Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

'Serikali haipangiwi tarehe, ipo imara muda wote na maeneo yote'

Waziri wa Mambo ya ndani, Patrobas Katambi akizungumza alipotembelea kwenye Banda la Jeshi la Polisi, kwenye viwanja vya Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa (Sabasaba) jijini Dar es Salaam. Picha na Said Powa

Dar/mikoani. Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Patrobas Katambi, amesema nchi itaendelea kuwa salama, akisisitiza Serikali haipangiwi tarehe, iko tayari na imara wakati wote na katika maeneo yote.

Pia, amesema Serikali itaendelea kuimarisha ulinzi katika maeneo yote, kuhakikisha kila anayestahili kwenda katika shughuli za kiuchumi anakwenda, anayepaswa kwenda shuleni anakwenda na shule zitafunguliwa.

Wakati Katambi akielezea hayo, Mwananchi imeshuhudia hali ya ulinzi ikiimarishwa katika maeneo mbalimbali ya Dar es Salaam na mikoa mingine.

Askari waliovalia sare, wenye mitutu ya bunduki, walionekana wakisimama na wengine wakizunguka kwa magari wakifanya doria.

Baadhi ya wananchi wameeleza kuwa wako katika hali ya wasiwasi na mashaka kwa kila sura ngeni wanayoiona, wakidhani ni askari kanzu.

Yote hayo yanakuja katikati ya vuguvugu la mipango ya maandamano linaloendelea katika mitandao ya kijamii, baadhi ya wanaharakati wakihamasisha wananchi waandamane kesho, Jumanne Julai 7, wakidai wanashinikiza upatikanaji wa haki ambapo, Serikali imeonya hatua hiyo.

Kutokana na hayo, Serikali ilishatangaza kusitishwa kwa baadhi ya matukio, ikiwemo mikutano ya hadhara ya vyama vya siasa, ikisema imebaini kuna viashiria vya uvunjifu wa amani.


Hali ilivyo mitaani

Katika Jiji la Mwanza, kumeshuhudiwa ulinzi ambao haujawahi kushuhudiwa hapo kabla.

 Askari wa Jeshi la Polisi waliokuwa na bunduki wameenea karibu kila eneo, hasa katika Stendi ya Mabasi ya Nyegezi.

Kila eneo walishuhudiwa askari zaidi ya watatu, wote wakiwa na silaha mikononi, baadhi wamevalia mavazi ya kuficha sura na wengine wakibeba vifaa vyenye vilipuzi.

Licha ya hali hiyo, katika masoko hakukuwa na msongamano wa wananchi wanaofanya manunuzi. Kama ilivyo siku zote, walikuwepo wananchi wanaonunua bidhaa mbalimbali kama kawaida.

Hii ni kutokana na kuwepo kwa taarifa zisizo rasmi kuwa kutakuwepo na maandamano siku ya Julai 7, 2026, hivyo Jeshi la Polisi limezidi kuimarisha ulinzi wake kuelekea kesho, Julai 7, 2026.


Watu hawaaminiani Dar es Salaam

Lakini mambo yalikuwa tofauti katika maeneo ya Mbezi Mwisho, Kimara na Ubungo, Dar es Salaam. Baadhi ya wananchi walidai kuwa wako katika hali ya wasiwasi, kwa kile walichosema kuwa kila sura ngeni waliyoiona waliihusisha na askari kanzu.

"Simwamini mtu. Leo tumeona sura nyingi mpya, wengine wanasema ni askari kanzu wamemwagwa mitaani. Yaani kila mtu anachunga maneno na matendo yake," amesema Sia Simwanza, anayeishi Kimara Suka, Dar es Salaam.

Maneno kama hayo yameelezwa pia na Said Said, dereva bodaboda wa Kimara Mwisho, aliyesema pamoja na wingi wa askari waliovalia sare na wenye mitutu mikononi, pia vijiweni kumekuwa na sura nyingi ngeni.

"Kila mtu anasema hao ni wazee wa kazi (askari), kwa hiyo tumekaa kwa kutulia, kwa sababu sisi hatuna nia ya kufanya vurugu."

Katika maeneo ya Ilala Boma, Mabibo, Buguruni na Magomeni ilikotembelea Mwananchi, hali ilikuwa shwari na wananchi walishuhudiwa wakiendelea na shughuli zao kama kawaida.

Polisi walishuhudiwa katika maeneo hayo, wengine wakiwa katika magari maalumu ya polisi na baadhi wakiwa wamesimama barabarani.

Pia, baadhi yao walionekana nje ya vituo vya mwendokasi katika eneo la Ilala Boma na Magomeni Mapipa.

Katika Viwanja vya Sabasaba, ndani na nje, ulinzi umeimarishwa ili kuhakikisha usalama wa wananchi wanaotembelea maonyesho hayo na waonyeshaji.

Ukaguzi unaofanywa nje ya uwanja huo umeongezeka zaidi. Sasa, badala ya kuchungulia ndani ya mkoba, ukaguzi unafanywa kwa kutoa kitu kimoja baada ya kingine, huku vile vinavyoonekana kuwa na mashaka askari polisi wakivihoji.

Kwa wale wanaokwenda na vyakula au vinywaji, hawaruhusiwi kuingia navyo. Badala yake huambiwa wale au wanywe, na wanaposhindwa huviacha getini.

Hilo limeenda sambamba na upimaji wa joto kwa kila anayeingia viwanjani hapo, ikiwa ni moja ya hatua za kudhibiti magonjwa ya Ebola.


Kauli ya Serikali

Akizungumza na waandishi wa habari katika maonyesho ya Sabasaba leo, Jumatatu Julai 6, 2026, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Patrobas Katambi amewahakikishia Watanzania kuwa tangu uhuru nchi imekuwa salama, sasa iko salama na itaendelea kuwa hivyo, akisisitiza Serikali haipangiwi tarehe kwani siku zote iko tayari.

"Serikali haipangiwi tarehe. Siku zote iko tayari. Tuko timamu katika kila eneo. Tumejipanga na tunaendelea kujipanga. Nchi yetu iko salama," amesema.

Amesema hadi sasa hakuna tishio lolote na halitakuwepo, na hata yanayosemwa na wananchi kuwa ni matishio, Serikali inaendelea kuchukua hatua.

"Tutakamata mhalifu na ndiyo tulisema kwamba sisi tutaendelea kuchukua hatua kwa mhalifu yeyote. Hakuna mtu mwenye kichwa kigumu mbele ya mkono wa sheria. Hakuna mtu yeyote akaona yeye ni Tanzania, hakuna aliyepo juu ya sheria," amesema.

Amesema Serikali itachukua hatua zote stahiki kwa yeyote atakayetishia au kutenda kitendo chochote cha uhalifu au kutishia amani.

Amesisitiza nchi iko salama na itaendelea kuwa hivyo, kama inavyoshuhudiwa watu wanaendelea na shughuli zao katika maonyesho ya Sabasaba bila matukio ya uhalifu na uvunjifu wa amani.

"Lakini, vilevile katika kila eneo tutaendelea kuimarisha ulinzi na usalama, kuhakikisha kila anayestahili kwenda katika shughuli za kiuchumi anaenda, anayepaswa kwenda shuleni anaenda, shule zitafunguliwa, na kwenye maeneo ya biashara shughuli zitaendelea kama kawaida. Kote tupo.

"Wahalifu si salama, si tu katika kipindi hiki, bali kipindi chochote. Tanzania si salama kwa wahalifu," amesisitiza.

Katambi amewataka wamiliki wa vyombo vya habari, waandishi wa habari na wengine wenye akaunti za mitandao ya kijamii kuepuka kurusha maudhui yanayotweza utu wa mtu, kuchochea uvunjifu wa amani na kuvuruga umoja.

"Hatua tutakazozichukua si tu kwa huyo aliyetengeneza maudhui yanayovunja amani, bali pia kwa mmiliki wa chombo cha habari ambacho habari yake inavunja sheria na kanuni," amesema.

Amesema kumekuwa na utaratibu wa watu kwenda katika vyombo vya habari kuzungumza mambo ambayo hayajachujwa, hawana mamlaka ya kuyazungumza, hawana uhakika nayo, yanapotosha na kuvunja umoja.

Ameeleza kuwa hali hiyo ikiruhusiwa, nchi itagawanyika vipandevipande, akisema kuna mifano mingi ya mataifa yaliyoharibika kwa kuruhusu haki isiyo na mipaka.

"Kwa heshima kabisa nawaomba Watanzania, wamiliki wa vyombo vya habari, wanasiasa, wanaharakati huru na wote, tunazungumzia amani ya Taifa letu. Bila amani, bila usalama wa Taifa, hakuna raia mmoja aliye salama.

"Vurugu yoyote haina mshindi, kwa sababu mwisho wa siku inaweza kumwathiri moja kwa moja au kwa njia isiyo ya moja kwa moja hata aliyeianzisha. Hakuna mshindi kwenye vurugu au vita," amesema.

Amesema Taifa linapozungumzia masuala ya amani lina ushahidi wa wakimbizi linaowalea, waliojikuta wakizikimbia nchi zao kwa sababu ya kile alichokiita chokochoko ndogo.

"Na sisi hatutakuwa na mzaha hata kidogo kwa mtu yeyote ambaye anavuruga amani ya Taifa letu," amesema.

Amesema hakuna Taifa ambalo likipoteza amani yake itarejea kwa urahisi na kwamba amani haina mbadala, akiwasihi wazazi na walezi kuwakanya watoto wao kwani jinai hailipi na haiozi.