Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

ACT Wazalendo: Kuanzishwa tozo mwendelezo kuwaumiza wananchi

Muktasari:

  • Katika uchambuzi wa Bajeti ACT Wazalendo, kimejikita katika maeneo tisa ambayo kimedai yanaonyesha dhahiri Bajeti ya Serikali haiendi kutoa nafuu kwa umma, bali kuwaongeza maumivu na mzigo ma Watanzania hasa wenye kipato kidogo.

Dar es Salaam. Chama cha ACT Wazalendo kimesema mapendekezo ya Serikali kuanzisha tozo mpya kutadumaza fursa za kiuchumi na kupunguza uwezo wa wananchi kujikimu, badala ya kutoa unafuu kwa walioko katika mazingira magumu.

Sambamba na hilo, chama hicho kimetoa wito kwamba pendekezo la bajeti iliyotengwa na Serikali kwa ajili ya kugharimia uchaguzi, isitumiwe kwa namna yoyote inayoweza kuhujumu haki na uwazi wa mchakato huo, kwa kuwa fedha hizo ni mali ya wananchi.

Kauli hiyo imetolewa leo, Jumamosi Juni 21, 2025 na viongozi waandamizi wa ACT Wazalendo wakiongozwa na Kiongozi wa chama hicho, Dorothy Semu, wakati wakizungumza na waandishi wa habari kuhusu Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2025/26.

Katika uchambuzi huo, chama hicho kimejikita katika maeneo tisa kinayosema, yanaonyesha wazi kuwa mapendekezo ya bajeti hayakulenga kutoa unafuu kwa wananchi.

Miongoni mwa maeneo hayo, kimedai bajeti hiyo haionyeshi kwenda kutatua changamoto za msingi zinazowakabili wananchi, ukiwemo uhaba wa walimu na madarasa.

Nyingine ni gharama kubwa za matibabu, upungufu wa wataalamu na vifaatiba, kupanda kwa bei za mafuta, pamoja na marekebisho ya tozo.

 Hoja hizo zinatokana na hotuba ya Bajeti ya Serikali iliyowasilishwa bungeni Juni 12, 2025 na Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba, inayoliomba Bunge liidhinishe Sh56.4 trilioni kwa mwaka fedha 2025/26.

Bajeti hiyo ina vipaumbele mbalimbali ikiwemo kugharimia Uchaguzi Mkuu wa Oktoba na maandalizi ya viwanja kwa ajili ya michuano ya Afcon 2027.

Vipaumbele vingine ni kukuza sekta ya afya kwa kuhakikisha zinapatikana dawa za kufubaza virusi vya Ukimwi na huduma bima ya afya kwa wote.

Pia, kupunguza mzigo wa kifedha kwa wananchi wenye kipato kidogo kupitia nafuu ya kodi na ada, kuongeza uwekezaji katika elimu na miundombinu ili kujenga maendeleo endelevu.

Vipaumbele vingine vya Serikali ni kuhakikisha uwazi na uwajibikaji katika matumizi ya bajeti kwa manufaa ya wananchi.

Mbali na vipaumbele hivyo, bajeti hiyo inalenga utekelezaji na uendelezaji wa miradi ya kimkakati, kuimarisha sekta za uzalishaji, rasilimali watu na kuboresha mazingira ya biashara.


Tozo

Kuhusu Semu amesema mapendekezo ya baadhi ya tozo zilizoanzishwa ambazo zinaenda kuongeza maumivu kwa wananchi ni pendekezo la tozo ya Sh10 kwa kila lita ya mafuta ya petroli, dizeli na mafuta ya taa.

“Tozo hii inaongeza ugumu wa gharama za maisha kwa wananchi, petroli na dizeli ndio zinazosukuma sehemu kubwa ya maisha ya wananchi, tozo hii itaongeza sana gharama za usafiri.

“Tozo ya Sh500 kwa kila tiketi inayotolewa na mtoa huduma za usafirishaji kwa njia ya treni. Serikali badala ya  kuhimiza matumizi ya treni kwa kuhakikisha inakua na bei ya chini, na kutengeneza faida itakayosaidia umma wa Watanzania, inazidi kuweka ugumu," amesema na kuongeza kuwa:

“Ushuru wa bidhaa kwenye bidhaa kwenye huduma za mawasiliano ya kielekroniki kutoka asilimia 17 had asilimia 17.5. Ushuru huu utaongeza makato kwa wananchi wa chini wanaofanya malipo kwa njia ya mtandao,”

Kwa mujibu wa Semu, ushuru huo utaongeza mzigo zaidi licha ya makato makubwa yaliyopo hivi sasa bado Serikali inaendelea kuminya wananchi kwa kuwaongezea ushuru.

“Tunaitaka Serikali ya CCM kuondoa mara moja tozo zote zinazozuia biashara ndogo kuchipua, wachimbaji wadogo kunufaika, viwanda vya ndani na rasilimali za ndani. Hatuoni namna ambayo Serikali ya CCM itakayoleta bajeti ya ahueni,” amesema Semu.


Alichokisema Dk Mwigulu akiwasilisha bajeti


Wakati akiwasilisha mapendekezo ya bajeti hiyo, Dk Nchemba alisema mabadiliko ya kisera yanayoendelea duniani yamesababisha wadau muhimu wa maendeleo kupunguza misaada iliyokuwa inatolewa kwa ajili ya huduma za afya ikiwemo kukabiliana na kudhibiti magonjwa mbalimbali hususan Ukimwi.

Kutokana na hilo, Dk Mwigulu alililieleza Bunge kuwa Serikali inapendekeza kuanzisha vyanzo mbadala vya mapato ili kupunguza nakisi ya kibajeti iliyotokana na kupungua kwa misaada hiyo kwa kufanya marekebisho katika sheria mbalimbali. 

Dk Mwigulu alisema Serikali inapendekezwa asilimia 70 ya mapato yatakayoongezeka ipelekwe kwenye Mfuko wa Udhamini wa Kudhibiti Ukimwi (ATF) na asilimia 30 ipelekwe kwenye Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya kwa Wote.

Alisema Serikali itafanya marekebisho kwenye Sheria ya Ushuru wa barabara na mafuta, Sura ili kutoza kiasi cha Sh10 kwa kila lita ya mafuta ya petroli, dizeli na mafuta ya taa.

“Kutoza Sh 500 kwa kila tiketi inayotolewa na mtoa huduma za usafirishaji kwa njia ya treni, na kutoza Sh1,000 kwa kila tiketi inayotolewa na mtoa huduma za usafirishaji kwa njia ya anga,”alisema Dk Mwigulu.


Bajeti ya uchaguzi

Kuhusu fedha zilizotengwa kwa ajili ya uchaguzi, Semu amesema ACT Wazalendo, kisisitiza zitumike kwa malengo yaliyokusudiwa kwa sababu ni fedha za Watanzania na si za chama chochote cha siasa.

“ACT Wazalendo tunasisitiza kwamba, hatutaki fedha zitumike kuumiza wananchi, hatutaki fedha hii itumike kupora uamuzi ya wananchi, tunataka uchaguzi huru na wa haki ili vyama vyote vitapata haki na uwanja sawa bila bughudha,” amesema.

Kwa nyakati tofauti Serikali imekuwa ikisisitiza uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba baadaye utakuwa huru na haki, atakayeshinda atatangazwa.

Semu amesema ACT Wazalendo imesisitiza kuwa mabadiliko ya sheria ya Tume Huru ya Uchaguzi (INEC) hayaridhishi na hayatoi nuru na mwanga wowote wa kuchochea mabadiliko ya kweli yatakayohakikisha kufanyika kwa uchaguzi wa haki, kweli na wenye kuaminika.

Kutokana na hilo, Semu amesema chama hicho kinaendelea kukazia ushauri wao wa kutaka makamishna wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi wapatikane kwa ushindani, tume iitishe mchakato wa usaili kama inavyotamkwa na sheria

“Wakurugenzi wa halmashauri wasiwe wasimamizi wa majimbo, Tume iajiri watumishi wasimamizi wa uchaguzi na wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi,”

“Mawakala wafanye shughuli zao bila bughudha na wasizuiwe wagombea wote wasienguliwe, wananchi wapewe nafasi ya mwisho kuamua viongozi wanaowataka,” amesema Semu. 


Bei za petroli, dizeli

Waziri Mkuu Kivuli wa ACT Wazalendo, Isihaka Mchinjita amesema licha ya pendekezo mapya ya Serikali ya kuongeza tozo kwenye bidhaa hizo, gharama ya mafuta ya petroli, dizeli  na mafuta ya taa bado zipo juu na kusababisha athari za bei za bidhaa zingine.

“Serikali inayojali watu wake ilipaswa kufikiria njia bora za kutatua tatizo hili la mafuta. Jambo la kushangaza ni bado Serikali imeng’ang’ania kuweka katika kila lita moja ya mafuta,” amesema Mchinjita.

Mbali na hilo, Mchinjita ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa ACT Wazalendo Bara, amedai bado kuna changamoto ya gharama za matibabu na kusababisha Watanzania kuwa na maisha na umaskini.

“ACT Wazalendo tumekuwa tukisisitiza wakati wote kwa kuitaka Serikali kuwekeza fedha ili kugharamia matibabu kwa watu wote nchini bila kuwepo na matabaka,”

“Pendekezo la ACT Wazalendo ni kutaka mfumo wa hifadhi ya jamii uongezwe wigo kutoka kwenye kundi dogo la watu wazima milioni 1.8 hadi milioni 18.2 ili kuhakikisha Watanzania wote wanakuwa na bima ya afya itakayowezesha kupata matibabu stahiki bila kujali vipato vyao,”amesema Mchinjita.




Sekta ya miundombinu

Waziri Kivuli Uchukuzi wa ACT Wazalendo, Halima Nabalang'anya amesema katika mwaka wa fedha 2025/26 Serikali imeendelea kutenga bajeti kiduchu kwa ajili ya ujenzi wa barabara mpya, ukarabati na matengenezo.

“Kwa upande mwingine, bajeti ya Serikali haiendi kujibu kilio cha kusuasua kwa miradi kutokana na kutoongeza bajeti ya miradi ya maendeleo,” amedai Halima.