Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Chadema, Msajili wa vyama vya siasa ngoma nzito

Muktasari:

  • Kikao hicho kimefanyika leo Jumanne Machi 18, 2025 katika ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, Posta jijini Dar es Salaam baada ya ofisi kupelekea wito Chadema wa mazungumzo baina yao kuhusu no reform no election (hakuna mabadiliko hakuna uchaguzi) katika muktadha wa Sheria ya Vyama vya Siasa.

Dar es Salaam. Ngoma nzito kati ya Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema). Ndivyo unavyoweza kueleza baada ya mazungumzo baina ya pande mbili yaliyochukua takribani saa nne kuhusu kaulimbiu ya chama hicho.

Kikao hicho kimefanyika leo Jumanne Machi 18, 2025 katika ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, Posta jijini Dar es Salaam baada ya ofisi hiyo kupelekea wito kwa Chadema kuhusu kaulimbiu ya no reforms no election (hakuna mabadiliko hakuna uchaguzi), katika muktadha wa sheria ya vyama vya siasa.

Kwenye kikao hicho kilichoanza saa nne asubuhi na kuhitimishwa saa nane mchana, taarifa zinaeleza jopo la maofisa wa Ofisi ya Msajili lilikuwa na watu saba, wakiongozwa na Jaji Francis Mutungi na wasaidizi wake akiwemo, Sisty Nyahoza.

Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi (kushoto) akisalimiana na Katibu wa Mkuu wa Chadema, John Mnyika alipofika ofisini kwake leo Machi 18, 2025 jijini Dar es Salaam.

Ujumbe wa Chadema ulioshiriki majadiliano hayo uliongozwa na Katibu Mkuu wa chama hicho, John Mnyika na kuwa shirikisha Mwanasheria Mkuu wa chama hicho, Dk Rugemeleza Nshala, manaibu makatibu wakuu Tanzania Bara na Zanzibar, Aman Golugwa na Ally Ibrahim Juma na Mkurugenzi wa Mawasiliano na Uenezi, Brenda Rupia.

Mwanzoni wa Desemba 2024, Kamati Kuu ya Chadema chini ya aliyekuwa mwenyekiti wa chama hicho, Freemna Mbowe ilipitisha kaulimbiu hiyo kuwa ndio msimamo wa chama hicho kuelekea Uchaguzi Mkuu 2025, kabla ya msimamo huo kuthibitishwa na mkutano mkuu wa chama hicho Januari 21, 2025.

Msimamo huo uliibua hisia za watu mbalimbali na kwa nyakati tofauti,  viongozi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) waliuzungumzia kwenye majukwaa ya kisiasa, wakisema mabadiliko ya uchaguzi yameshafika kupitia 4R (Ustahimilivu, mageuzi, kujenga upya na maridhiano).

Lakini pia, Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria, Eliakim Maswi aliwahi kujibu hilo, akisema kama kuna nia njema ya mabadiliko, ofisi za wizara hiyo ziko wazi kwa yeyote kwenda kujadiliana.

Hata hivyo, Maswi alisisitiza kuwa Chadema pekee haiwezi kuzuia uchaguzi kwa kuwa mchakato huo unawahusisha wananchi na chama zaidi ya kimoja.

Chadema kwa upande wake wanasema pasipo mabadiliko hayo hawatasusia uchaguzi huo wa Oktoba 2025, bali watauzuia kufanyika.

Msimamo wa Maswi ulisisitizwa na Makamu Mwenyekiti wa CCM-Bara, Stephen Wasira kwamba “hakuna mtu anayeweza kuzuia uchaguzi kufanyika.”

Wasira alisema hakuna taasisi yoyote ya kiserikali wala chama cha siasa chenye uwezo wa kuahirisha uchaguzi mkuu labda itokee vita, ambavyo Tanzania hakuna.

“Sis ni wadau wa uchaguzi, kazi yetu ni kuitumia dola kuleta mabadiliko ya watu…kwa hiyo hatuwezi kuambiwa hakuna uchaguzi. Wao kama wanataka kuingia kwenye uchaguzi bahati mbaya sisi tunawakaribisha maana uwezo wa kuwashinda tunao wanasingizia CCM wanaiba, tunaiba nini?

"Tumefanya uchaguzi wa serikali za mitaa kuna mitaa hawakupata hata mtu mmoja wa kusiamamisha, sasa mtu ambaye hana mtu wa kusimamisha kwenye mtaa na kijiji atakushinda kwa namna gani, ni muujiza au ni kitu gani,” alihoji Wasira.


Chadema na Msajili

Wakati fukuzo za kaulimbiu hiyo likiendelea, ndipo msajili akawaita Chadema ili waijadili kwa muktadha wa sheria ya vyama vya siasa.

Akizungumza na wanahabari baada ya kutoka katika kikao hicho, Mnyika amesema wameulizwa wanamaanisha nini wanaposema ‘no reform no election’ na kuwa wao wamefafanua ajenda hiyos.

“Tumeieleza Ofisi ya Msajili kuhusu msimamo huu, baada ya kilichotokea katika uchaguzi wa serikali za mitaa, vijiji na vitongoji wa mwaka 2024 na historia ya chaguzi kuanzia mwaka 2019 na uchaguzi mkuu wa mwaka 2020,” amesema Mnyika.

Mnyika amesema wameieleza ofisi ya msajili kwa kina, namna ambavyo mifumo ya uchaguzi haipo huru, tangu kuasisiwa kwa mfumo wa vyama vingi.

Pia, amesema wamezungumzia namna ambavyo mchakato wa Katiba Mpya chini ya Tume ya Jaji mstaafu, Joseph Warioba uliyokwama ambao ulipendekeza kufanyika kwa mabadiliko ya kikatiba, kisheria na kuwezesha Taifa kuwa na chaguzi huru na haki.

“Tumeeleza michakato yote ya kutafuta mabadiliko kabla ya kuelekea uchaguzi, kupitia mazungumzo kati ya Chadema, CCM na Serikali ilivyokwenda.

“Tumewaambia katika mazingira haya yote yaliyojitokeza kwa nini ni lazima kabla ya uchaguzi wa mwaka 2025, kufanyika kwa mabadiliko ya kisheria, kikatiba, kikanuni na kitaasisi ili kuwezesha uchaguzi huru na haki,” amesema Mnyika.

Hata hivyo, jitahada za kumtafuta Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Mutungi ziligonga mwamba, baada ya waandishi kushindwa kuingia ofisini kwake.

Sambamba na hilo, Mwananchi lilimtafuta kwa simu Jaji Mutungi, bila mafanikio, awali ikipokewa na msaidizi wake, aliyedai bosi wake yupo katika kikao, atafutwe baadaye.

Hata hivyo, alipotafutwa baadaye simu yake haikupokewa.


Kikao kingine kufanyika tena

Kwa mujibu wa Mnyika, bado kuna mambo mengine zaidi yanahitaji kuzungumzwa baina ya Chadema na Ofisi ya Msajili ili kupata ufahamu na uelekeo.

Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi (kushoto) akiwa kwenye kikao na baadhi ya viongozi wa Chadema waliofika ofisini kwake leo Machi 18, 2025 jijini Dar es Salaam.

Amesema wameelezwa kuwa wataitwa tena siku nyingine kwa ajili ya mwendelezo wa mazungumzo hayo.

“Wakati tukisubiri kukutana nao tena, Chadema inaendelea na ratiba zake kama kawaida, tutaendelea na jitihada na majukumu yote tunayoyatekeleza kuhakikisha ‘no reform no election’ inatekelezeka,” amesema.

“Hivi karibuni tutawatangazia ziara ya kuanza kwa mikutano ya hadhara katika maeneo mbalimbali ya nchi, ili kuzungumza na Watanzania kuhusu no reform no election na mustakabali wa nchi,” amesema Mnyika.


Alichokisema mchambuzi

Wakati Chadema ikijiandaa kwa hilo, Mchambuzi wa siasa na jamii, Ramadhan Manyeko amesema kwa wakati huu, Chadema haiwezi kufanikiwa na ajenda hiyo, kwa sababu ni ajenda yao binafsi, si ya vyama vyote vya siasa.

“Ili uungwe mkono lazima ushirikishe wadau, sasa Chadema wapo kama wao na huu ni mfumo wa vyama vingi. Mwaka 2015 Chadema walifanya vizuri na kupata viti vingi bungeni kupitia Ukawa (Umoja wa Katiba ya Wananchi),

“Ajenda hii ina nguvu, kama ingekuwa inaungwa mkono na wadau wote wa uchaguzi na kama unavyojua kidole kimoja hakivunji chawa,” amesema Manyeko.

Kuhusu kuitwa kwa Ofisi ya Msajili, Manyeko amesema: “Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, ni mlezi wa vyama vya siasa, lazima amsikilize mwanaye ana hoja gani, kisha kutoa msimamo kama baba.”