumbe wa halmashauri.

Uchaguzi mwingine ni wa Jumuiya ya Vijana (UVCCM), ambao Mohammed Ali Mohammed (Kawaida) aliibuka mshindi kwa kupata kura 523, Farid Mohammed Haji (25), Kassim Haji Kassu aliyeambulia kura mbili na Abdallah Ibrahim Natepe kura moja.


Yaliyojitokeza

Miongoni mwa mambo yaliyojitokeza kwenye chaguzi hizo ni kura kuhesabiwa kwa muda mrefu ikiwemo katika uchaguzi wa Jumuiya ya Wazazi, zilizoanza kuhesabiwa kwa saa saba baada ya shughuli ya upigaji kura kukamilishwa saa 12:00 jioni.

Mengine ni kwa baadhi ya wajumbe kuanza kutaja majina ya washindi katika chaguzi kabla ya muda wa shughuli ya kupiga kura kuanza katika moja ya mikutano ya uchaguzi.

Mgombea alichaguliwa kushika nafasi ya uenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi, Fadhil Maganya kutamba kuwa ameokota dodo kwenye mti wa mpilipili baada ya kuchaguliwa kuongoza jumuiya hiyo kwa miaka mitano ijayo.