CCM yawatahadharisha wagombea na rushwa

Katibu wa Itikadi na Ueenezi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Mbeya, Chrisopher Uhagile akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani).
Muktasari:
- Uchaguzi huo unafanyika ili kuziba nafasi iliyoachwa wazi na Dk Stephen Mwakajumilo aliyeteuliwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Nanyumbu mkoani Mtwara.
Mbeya. Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Mbeya kimetangaza Desemba 4 kuwa siku ya uchaguzi wa nafasi ya Mwenyekiti wa Mkoa huku kikiwatahadharisha wagombea walioteuliwa kujiepusha na rushwa.
Chama hicho pia kimeviomba vyombo vya dola ikiwamo Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kufuatilia wagombea wote ili atakayebainika kufanya vitendo vyovyote vya rushwa achukuliwe hatua.
Uchaguzi huo unafanyika ili kuziba nafasi iliyoachwa wazi na Dk Stephen Mwakajumilo aliyeteuliwa kuwa mkuu wa Wilaya ya Nanyumbu mkoani Mtwara.
Novemba 29, Halmashauri Kuu ya CCM Taifa ilitangaza majina matatu ya wagombea wa nafasi ya Mwenyekiti wa chama hicho Mkoa wa Mbeya miongoni mwa wagombea 48 waliokuwa wameomba kuwania nafasi hiyo.
Waliopita kuwania nafasi hiyo ni Patrick Mwalunenge, Felix Liyaniva na Fatuma Kasenga ambao wanatarajia kuchuana kuwania nafasi hiyo.
Akizungumza na wanahabari jana Alhamisi, Novemba 30,2023 Katibu wa Itikadi na Uenezi wa chama hicho mkoani Mbeya, Chrisopher Uhagile amesema wagombea wanapaswa kufuata utaratibu vinginevyo chama hakitasita kuchukua hatua.
“Uchaguzi utakuwa Desemba 4 mwaka huu, tunawapongeza waliopita ila tunawataka wafuate utaratibu kwa kuwa watajinadi siku hiyo ukumbini kwa wajumbe.
“Niziombe mamlaka ikiwamo Takukuru kuwa makini kufuatilia zaidi hatua kwa hatua wagombea hawa ili kama kutakuwapo viashiria vya rushwa wachukuliwe hatua, tunataka kumpata kiongozi aliye bora,” amesema Uhagile.
Nao baadhi ya waliopitishwa kuwania nafasi hiyo, wameshukuru kamati wakiahidi kukitumikia vyema chama hicho na Taifa.
“Niishukuru Halamshauri kuu chini ya Rais Samia kuweza kunipitisha kuwania nafasi hii, sijawahi kuwa kiongozi wa siasa kwa nafasi yoyote lakini kupitia kazi ninayoifanya kwa jamii inatosha kutimiza malengo,” amesema.
Naye Liyavina amesema, “Naipongeza na kuishukuru Halmashauri Kuu ya chama changu kurejesha majina yangu, ninao uwezo, nia na uzoefu kwenye kukitumikia chama kuanzia ngazi ya wilaya hadi mkoa nikiwa mhasibu, lakini nimekuwa Mkuu wa Wilaya za Rorya na Temeke,” amesema.