48 warejesha fomu CCM Mbeya, watatu wakwama

Katibu wa Itikadi ya Uenezi CCM Mkoa wa Mbeya, Christopher Uhagile akionyesha fomu za majina ya wagombea nafasi ya Uenyekiti wa chama ngazi ya Mkoa leo, Alhamisi Novemba 16, 2023 mara baada ya kufunga zoezi hilo. Picha na Hawa Mathias
Muktasari:
- Makada 51 wachukua fomu kugombea nafasi ya Mwenyekiti CCM Mkoa wa Mbeya, ambapo kati ya hao, wanaume ni 43 huku kukiwa na wanawake wanane. Hata hivyo, waliorejesha fomu hizo ni wanachama 48 kati ya hao wanaume 41 wanawake saba.
Mbeya. Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Mbeya kimesema jumla ya makada wake 51 walichukua fomu za kuwania nafasi ya mwenyekiti wa chama hicho mkoa huo, ambapo 48 wamerejesha fomu hizo kwa hatua zinazofuata huku watatu wakikwama kurejesha.
Nafasi hiyo iliyoachwa wazi baada ya aliyekuwa akiishikilia, Stephen Mwakajumilo kuteuliwa na Rais Samia Suluhu Hassan kuwa Mkuu wa Wilaya ya Nanyumbu, Mkoa wa Mtwara.
Katibu Itikadi na Uenezi mkoa huo, Christopher Uhagile amewaambia waandishi wa habari leo Alhamisi Novemba 16, 2023 kuwa kati ya makada waliochukua fomu 51 watatu ndio hawajaresha wakiwepo wanaume wawili mwanamke mmoja.
“Tunashukuru mwitikio umekuwa mkubwa, kwa sasa baada ya kupata idadi ya wagombea, kesho tunaanza vikao vya kupendekeza majina ambapo Jumapili Novemba 19 mwaka huu tuwaita kwa ajili ya kukagua taarifa zao na kuzithibisha,” amesema.
Uhagile amesema tayari wametoa mwongozo kwa wagombea wote waliorejesha fomu kutojihusisha kupiga kampeni kwa wajumbe kabla majina hayapitishwa kuanzia ngazi ya kata, wilaya na mkoa kwani kuna utaratibu wa ufuatiliaji.
Ameongeza kuwa: “Mgombea atakaye bainika kukiuka utaratibu atawajibishwa na kufutiwa ushiriki katika kuwania nafasi hiyo ngazi ya mkoa,” amesema.
Akizungumza na Mwananchi Digital, mmoja wa wagombea hao waliorejesha fomu ambaye ni Mwanahabari Isack Kyando, amesema kwa sasa hawezi kueleza mipango yake kulingana na taratibu na maagizo yaliyotolewa CCM ngazi ya Mkoa.
“Tusubiri wakati ukifika nitaongea, kwa sasa tusubiri vikao vya ndani ya chama kupendekeza majina endapo Mwenyezi Mungu akijalia jina langu likarudi, basi utakuwa ni wakati sahihi wa kusema neno,” amesema Kyando.
Kaimu Katibu wa CCM Mkoa, Clemence Mponzi amesema mwamko wa makada wa chama kuwania nafasi hiyo ni mkubwa sana na kuonyesha ni jinsi gani chama kinavyozidi kukua na kuongeza idadi ya wanachama.