Prime
CCM, ACT na Chaumma wanavyogawana wabunge 19 wa Chadema

Muktasari:
- Baada ya Bunge kuvunjwa, wabunge 19 wa Chadema waliokuwa na mgogoro wa ndani, wamejiunga na vyama vingine. Tisa wamehamia CCM na kuchukua fomu za ubunge, wawili wamejiunga na ACT Wazalendo na Chaumma. Wanane bado hawajaweka wazi msimamo wao.
Dar es Salaam. Vyama vya CCM, ACT Wazalendo na Chaumma vimejikuta vikigawana waliokuwa wabunge 19 wa viti maalumu kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), wanaotafuta hatima yao kisiasa kwenye vyama hivyo.
Baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kuhitimisha shughuli za Bunge, Juni 27, 2025, wabunge hao, walioingia kwenye mgogoro na chama chao baada ya Uchaguzi Mkuu 2020, wameibukia kwenye vyama vingine vya siasa.
Wakati CCM kikiendelea na mchakato wa uchukuaji na urejeshaji fomu za kutia nia ya kugombea ubunge na udiwani, baadhi ya wabunge hao wameenda mbali zaidi kwa kwenda kuchukua fomu za kuomba ridhaa ya kuteuliwa kukiwakilisha chama hicho katika uchaguzi mkuu ujao.
Licha ya Baraza Kuu la Chadema kuwavua uanachama wabunge hao baada ya kukaidi wito wa kwenda kuhojiwa kuhusu tuhuma za kwenda kinyume na msimamo wa chama hicho, wabunge hao walipinga hatua hiyo na kukimbilia mahakamani.
Kati ya wabunge hao 19, 11 kati yao wametangaza kujiunga na vyama vingine vya CCM, Chaumma na ACT Wazalendo. Wabunge wengine wanane bado hawajaeleza hatima yao kisiasa. Hata hivyo, bado wana muda wa kufanya hivyo.
CCM ndiyo chama kilichovuna makada hao wengi zaidi, ambao wote wamejitoa kugombea ubunge wa majimbo na wengine viti maalumu. Hadi leo, tisa wamekwenda CCM na kuchukua fomu za kutia nia ya kugombea ubunge.
Vyama vingine vya ACT Wazalendo na Chaumma vimepata mbunge mmoja kila kimoja, huku vikitarajia kuvuna wengine.
Wengine ambao mpaka sasa hawajatangaza uelekeo wao kisiasa ni pamoja na Halima Mdee, Grace Tendega, Jesca Kishoa, Tunza Malapo, Kunti Majala, Conchesta Rwamlaza, Anatropia Theonest na Asia Mohammed.
Waliotimkia CCM
Wabunge waliohamia CCM na kuchukua fomu za kuomba kuteuliwa ni Felista Njau anaomba ridhaa ya kuteuliwa kuwania ubunge katika Jimbo la Moshi Vijijini mkoani Kilimanjaro. Amechukua fomu Juni 29, 2025, katika ofisi za CCM Wilaya ya Moshi Vijijini. Jimbo hilo kwa sasa linaongozwa na Profesa Patrick Ndakidemi.
Kwingineko, mkoani Shinyanga, aliyekuwa mbunge wa viti maalum kupitia Chadema, Salome Makamba, amejitokeza katika ofisi za CCM mkoani humo kuchukua fomu ya kuomba ridhaa ya kugombea tena nafasi hiyo kupitia Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT).
Kwa upande wake, Esther Matiko ametangaza kujiunga na CCM na kuchukua fomu ya kugombea ubunge katika Jimbo la Tarime Mjini. Matiko alikuwa mbunge wa jimbo hilo kupitia Chadema kuanzia mwaka 2015–2020.
Huko mkoani Mara, Esther Bulaya amechukua fomu kuomba ridhaa ya kuteuliwa kugombea ubunge Bunda Mjini kupitia CCM. Bulaya aliwahi kuwa mbunge wa jimbo hilo baada ya kumshinda Stephen Wasira katika Uchaguzi Mkuu 2015.
Sophia Mwakagenda naye hakubaki nyuma. Baada ya kutimkia CCM, ametangaza nia ya kugombea ubunge katika Jimbo la Rungwe ambapo, pamoja na makada wengine wa CCM, anatarajiwa kuchuana na aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo, Antony Mwantona.
Huko Manyara, Cecilia Paresso naye ametimkia CCM, akitia nia ya kuwania ubunge Jimbo la Karatu. Hadi sasa, wanaowania nafasi hiyo wamefika wanane, akiwemo mbunge anayemaliza muda wake, Daniel Awack, Pantaleo Paresso, Patrice Mattay, Shedrack Qamna na Damian Sanka.
Katika orodha hiyo pia yumo Nusrat Hanje ambaye amekwenda kutia nia ya kugombea ubunge katika Jimbo la Ikungi Mashariki kupitia CCM.
Stella Simoni Fiyao naye amechukua fomu ya kuomba ridhaa ya kuchaguliwa kugombea ubunge Jimbo la Ileje kupitia CCM. Fiyao anatarajiwa kushindana na mbunge wa sasa Godfrey Kasekenya ambaye ni Naibu Waziri wa Ujenzi. Wengine ni Elius Ndabila, Joel Kaminyoge na Edison Ngabo, ambao wote walitia nia jimboni humo mwaka 2020.
Mwingine ni aliyekuwa Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Tabora kupitia Chadema, Hawa Mwaifunga, leo amefika katika ofisi za CCM Wilaya ya Tabora Mjini kuchukua fomu ya kuomba ridhaa kwa chama hicho ateuliwe kugombea nafasi ya ubunge Jimbo la Tabora Mjini.
Waliokwenda upinzani
Mbali na wanasiasa hao waliotimkia CCM, wengine wawili wamekwenda vyama vya upinzani vya ACT Wazalendo na Chaumma, ambako nako inatarajiwa watachukua fomu za kugombea ubunge wakati mchakato huo ukiendelea.
Juni 28, 2025, Naghenjwa Kaboyoka alihamia ACT Wazalendo baada ya kukabidhi kadi yake ya Chadema na kukabidhiwa kadi mpya ya chama hicho. Itakumbukwa kuwa Kaboyoka alikuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) kwa miaka 10.
Wakati huohuo, Agnesta Kaiza amejiunga na Chaumma akiwa ni kada pekee kutoka kundi la waliokuwa wabunge 19 wa Chadema, huku viongozi wakieleza kuwa milango iko wazi kwa wengine wanaotaka kujiunga na chama hicho.
Akizungumzia ujio wa wabunge hao, Katibu Mkuu wa Chaumma, Salum Mwalimu, amesema chama hicho hakibagui mtu, yeyote anayetaka kujiunga awasiliane na viongozi, kwani milango iko wazi.
“Sisi hatuangalii huyu ni nani au yule ni nani, kila mtu anakaribishwa kujiunga na chama chetu na akitaka anaweza kugombea, hatuna ubaguzi. Hatuwezi kusema kuna watu wanakuja, yeyote anakaribishwa,” amesema Mwalimu.
Chaumma yapuliza kipyenga
Wakati huohuo, Chaumma kimepuliza kipyenga kwa wananchi wote wenye nia ya kugombea nafasi ya ubunge na udiwani kupitia chama hicho kuchukua fomu kuanzia kesho, Julai Mosi, 2025, huku kikieleza kuwa nafasi ya urais imewekwa kiporo.
Pamoja na kutangaza fursa hiyo, Chaumma kimeweka masharti kwa kila anayetaka kugombea ubunge au udiwani viti maalumu. Sharti aanze kuonyesha nia ya kugombea kata au jimbo kwa nafasi tarajiwa upande wa Tanzania Bara na Zanzibar.
Chama hicho kinaungana na CCM na ACT Wazalendo ambao tayari wametangaza ratiba ya uchukuaji na urejeshaji fomu za ubunge, udiwani na uwakilishi ili kutoa fursa kwa wanachama wao kuomba uongozi.
Utaratibu huo wa Chaumma kuelekea uchaguzi mkuu wa Oktoba 2025 umetangazwa leo, Juni 30, 2025, jijini Dar es Salaam na Katibu Mkuu wa chama hicho, Salum Mwalimu.
“Tunawaomba wanachama wetu na wale ambao si wanachama wenye dhamira ya kugombea ubunge na udiwani kupitia Chaumma, ni wakati sahihi kujiandaa kuchukua fomu na kuzijaza kwa utaratibu na kuzirejesha kwa utaratibu ambao chama kimeweka.
Nimekuwa nikipokea simu nyingi na viongozi wenzangu nao walikuwa wakipokea simu lini tutafungua milango. Ni dhahiri Chaumma imeonekana ndiyo kimbilio kwa sasa, sauti mbadala wa makundi yote kwenye jamii,” amesema Mwalimu.
Amesema fomu za kugombea nafasi ya uwakilishi, nafasi ya ubunge Tanzania Bara na Zanzibar zitatolewa kupitia ofisi za chama hicho kote nchini.
Amesema fomu ya ubunge itatolewa kwa Sh50,000 na udiwani kwa Sh10,000. Wale wanaohitaji viti maalum vya ubunge na udiwani, sharti ni lazima wachukue fomu mbili-- ya kugombea kata au jimbo pamoja na fomu ya viti maalumu.