Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

ACT- Wazalendo wakutana kutathmini hali ya kisiasa, SUK

Muktasari:

  • Mwenyekiti wa ACT-Wazalendo Taifa, Othman Masoud Othman amesema Watanzania kwa muda mrefu wamepoteza matumaini kutokana na uongozi kushindwa kusimamia misingi ya haki, uadilifu na ustaarabu

Dar es Salaam. Mwenyekiti wa ACT-Wazalendo, Othman Masoud Othman, ameongoza kikao cha dharura cha Kamati Kuu Maalumu ya chama hicho kilicholenga kujadili na kutathmini hali ya kisiasa nchini.

Akizungumza leo Jumapili, Machi 3, 2026, wakati akitoa salamu zake katika kikao kilichofanyika makao makuu ya chama hicho Magomeni jijini Dar es Salaam, Othman amewataka viongozi wa chama hicho kutumia hekima na weledi katika kujadili masuala ya Taifa ili kusaidia kuifikisha Tanzania kwenye mafanikio.

Othman ambaye amewahi kuwa Makamu wa Kwnaza wa Rais Zanzibar amedai Watanzania kwa muda mrefu wamepoteza matumaini kutokana na uongozi kushindwa kusimamia misingi ya haki, uadilifu na ustaarabu.

Mwenyekiti wa ACT Wazalendo Taifa, Othman Masoud Othman, wakati akiongoza kikao cha Kamati Kuu kilichofanyika Mei 3, 2026 kwenye ukumbi wa Hakainde Hichilema, Makao Makuu ya ACT Magomeni Jijini Dar es Salaam.

“Hii ni kutokana na ukweli wa dhati kwamba wale waliojipa mamlaka ya kuongoza Taifa hili wanatukosea kwa kushindwa kusimamia misingi ya haki, uadilifu na ustaarabu,” amesema.

Othman amesema chama hicho kinatakiwa kuweka mwelekeo utakaowajengea Watanzania matumaini mapya na kuandaa barabara ya kuwafikisha kwenye maendeleo wanayoyatarajia.

Amesema viongozi wanapaswa kuzingatia masilahi ya Taifa kwanza, badala ya kuangalia masuala ya kisiasa au nani ametenda nini, ili kujenga mustakabali bora wa nchi.

Akisisitiza ujumbe wa uongozi, alinukuu maneno ya Kiingereza akisema: “Give your emotions, all the intellects you have…” akieleza viongozi wanapaswa kutumia busara, hekima na maarifa yao kulinda heshima na matarajio ya wananchi.

Amesema wananchi wengi wamekata tamaa kufuatia matukio ya kisiasa yaliyotokea baada ya uchaguzi mkuu uliopita, hivyo kuna haja ya kuwatengenezea njia mpya ya matumaini na maendeleo.

Baadhi ya wajumbe wa Chama cha ACT Wazalendo wakati wakiwa kwenye kikao cha Kamati Kuu kilichofanyika leo Mei 3, 2026 kwenye Ukumbi wa Hakainde Hichilema, Makao Makuu ya Chama hicho Magomeni Jijini Dar es salaam.

“Tuitazame nchi yetu na taasisi zake madhubuti, tuyazingatie hayo sambamba na kuheshimu matarajio ya umma uliokwisha katishwa tamaa,” amesema.

Awali, Katibu Mkuu wa ACT Wazalendo, Ado Shaib amesema kikao hicho ni cha dharura na kimehusisha pia wajumbe wa Baraza la Wawakilishi la Zanzibar pamoja na wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kama waalikwa.

Amesema kikao hicho kilitanguliwa na kikao cha Kamati ya Uongozi kilichofanyika Aprili 29, 2026 mjini Unguja, chini ya uongozi wa Kiongozi wa chama, Doroth Semu.

Amesema kikao hicho kinatarajiwa kutoa maazimio na msimamo wa chama kuhusu mwenendo wa hali ya kisiasa nchini.

Viongozi mbalimbali wa ACT- Wazalendo, wakiwamo Makamu Wenyeviti Is-haka Mchinjita na Ismail Jussa, pamoja na watendaji wakuu wa chama hicho, wamehudhuria kikao hicho kinachoendelea.

Taarifa ambazo Mwananchi inazo ni kwamba miongoni mwa maazimio ni chama hicho kukubali kuingia serikalini Zanzibar ili kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK).

Tayari imeshapita miezi mitano tangu Dk Hussein Ali Mwinyi, aapishwe kuwa Rais wa Zanzibar, hatua iliyopaswa kufuatwa na ACT- Wazalendo iliyopata zaidi ya asilimia 20 ya kura, kumpendekeza kada wake mmoja, atakayeteuliwa kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais.

Mwanachama wa ACT wazalendo, Luhaga Mpina akichangia mada kwenye kikao cha Kamati Kuu kilichofanyika leo Mei 3, 2026 kwenye Ukumbi wa Hakainde Hichilema, Makao Makuu ya Chama hicho Magomeni Jijini Dar es salaam.

Ukimya ukatawala kwa chama hicho kikuu cha upinzani visiwani humo, hakikupendekeza kada yeyote. Ndipo vikao vya majadiliano vilipoanza vikihusisha ujumbe wa CCM na ACT- Wazalendo kutafuta mwafaka.

Kutoka kwenye vikao vya kamati hizo maalumu, majadiliano hayo hatimaye yakafika hadi kwenye vikao rasmi vya vyama hivyo. Kwa maana Kamati Kuu kwa upande wa CCM na Kamati ya Uongozi kwa ACT Wazalendo.

Hata hivyo, bado haujapatikana mwafaka. Isipokuwa Mwananchi imetaarifiwa na vyanzo mbalimbali kutoka ACT- Wazalendo kuwa, kabla ya kumalizika kwa Mei mwaka huu, tayari chama hicho kitakuwa ndani ya SUK.

“Mambo yanakwenda vizuri, subirini mtaona tu mwezi wa tano tunakwenda kuapa niamini kwa hili. Jumapili (Mei 3) tutakuwa na kamati huenda tukajadili suala hili pia,” alieleza mmoja wa viongozi wa ACT Wazalendo, aliyeomba hifadhi ya jina lake.