Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mambo manne kuamua SUK Zanzibar

Wajumbe wa kamati ya uongozi ya Chama cha ACT Wazalendo, wakiwa katika kikao kilichofanyika Jumatano Aprili 29, 2026 katika ofisi ndogo za makao makuu ya chama hicho Vuga mjini Unguja.

Muktasari:

  • Mambo manne hayo ni masharti yaliyowekwa na ACT Wazalendo ili ikubali kuwa sehemu ya Serikali hiyo.

Dar es Salaam. Hatima ya kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) visiwani Zanzibar, itapatikana baada ya makubaliano kuhusu mambo manne kati ya upande wa Chama cha Mapinduzi (CCM) na ule wa Chama cha ACT Wazalendo.

Mambo manne hayo ni masharti yaliyowekwa na ACT Wazalendo ili ikubali kuwa sehemu ya Serikali hiyo. Mambo hayo ni mabadiliko ya Katiba ya Zanzibar, mifumo ya uchaguzi, majukumu ya Makamu wa Kwanza Rais na SUK ishuke ngazi za chini.

Tayari imeshapita miezi mitano tangu Dk Hussein Ali Mwinyi, aapishwe kuwa Rais wa Zanzibar, hatua iliyopaswa kufuatwa na ACT Wazalendo iliyopata zaidi ya asilimia 20 ya kura, kumpendekeza kada wake mmoja, atakayeteuliwa kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais.

Ukimya ukatawala kwa chama hicho kikuu cha upinzani visiwani humo, hakikupendekeza kada yeyote. Ndipo vikao vya majadiliano vilipoanza vikihusisha ujumbe wa CCM na ACT Wazalendo kutafuta mwafaka.

Kutoka kwenye vikao vya kamati hizo maalumu, majadiliano hayo hatimaye yakafika hadi kwenye vikao rasmi vya vyama hivyo. Kwa maana Kamati Kuu kwa upande wa CCM na Kamati ya Uongozi kwa ACT Wazalendo.

Hata hivyo, bado haujapatikana mwafaka. Isipokuwa Mwananchi imetaarifiwa na vyanzo mbalimbali kutoka ACT Wazalendo kuwa, kabla ya kumalizika kwa Mei mwaka huu, tayari chama hicho kitakuwa ndani ya SUK.

“Mambo yanakwenda vizuri, subirini mtaona tu mwezi wa tano tunakwenda kuapa niamini kwa hili. Jumapili (Mei 3) tutakuwa na kamati huenda tukajadili suala hili pia,” alieleza mmoja wa viongozi wa ACT Wazalendo, aliyeomba hifadhi ya jina lake.


Mambo manne

Leo, Mei 1, 2026 Mwananchi imezungumza na moja ya chanzo kilichomo kutoka ndani ya kamati za majadiliano kuhusu SUK na kimetaja mambo manne yaliyoorodheshwa na ACT Wazalendo kama masharti yake ili iingie serikalini, ikiwemo mabadiliko ya Katiba ya Zanzibar.

Masharti mengine kwa mujibu wa chanzo hicho, ni kupitiwa upya na kuboreshwa kwa mifumo ya uchaguzi, kuangaliwa upya kwa majukumu ya Makamu wa Kwanza wa Rais na SUK isiishie ngazi za juu iende hadi kwa wakuu wa wilaya.

Kuhusu mabadiliko ya Katiba ya Zanzibar, chanzo hicho kimesema ACT Wazalendo imetaka kupitiwa upya na kurekebishwa kwa vifungu vinavyoeleza madaraka ya Rais na mgawanyo wa madaraka.

Kwa upande wa maboresho ya mifumo ya uchaguzi, kimesema chama hicho kimetaka kubadilishwa kwa utaratibu wa watumishi wa umma kuwa wasimamizi wa uchaguzi na kuondolewa kwa utaratibu wa kura ya mapema.

Chanzo hicho, kimesema kwenye mamlaka ya Makamu wa Kwanza wa Rais, ACT Wazalendo kimetaka kiongozi huyo awe na nguvu ya kiutendaji, badala ya kubaki kuwa mshauri na mshiriki wa shughuli za kukata utepe wakati wa uzinduzi wa miradi.

“Ni kwamba hawakutaka ile nafasi ya Makamu wa Kwanza wa Rais iwe ‘ceremonial’ wametaka awe kiongozi mwenye nguvu ya kiutendaji na maamuzi, asibaki kuwa mshauri ambaye ushauri wake ni hiari kusikilizwa au kupuuzwa,” kimesema chanzo hicho.

Kuhusu kupitiwa upya kwa SUK yenyewe, chanzo hicho kimesema ACT Wazalendo imetaka umoja wa kitaifa usiishie kwenye nafasi za urais na mawaziri pekee, bali ushuke hadi ngazi za chini, ikiwemo wakuu wa mikoa na wilaya.


Ilichosema CCM

Alipotafutwa kuzungumzia hilo, Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Dk Mohammed Said Dimwa, amesema mambo hayo ni ajenda zilizoandaliwa kwa ajili ya kujadiliwa kuelekea SUK.

Kuandaliwa kwake, amesema kumetokana na timu ya marais wastaafu kuiomba kamati maalumu ya ACT Wazalendo, iandae ajenda ambazo inaziona zitafaa kwa makubaliano ya pamoja na hatimaye kuundwa kwa Serikali. Marais wastaafu waliopewa jukumu hilo ni Dk Ali Mohamed Shein na Amani Abeid Karume.

“Bado hatukujadiliana, isipokuwa marais wastaafu waliiomba kamati maalumu ya ACT Wazalendo itengeneze hizo ajenda baada ya hizo ndiyo tulipanga tuje na tamko la pamoja la kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa,” amesema.

Dk Dimwa amesema baada ya kuandaliwa kwa ajenda hizo, kukatokea kikwazo cha kuandaa tamko la pamoja, hali iliyosababisha timu za pande zote zirudi kujadiliana upya.

“Tulipokwama kuandaa tamko la pamoja, sasa tumeziachia timu ya marais wastaafu (CCM) na ile timu ya ACT Wazalendo chini ya mwenyekiti wao (Othman Masoud Othman), zikaangalie upya ajenda hizo na wakubaliane kisha watuletee,” amesema.

Alipoulizwa kuhusu nini hasa kilikwamisha kukamilika kwa tamko la pamoja, Dk Dimwa amesema ni mapema sana kulizungumzia hilo na kwamba bado hajapata ridhaa ya kuliweka hadharani.

“Ni mapema zaidi kulisemea hilo kwa sababu sijapata mamlaka ya kulizungumza kwa sasa. Nafikiri tuziache hizi timu za wastaafu zijadiliane na wenzetu kisha tutapata mwafaka,” amesema.

Amesisitiza ni matamanio ya CCM kuona maridhiano na SUK inaundwa ili kuleta utulivu visiwani humo na hatimaye kujenga mustakabali mzuri wa maendeleo ya uchumi.

Kwa upande wa Makamu Mwenyekiti wa ACT Wazalendo Bara, Issihaka Mchinjita Aprili 29, 2026 aliiambia Mwananchi kuwa kamati maalumu inayosimamia suala hilo ikiongozwa na Othman bado inaendelea na jukumu hilo kama ambavyo ilielekezwa na kamati kuu.

“Jumapili tutakuwa na kamati kuu nyingine ni maalumu kwa ajili ya masuala mengine, kama kamati ya SUK itakuwa na cha kueleza basi itatoa mrejesho. Kwa sasa, kamati ya SUK imefikia hatua ya makubaliano ya kutambua mambo gani ya msingi yanayopaswa kufanyiwa kazi,” ameeleza.

Amesema kila upande kwa sasa unapaswa kufanyia kazi makubaliano yaliyofikiwa na kwenda kwa umma kueleza yaliyokubaliwa katika mchakato huo.

“Nadhani hatua hiyo ikikamilika kamati zitatoka hadharani na hatua zitakazochukuliwa baada ya hapo. Ikiwa mapema itakuwa bora zaidi, kama kila upande utatekeleza kile tulichokubaliana,” amesema.

Kamati hizo maalumu kwa upande wa ACT Wazalendo inawakilishwa na Othman Masoud Othman na Juma Duni Haji, huku CCM ikiwakilishwa na marais wastaafu wa Zanzibar, Amani Abeid Karume na Dk Ali Mohamed Shein.

Machi 14, 2026 Othman ambaye ni mwenyekiti wa ACT Wazalendo aliwaondoa wasiwasi Wazanzibari, akiwataka kuwa watulivu kwa kuwa mazungumzo ya kuleta suluhu ya kisiasa Zanzibar yanaendelea vizuri.