ACT-Wazalendo ‘kutimua vumbi’ siku 28

Muktasari:
- Kuanzia Januari 12, 2024 Chama cha ACT-Wazalendo, kitaendesha uchaguzi wa kuwapata viongozi wa mikoa wa chama hicho, mchakato huo utasimamiwa na viongozi wakuu wa chama hicho waliojigawa kwa kanda.
Dar es Salaam. Vigogo watano wakiwemo wa wajumbe wa Kamati Kuu ya Chama wa ACT-Wazalendo, wanatarajiwa kutimua vumbi kwa siku 28 katika mikoa 26 nchini wakifanya mikutano ya kuimarisha chama hicho.
Ziara hiyo ya viongozi pia itahusika kusimamia mikutano mikuu ya mikoa itakayowachagua viongozi wapya watakaohudumu nafasi hizo kwa miaka mitano.
Makamu Mwenyekiti wa ACT-Wazalendo, Zanzibar Othman Masoud Othman ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar, atafanya ziara katika mikoa ya Dar es Salaam, Ruvuma, Mtwara, Lindi na Selous (mkoa wa kichama wenye majimbo ya Tunduru Kusini, Tunduru Kaskazini na Namtumbo).
Naye Makamu Mwenyekiti wa chama hicho, Tanzania Bara Dorothy Semu atakuwa kwenye mikoa ya Tanga, Kilimanjaro, Arusha, Manyara, Simiyu, Shinyanga na Kahama (mkoa wa kichama).
Vumbi la Naibu Katibu Mkuu (Bara), Joran Bashange litakuwa likitimka katika mikoa ya Morogoro, Iringa, Njombe, Songwe, Rukwa na Katavi.
Naye, Mjumbe wa Kamati Kuu ya ACT-Wazalendo, Ismail Jussa Ladhu afanya ziara mikoa Kigoma, Tabora, Singida na Dodoma.
Wakati wa mwenyekiti wa chama hicho, Juma Duni Haji, akielekea mikoa ya Kagera, Mwanza, Mara na Geita.
Katibu Mkuu wa ACT-Wazalendo, Ado Shaibu ameliambia Mwananchi leo Jumanne Januari 9,2024 kuwa ziara hiyo zinatarajiwa kuanza Ijumaa, Januari 12, 2024 na viongozi hao watakuwa katika mikoa husika.
Shaibu amesema katika ziara hiyo kuna viongozi watatumia siku moja hadi saba huku wengine wakitumia siku zisizopungua nne.
Ziara na uchaguzi huo ni maandalizi ya mkutano mkuu wa chama hicho, utakaokuwa ajenda ya uchaguzi mkuu utakaofanyika Machi, 2024 jijini Dar es Salaam.
Katika mkutano huo, ACT-Wazalendo, kinatarajia kuwapata viongozi wapya kuanzia nafasi ya Kiongozi wa Chama (KC) ambayo kwa sasa inashikiliwa na Zitto Kabwe anayemaliza muda wake wa miaka 10.
Macho na masikio yatakuwa ni katika nafasi ya KC, na tayari baadhi ya wanachama wa ACT-Wazalendo, akiwemo Jussa wameonyesha kuinyemelea huku Semu akitafakari na kusema wakati ukifika watamuona katika mchakato huo.
Naibu Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mawasiliano kwa Umma, Janeth Rithe amesema mbali na viongozi hao kushiriki mikutano hiyo, pia watapata fursa ya kusikiliza kero za wananchi wa maeneo husika na kuziwasilisha kwenye mamlaka husika.
“Tumegawa viongozi hawa kikanda hivyo, kila maeneo kutakuwa na ujumbe maalumu kulingana na changamoto zilizopo, lakini kutakuwa na ujumbe wa pamoja kuhusu mkutano mkuu wa chama utakaochagua viongozi wapya,” amesema Rithe.
Mkutano Mkuu wa Machi utakuwa ni wa tatu kufanyika tangu kuanzishwa kwa chama hicho mwaka 2014.