Zege halilali...wengine wajitosa ubunge CCM, yumo Mama Salma Kikwete

Muktasari:
- Mchakato huo unatarajiwa kukamilika Julai 2, 2025 ambapo tayari wabunge wanaotetea majimbo yao, wabunge wa zamani, watoto wa vigogo na wafanyabiashara, wamejitokeza kuchukua fomu.
Dar/Mikoani. Ikiwa ni siku ya tatu tangu kuanza kwa mchakato wa uchukuaji na urejeshaji wa fomu za kuwania ubunge ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), makada wa chama hicho wameendelea kujitokeza kutia nia katika majimbo mbalimbali nchini.
Mchakato huo unatarajiwa kukamilika Julai 2, 2025 ambapo tayari wabunge wanaotetea majimbo yao, wabunge wa zamani, watoto wa vigogo na wafanyabiashara, wamejitokeza kuchukua fomu.
Leo Juni 30, 2025, wanachama wa CCM wameendelea kuchukua fomu huku wanasiasa wengine waliokuwa upinzani, nao wameibukia kwenye chama hicho kama wanachama wapya huku nao wakitia nia za kugombea ubunge.

Mwenyekiti wa Chama cha Maofisa Rasilimali Watu na Utawala nchini ambaye pia alikuwa Diwani wa Kata ya Sandali Wilaya ya Temeke jijini Dar es Salaam, Christopher Kabalika (kulia) leo Juni 30, 2025 amechukua fomu ya kuomba ridhaa kwa Chama cha Mapinduzi CCM, kugombea nafasi ya Ubunge Jimbo la Temeke. Kabalika amekabidhiwa fomu hiyo na Katibu wa Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi UVCCM, Wilaya ya Temeke, Sayi Samba
Baada ya kukamilika kwa mchakato huo wa awali, wajumbe watapiga kura kuchagua mgombea atakayekiwakilisha chama hicho na baadaye, majina yatawasilishwa mbele ya Kamati Kuu ya CCM kujadiliwa.
Mama Salma atia nia
Aliyekuwa mbunge wa Jimbo la Mchinga, Salma Kikwete ambaye ni mke wa Rais wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete, amechukua fomu ya kuwania tena ubunge wa Jimbo la Mchinga lililopo Manispaa ya Lindi.

Mama Salma amekabidhiwa fomu hiyo leo Jumatatu Juni 30, 2025 na Katibu wa CCM Wilaya ya Lindi, Mohamed Lawa, katika ofisi za makao makuu ya chama hicho zilizopo manispaa ya Lindi mkoani Lindi.
Mwingine aliyechukua fomu ni aliyekuwa mbunge wa Tanga Mjini, Ummy Mwalimu. Ummy amechukua fomu ya kutetea nafasi hiyo kwenye uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 2025, leo Jumatatu Juni 30, 2025 akikabidhiwa na Katibu wa CCM Wilaya ya Tanga, Jamal Abbas.
Aliyekuwa mbunge wa Jimbo la Kwela na Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi na Utawala Bora, Deus Sangu amechukua fomu ya kuomba ridhaa kuwawakilisha wananchi katika jimbo la Kwela.
Wabunge wa Chadema wamo
Waliokuwa wabunge wa Chadema wameendelea kujitosa kwenye ubunge kupitia CCM ambapo katika siku ya tatu leo, wengine wamejitosa kwa kuchukua fomu kuomba ridhaa ya chama hicho kugombea ubunge.
Aliyekuwa mbunge wa viti maalumu Chadema (aliyefukuzwa uanachama na chama hicho), Esther Bulaya amechukua fomu kuomba ridhaa ya kukiwakilisha chama hicho katika uchaguzi wa ubunge katika Jimbo la Bunda Mjini alilowahi kulitumikia kama mbunge wake kati ya 2015 - 2020.

Hii ni mara ya tatu Bulaya kugombea ubunge wa jimbo hilo ambapo kwa mara ya kwanza aligombea mwaka 2010 kupitia Chadema, baada ya kushindwa kwenye kura za maoni ndani ya CCM, alihamia Chadema ambapo alimshinda aliyekuwa mpinzani wake, mwanasiasa mkongwe, Stepehn Wasira.
Katika uchaguzi wa mwaka 2020, aligombea tena lakini alishindwa mbele ya mgombea wa CCM, Robert Maboto, hata hivyo alirejea bungeni kama mbunge wa viti maalumu kupitia nafasi 19 za Chadema.
Kwa upande wake, Cecilia Paresso, mmoja wa waliokuwa wabunge 19 wa Chadema, amechukua fomu ya kugombea ubunge katika Jimbo la Karatu kwa tiketi ya CCM. Paresso amekabidhiwa fomu na Katibu wa CCM Wilaya ya Karatu, Hanafi Msabaha.
Hadi sasa, waliojitokeza kuwania nafasi hiyo wanazidi kuongezeka akiwemo mbunge anayemaliza muda wake, Daniel Awack, Pantaleo Paresso, Patrice Mattay, Shedrack Qamna na Damian Sanka.

Stella Fiyao, naye amechukua fomu kuomba ridhaa ya kuchaguliwa kugombea ubunge Jimbo la Ileje kupitia CCM. Fiyao anatarajiwa kushindana na mbunge wa sasa ambaye ni Naibu Waziri wa Ujenzi, Godfrey Kasekenya, Elius Ndabila, Joel Kaminyoge na Edison Ngabo ambao wote walitia nia jimboni humo mwaka 2020.
Aliyekuwa mbunge wa viti maalumu Mkoa wa Tabora kupitia Chadema, Hawa Mwaifunga, leo amefika katika ofisi za CCM Wilaya ya Tabora Mjini kuchukua fomu ya kuomba ridhaa kwa chama hicho ili ateuliwe kugombea nafasi ya ubunge Jimbo la Tabora Mjini.
Wengine waliotia nia
Mbunge wa Simanjiro mkoani Manyara, anayemaliza muda wake, Christopher Ole Sendeka ni mmoja wa makada wa CCM waliochukua fomu. Leo amekabidhiwa fomu ya kuomba ridhaa ya kugombea tena ubunge wa Simanjiro na Katibu wa CCM Wilaya ya Simanjiro, Amos Shimba katika mji mdogo wa Orkesumet.

Vilevile, mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki (Eala), James Ole Millya amechukua fomu akitangaza nia ya kugombea katika Jimbo la Simanjiro. Ole Millya amekabidhiwa fomu yake na Katibu wa CCM Wilaya ya Simanjiro Amos Shimba.
Mbali na vigogo hao, Abubakari Alawi naye amechukua fomu akiwania ubunge katika Jimbo la Kibaha Mjini. Hii itakuwa ni mara yake ya pili kutia nia kwenye nafasi ya ubunge katika jimbo hilo ambapo mara ya kwanza ilikuwa mwaka 2020.

Kwingineko mkoani Kilimanjaro, mjumbe wa mkutano mkuu wa CCM kutoka Kilimanjaro, Samweli Tesha amechukua fomu ya kuomba ridhaa ya kugombea ubunge katika Jimbo la Moshi Vijijini. Amepokea fomu hiyo leo kutoka kwa Katibu wa Jumuiya ya wazazi, Hendry Mwandu.
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kigoma, Jamal Tamimu naye amechukua fomu ya kuomba ridhaa ya chama hicho kugombea ubunge katika Jimbo la Muhambwe ikiwa ni mara yake ya nne kutia nia katika jimbo hilo bila mafanikio.
Mbunge wa Missenyi aliyemaliza muda wake, Frolent Kyombo amechukua fomu ya kugombea ubunge wa jimbo hilo.
Kadhalika, mwanachama wa CCM, Zuhura Mkumba amejitosa kuwania ubunge katika Jimbo la Newala Mjini mkoani Mtwara. Mkumba amekabidhiwa fomu hiyo leo na Katibu wa CCM Wilaya, Robert Mwega.
Jimbo hilo lilikuwa likiongozwa na mwanasiasa mkongwe, Kapteni George Mkuchika kwa miaka 20, hata hivyo sasa ametangaza kutogombea tena katika nafasi hiyo kwa kile alichoeleza mwenyewe kuwa ni uzee na anataka kupisha damu changa.
Kada wa CCM, Omary Mgumba, aliyewahi kuwa mbunge katika Jimbo la Morogoro Kusini Mashariki kati ya mwaka 2015 – 2020, amechukua tena fomu akiomba kukiwakilisha chama hicho katika uchaguzi ujao. Katika uchaguzi uliopita, Mgumba alipoteza kwa Hamis Taletale ambaye naye amechua fomu kutetea nafasi yake.
Aliyekuwa mbunge wa viti maalumu Mkoa wa Tanga, Mhandisi Mwanaisha Ulenge amechukua fomu kutetea nafasi hiyo kwa mara nyingine.
Mhandisi Ulenge amekabidhiwa fomu na Katibu wa Umoja wa Wanawake (UWT) Mkoa wa Tanga, Anastazia Amani.