1,000 wachukua fomu ACT-Wazalendo kuelekea Uchaguzi Mkuu

Katibu wa Kamati ya Uchaguzi chama cha ACT-Wazalendo, Mhene Said Rashid akizungumza na waandishi wa habari makao makuu ya chama Vuga Unguja. Picha na Zuleikha Fatawi
Muktasari:
- Mhene amesema urejeshaji wa fomu umekamilika, kwa sasa wanaanza mchakato wa kura za maoni ambapo utaanza Juni 18 hadi Jalai 7 ili kupata wagombea watakaokiwakilisha chama hicho katika Uchaguzi Mkuu Oktoba mwaka huu.
Unguja. Zaidi ya wanachama ya 1,000 wa chama cha ACT-Wazalendo wamechukua fomu za kugombea nafasi mbalimbali za uongozi kupitia chama hicho ikiwemo urais, udiwani, uwakilishi na ubunge.
Hayo yameelezwa leo Ijumaa Juni 13, 2025 na Katibu wa Kamati ya Uchaguzi wa chama hicho, Mhene Said Rashid wakati akizungumza na waandishi wa habari makao makuu ya chama Vuga Unguja.
Mhene amesema urejeshaji wa fomu umekamilika, kwa sasa wanaanza mchakato wa kura za maoni ambapo utaanza Juni 18 hadi Jalai 7 ili kupata wagombea watakaokiwakilisha chama katika Uchaguzi Mkuu Oktoba mwaka huu.
Mchakato wa kuchukua fomu ulifunguliwa Aprili mosi kwa ngazi ya ubunge, udiwani na uwakilishi na kukamilika Aprili 10, kuanzia Aprili 12 hadi 17 ilikuwa kwa ngazi ya Urais.
Amesema ifikapo Julai chama hicho kitakuwa tayari kimeshakamilisha hatua zote za kuwapata wapeperusha bendera katika uchaguzi huo.
"Nachukua fursa hii kutoa taarifa kuwa dirisha la kura za maoni limefunguliwa rasmi na itafanyika ndani ya siku saba katika majimbo 50 ya Unguja na Pemba," amesema.
Katibu huyo, ametoa wito kwa wananchama na viongozi kujitokeza kwa wingi ili kutekeleza haki yao ya kidemokrasia kwa kuchagua viongozi ambao watakuwa na sifa kwao
Katibu wa Habari, Uenezi na Mawasiliano na Umma wa chama hicho, Salim Bimani amesema chama kinaingia katika uchaguzi Mkuu kwa kupambana na kujiamini kwa lengo la kushinda.
Mbali na hayo, Bimani amewakaribisha wananchama kutoka chama chochote wanaotaka kujiunga na chama hicho wajiunge bila hofu kwani kipo wazi kuwapokea