Prime
Chadema yaivaa Polisi, Heche atoa msimamo

Muktasari:
- Makamu Mwenyekiti wa Chadema (Bara), John Heche amesema hawatarudi nyuma katika kudai haki.
Dar es Salaam. Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimesema hakirudi nyuma katika mapambano ya kudai haki, licha ya viongozi na makada wake kukumbwa na kadhia walipokwenda Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kusikiliza kesi inayomkabili Mwenyekiti wa chama hicho, Tundu Lissu.
Chama hicho kimedai miongoni mwa kadhia walizokumbana nazo juzi ni viongozi na makada wao 21 kujeruhiwa, baadhi wakivunjwa miguu na mikono walipokamatwa na Polisi Kanda Malumu ya Dar es Salaam.
Licha ya viongozi wa Jeshi la Polisi kutopatikana jana, kuzungumzia madai hayo, juzi lilithibitisha kuwakamata na baadaye kuwaachia kwa dhamana viongozi na wafuasi watano wa Chadema wanaodaiwa kujihusisha na mkusanyiko katika eneo la Mahakama ya Kisutu, wakati wa usikilizwaji kesi dhidi ya Lissu.

Makamu Mwenyekiti wa Chadema (Bara), John Heche akizungumza na wanahabari leo Ijumaa Aprili 25, 2025, makao makuu ya chama hicho Mikocheni, amesema: "Lissu yupo ndani, sisi tuliobaki hatutarudi nyuma, jambo lolote tulilopanga la chama tulisimamie. Wana Chadema poleni, jifuteni nguo mapambano yaendelee...
"Naomba waelewe hakuna kiwango cha vitisho na udhalilishaji utakaotuzuia au kuturudisha nyuma katika harakati za mapambano ya kudai haki," alisema.
Miongoni mwa mapambano wanayodai Chadema ni mabadiliko ya mifumo ya uchaguzi kupitia ajenda ya No reforms, No election ili kuwapo usawa kwa vyama vyote vitakavyoshiriki uchaguzi mkuu wa Oktoba, 2025.
Heche amesema haijawahi kutokea makamu mwenyekiti wa chama kuzuiwa kwenda mahakamani kufuatilia kesi inayomkabilia mwenyekiti wa chama hicho.
Amesema hawajakata tamaa, akisisitiza: "Natoa wito kwa wanachama wa Chadema, kesi ijayo tutakwenda zaidi na kutakuwa na watu wengi zaidi, hatutafanya fujo."
Katika hatua nyingine, Heche amedai kitendo cha wasaidizi wake kukamatia usukani baada ya kubaini wanapelekwa kusikojulikana ndicho kilichowaokoa, kisha baadaye kuachiwa kwa dhamana na Jeshi la Polisi.
Amedai baada ya kuzuiwa na kukamatwa eneo la Daraja la Selander alizungushwa Bahari Beach na Oysterbay kabla ya kupelekwa kituo cha polisi Kunduchi Mtongani alikoachiwa kwa dhamana.
Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika amedai kitendo cha polisi kumshikilia kwa saa 10 kililenga kumzuia kutekeleza majukumu yake, ikiwamo kwenda mahakamani kusikiliza kesi inayomkabili Lissu.

Mnyika amedai alikamatwa na polisi eneo la Jangwani alipokuwa akielekea Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu. Alidai akiwa kwenye foleni, polisi walikagua magari na walipolifikia alilokuwamo lililokuwa na nembo alitakiwa kufungua mlango, kisha wakatumia nguvu kumshusha kwenye gari hilo.
"Nikaanza kusukumwa kuanzia Jangwani pale bondeni hadi Fire kituo cha mafuta nikaingizwa kwenye gari la polisi, walinipeleka Karume karibu na ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, maelekezo yakatolewa kwamba nipelekwe Mbweni," amedai Mnyika.
Amedai walipofika Magomeni gari liligeuza uelekeo na kurejea Karume, huku mawasiliano yakiendelea kufanyika kwamba apelekwe Kituo cha Polisi Oysterbay.
"Tukafika Oysterbay, gari halikwenda moja kwa moja eneo la mapokezi kwa ajili ya kuandikisha, bali lilienda pembeni, kuanzia saa tatu asubuhi nilikuwa ndani gari hadi saa moja usiku.
"Waliamua kunishikilia nisiende popote, kwa sababu wakati wananichukua hawakuniambia kosa langu," amedai.

Kupitia taarifa kwa vyombo vya habari Aprili 24, Jeshi la Polisi lilisema: “Kazi ya kuzuia vitendo vya kihalifu inaendelea, kwani hilo ndilo jukumu kubwa la msingi la Jeshi la Polisi.”
Polisi liliwataja waliokamatwa kuwa ni Heche, Mnyika, Chacha Heche Seguta, Swezi Dani Naradufu na James Mseti.
“Baada ya mahojiano, dhamana zao ziko wazi. Jeshi linatoa wito kwa wananchi wote kutojihusisha na vitendo vya kihalifu kwani halitakuwa na huruma, lakini litashughulikia kwa kufuata misingi ya kisheria,” ilieleza taarifa.
Jeshi la Polisi lilisema linaendelea na kazi ya kuhakikisha usalama wa Jiji unadumishwa na litachukua hatua kali dhidi ya yeyote atakayejaribu kuvuruga amani, hasa katika maeneo yenye mvutano wa kisiasa.
Taarifa ya Polisi ilisema uwepo wa viongozi hao katika eneo la Kisutu ulikuwa ukifuatilia mwenendo wa kesi ya Lissu, lakini hatua zao zilitafsiriwa kama kikwazo kwa taratibu za usalama zilizokuwa zikiendelea katika eneo hilo.
Kuishitaki Serikali, Kamanda Muliro
Katika hatua nyingine, Heche amesema chama hicho kinajiandaa kuchukua hatua za kisheria dhidi ya Serikali pamoja na Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, SACP Jumanne Muliro.

Alisema matukio ya ukandamizaji wa haki za binadamu yaliyofanywa na Serikali kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi yanapaswa kuwekewa kumbukumbu.
Alisema tayari mawakili wa chama hicho kwa kushirikiana na mawakili wa haki za binadamu wakiwemo wa kimataifa wameanza kuchambua vifungu vya sheria ili kufungua kesi ndani na nje ya nchi.
“Tuna mawakili wa haki za binadamu wako hapa, wanaangalia vifungu mbalimbali kwa kushirikiana na mawakili wetu wa chama ambao, wataanza kukutana na watu wote walioumizwa. Tutaanza na kesi ya Dar es Salaam kisha Mbeya.
Kuanzia leo mawakili wetu wanashughulikia suala hili, na tutaanza kwa kumshtaki Muliro,” alisema Heche ambaye pia alieleza kushangazwa na uwepo Kamanda Muliro ofisini kwa sasa.
Heche pia alionyesha kukerwa na hatua ya Polisi kumkamata wakati akienda kusikiliza kesi ya mwenyekiti wake, akisema hata Nelson Mandela hajawahi kufanyiwa hivyo.
“Haijawahi kutokea, hata kina Mandela (Nelson – Rais wa zamani wa Afrika Kusini) hakufanyiwa hivi, unamzuiaje makamu mwenyekiti wa chama?
“Natoa wito kwa wanachama wa Chadema, kesi ijayo tutakwenda zaidi na kutakuwa na watu wengi zaidi, hatutafanya fujo, tutakuwa watulivu kabisa,” alisema.

Polisi yamuachia Hilda
Baada ya kutafutwa huku makada wa Chadema wakipaza sauti kupitia mitandao ya kijamii, hatimaye Jeshi la Polisi limemuachia Mjumbe wa Baraza Kuu kupitia Baraza la Wanawake Chadema (BAWACHA) Hilda Newton ambaye alikuwa anashikiliwa tangu juzi.
Awali, ilielezwa kuwa Hilda alikamatwa na Polisi maeneo ya Mahakama ya Kisutu jijini Dar es Salaam na kuhifadhiwa katika Kituo Kikuu cha Polisi Central.
Hata hivyo, uongozi wa Chadema umetangaza kuwa Hilda ameachiwa kwa dhamana jana usiku.