ACT-Wazalendo kukomaa na kupanda nauli, marekebisho ya kanuni sheria ya kikokotoo

Waziri Mkuu wa baraza Kivuli la ACT- Wazalendo, Dorothy Semu akizungumza na wanahabari leo Januari 10, 2024 kuhusu mwelekeo wa baraza hilo kwa mwaka 2024. Picha na Michael Matemanga
Muktasari:
- Waziri Mkuu baraza Kivuli la ACT- Wazalendo, Dorothy Semu ametaja mambo matano yatakayosimamiwa na baraza hilo kwa mwaka 2024 ili kuyapatia ufumbuzi na kuleta unafuu kwa wananchi.
Dar es Salaam. Chama cha ACT- Wazalendo, kimeainisha mambo matano watakayoyapigania kwa mwaka 2024, kupitia baraza la kivuli la chama hicho, huku suala la kupanda kwa nauli za mabasi na daladala likiwa miongoni mwa mambo hayo.
Maeneo mengine ambayo baraza hilo litayasemea ni pamoja na kupigania unafuu wa gharama za maisha, upatikanaji umeme wa uhakika, haki na usalama wa ardhi kwa wananchi wa mijini na vijijini, migogoro ya ardhi na marekebisho ya kanuni ya kikotoo cha mafao.
Waziri Mkuu Kivuli wa chama hicho, Dorothy Semu ameeleza hayo leo Jumatano Januari 10, 2024 wakati akizungumza na wanahabari kuhusu utendaji kazi wa baraza hilo kwa mwaka 2023 na mwelekeo wao kwa 2024.
“Kwa miaka miwili tumeendelea kuwa sauti ya Watanzania katika masuala mbalimbali, lakini bado hali haijabadilika hivyo tutaongeza nguvu zaidi kwa robo ya kwanza ya mwaka huu kupigania changamoto hizi ili kuleta unafuu kwa Watanzania,” amesema Semu.
Katika mkutano huo, Semu amesema kwa nyakati tofauti chama hicho, kimekuwa kikipokea malalamiko kutoka kwa wananchi kuhusu kupanda kwa nauli za daladala na mabasi ya mikoani kulikosababisha gharama za maisha kuwa juu zaidi.
“Tutaishinikiza Serikali kuangalia upya bei za nauli za mabasi na daladala, kwa sababu malalamiko yamekuwa mengi kuhusu viwango hivi,” amesema.
Desemba 8, 2023 Mamlaka ya Usafiri wa Ardhini (Latra), ilitangaza nauli mpya kwa watumiaji wa usafiri wa daladala na mabasi ya mikoani, hatua iliyozua gumzo kwa baadhi ya wananchi walioshauri Serikali kuangalia upya viwango hivyo.
Kwa mujibu wa Latra, sababu za kupanda kwa nauli hizo ni gharama za uendeshaji ikiwemo kupaa kwa bei za petroli na dizeli.
Semu ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa ACT-Wazalendo (Bara), amesema mwaka 2023 ulikuwa mgumu kwa mwananchi wa kawaida kutokana na gharama za maisha kuwa juu, ikiwemo mfumuko wa bei za vyakula, licha ya hatua mbalimbali zilizochukuliwa na Serikali kukabiliana na changamoto hiyo.
“Tutajikita kutoa ushauri na mapendekezo zaidi yatakayowezesha kudhibiti kupanda kwa bidhaa ili Watanzania wamudu kuzinunua,” amesema Semu.
Juni mwaka 2023, Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba alitaja sababu mbalimbali zilizochochea mfumuko wa bei ikiwemo ya kupanda kwa gharama za bidhaa za ngano, mafuta ya kupikia, mbolea, petroli na dizeli zinazoagizwa nje ya nchi.
Semu amesema watatumia kila mbinu zikiwemo za kuandika barua, kufanya mikutano ya hadhara, wasemaji wa kisekta kufanya mikutano na wanahabari, kushiriki mijadala, kuonana na viongozi wa Serikali ana kwa ana ili kushughulikia maeneo hayo matano.
Baraza Kivuli la ACT-Wazalendo, liliundwa Februari mwaka 2022, likiwa na wasemaji kwa kisekta wenye jukumu la kuisimamia Serikali kwa kuhakikisha changamoto zinazowakabili wananchi zinapatiwa ufumbuzi.