Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

ACT Wazalendo yawapigia rada wabunge 19 wa Chadema

Muktasari:

  • Ukiacha lengo kuu la kuongeza wigo zaidi kwa wanachama wake kuchukua fomu hizo, pia, uamuzi huo una lengo la kuvuna wabunge 19 wa viti maalumu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).

Dar es Salaam. Uamuzi wa ACT Wazalendo kuongeza muda kwa makada wake kuchukua na kurudisha fomu za ubunge na udiwani, una mengi yaliyojificha nyuma yake, Mwananchi limebaini.

Ukiacha lengo kuu la kuongeza wigo zaidi kwa wanachama wake kuchukua fomu hizo, pia, uamuzi huo una lengo la kuvuna wabunge 19 wa viti maalumu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).

Si hivyo tu, chama hicho kikuu cha upinzani Zanzibar, kinaongeza muda kama mtego wa kuwa jukwaa mbadala kwa wabunge wa sasa wa Chama cha Mapinduzi (CCM) ambao hawatateuliwa wakati wa mchakato wa kura za maoni.

Aprili 18, 2025, ACT Wazalendo, kwa mara ya kwanza kilifungua pazia la uchukuaji na urejeshaji wa fomu za ubunge, ubunge wa viti maalumu, uwakilishi na udiwani mchakato uliotarajiwa kuhitimishwa Mei 31, 2025.

Wakati huohuo, CCM ilitangaza ratiba ya awali ikionyesha uchukuaji na urejeshaji wa fomu za udiwani, uwakilishi na ubunge ungeanza Mei Mosi hadi Mei 15, 2025, kisha hatua za uteuzi, hata hivvyo kilibadili gia angani kwa kusogeza mbele mchakato huo kwa sababu mbalimbali.

Baada ya Mei 31, 2025 kupita, Juni 8, 2025 Naibu Katibu Idara ya Habari, Uenezi na Uhusiano na Umma wa ACT Wazalendo, Shangwe Ayo alitangaza chama hicho kimeongeza muda wa uchukuaji na urejeshaji wa fomu kuanzia Juni 8 hadi Juni 30, 2025.

Uamuzi wa kuongeza muda uliazimiwa na kikao cha Kamati ya Uongozi Taifa ya ACT Wazalendo, kilichoketi Juni 6, 2025 na kupendekeza muda wa nyongeza baada ya kupokea taarifa ya mwenendo wa uchukuaji na urejeshaji wa fomu katika chama hicho.

“Uamuzi huu unakusudia kutoa nafasi kwa wapambanaji mbalimbali wanaokusudia kulitumia jukwaa la ACT Wazalendo kama jukwaa la kimapambano kuilinda na kuitetea demokrasia kwa kugombea kwenye uchaguzi mkuu 2025 kupata fursa hiyo,” alisema Ayo katika taarifa hiyo.

Hiyo ilikuwa mara ya pili kwa chama hicho kuongeza muda kwa wanachama wake kuchukua na kurejesha fomu hizo, mara ya kwanza iliongeza muda kuanzia Aprili 18 hadi Mei 25, 2025 kwa upande wa Tanzania Bara.


Kilichomo nyuma ya pazia

Licha ya sababu mbalimbali zinazotolewa ikiwemo kutoa fursa pana kwa makada wa chama hicho na wengine watakaohamia, jambo jingine lilipo nyuma ni kusubiria Bunge kuvunjwa ili kuvuna wanachama wapya hasa wabunge 19 wa Chadema na wengine watakaokatwa CCM.

Ingawa kati ya wabunge 19 baadhi yao wamejipambanua wazi kuelekea CCM, lakini wapo miongoni mwao hawajatangaza ni wapi wataelekea ili kupata jukwaa mbadala la kufanya shughuli za kisiasa.

Vyanzo vya ndani ya ACT Wazalendo vinaeleza kuwa pamoja na mambo mengine, chama hicho kinatoa nafasi kwa wabunge kujiunga baada ya Bunge kuvunjwa Juni 27, 2025.

Hata hivyo, Mwananchi limedokezwa kuwa hata baada ya pazia la uchukuaji na urejesha fomu kufungwa rasmi Juni 30, 2025, ACT Wazalendo kitatoa nafasi kwenye baadhi ya majimbo kwa makada wa CCM kugombea baada ya uchambuzi wa kina wa kukubalika kwa wagombea husika kutoka CCM na vyama vingine.


Ratiba ya CCM ilivyo

Kwa mujibu wa ratiba ya CCM mchakato wa uchukuaji na urejeshaji wa fomu za udiwani, ubunge na uwakilishi utaanza Juni 28 hadi Julai 2, 2025 ukifuatiwa na vikao vya kuchuja wagombea vitakavyoanza Julai 4 hadi 8.

Kati ya Julai 9 hadi 10, vikao vya kamati za siasa za mikoa zitaketi na kuteua wagombea watatu wa udiwani, ubunge na uwakilishi, kisha kutoa mapendekezo yake kwa kamati kuu ya halmashauri kuu ya Tanzania Bara na ile ya kamati kuu maalumu ya halmashauri kuu ya Zanzibar.

Ratiba hiyo inaonyesha kuwa Agosti 17 hadi 18, kikao cha Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM ya Taifa kitaketi na kufikiria na kutoa mapendekezo yake kwa Halmashauri Kuu ya CCM ya Taifa kuhusu wanachama waliomba ubunge na ujumbe wa Baraza la Wawakilishi wa Jimbo na viti maalumu.

Wakati Agosti 20, 2025 kikao cha Halmashuri Kuu ya CCM ya Taifa kitaketi kufanya uteuzi wa mwisho wa majina ya wanachama wanaoomba nafasi ya ubunge na ujumbe wa Baraza la Wawakilishi wa majimbo na viti maalumu.

Hata hivyo, taarifa zingine zinadai kuwa ofisi ya katibu mkuu wa ACT Wazalendo, ndio imepewa meno ya kutoa fursa kwa wagombea wenye nguvu kuchukua fomu za ubunge na udiwani baada ya mchakato kufungwa Juni 30.

Hali kama hiyo, iliwahi kutokea katika chaguzi za mwaka 2015 na 2020 ambapo wagombea Modestus Kilufi aliyekatwa na CCM alihamia ACT Wazalendo na kupewa nafasi ya kuwania ubunge wa Mbarali mkoani Mbeya.

Vivyo hivyo kwa Mtutura Mtutura ambaye baada ya jina lake kukatwa na CCM alitimkia ACT Wazalendo, kilichompa nafasi ya kuwania ubunge wa Tunduru Kusini mkoani Ruvuma.


Alichokijibu Ado

Mwananchi leo Jumatatu Juni 10, 2025 lilimtafuta Katibu Mkuu wa ACT Wazalendo, Ado Shaibu kuelezea hali hiyo, ambapo amejibu kuwa hatua ya kuongeza muda inakusudia kutoa muda zaidi kwa wanachama wa Bara kuchukua fomu.

“Nafahamu wapo wanachama kadhaa wa vyama ikiwemo wabunge wanaotaka kujiunga na ACT Wazalendo (ambao hakuwa tayari kuwataja), hivyo nyongeza ya muda itawafaa kwa sababu Bunge litakuwa limevunjwa.

“Vivyo hivyo kwa upande wa madiwani, mabaraza yatakuwa yamevunjwa, pia, hivyo itakuwa fursa nzuri kwao kujiunga na ACT Wazalendo,” amesema Ado.