ACT-Wazalendo, CCM waliamsha tena Zanzibar

Dar es Salaam. Je, ni kwa nini Chama cha ACT-Wazalendo kimekuwa kikirejea mara kadhaa kauli ya kutaka kujitoa katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK?).
Akizungumza jana kwa simu na gazeti hili, Mwenyekiti wa chama hicho, Juma Duni Haji ametaja sababu akisema suala la demokrasia katika uwanja wa siasa Zanzibar halijafanyiwa kazi.
Alifafanua kuwa, Desemba 2020 aliyekuwa Mwenyekiti wa chama hicho, hayati Maalim Seif Sharif Hamad, akiongoza ujumbe wa ACT-Wazalendo walifanya mazungumzo na Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi, pamoja na mambo mengine mazungumzo hayo yalilenga kuleta utulivu baada ya uchaguzi.
Katika mazungumzo hayo, alisema walipendekeza kufanyika mabadiliko katika taasisi mbalimbali, ikiwemo Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) kuwezesha kuwapo uchaguzi huru na wa haki ifikapo mwaka 2025, pendekezo analodai halijatekelezwa.
“Tulipendekeza kufumuliwa sheria ya uchaguzi ya Zanzibar na kufanyiwa maboresho, mfano sheria inasema kupiga kura siku mbili, hivi kweli watu 500,000 wanaweza kupiga kura kwa siku mbili?” alihoji Duni.
Alisema licha ya Rais Mwinyi kuwaachia huru wanachama wa ACT-Wazalendo walioathiriwa katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2020, hawajapelekwa hospitali wala kufidiwa.
“Hawa walitakiwa kufidiwa, bado hakuna kilichofanyika hadi sasa, waliokuwa wagonjwa hawajapelekwa hospitali,” alisema.
Alisema baadhi ya mambo yaliyolalamikiwa katika uchaguzi wa mwaka 2020 ni uwepo wa Mkurugenzi wa ZEC, Thabit Idarous Faina ambaye bado anaendelea na majukumu yake.
Duni, maarufu kama ‘Babu Duni’ alidai baadhi ya watendaji wa Serikali wanadharau makubaliano waliyoingia na Dk Mwinyi, akitoa mfano mmoja wa mawaziri wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), aliwahi kutamka kuwa hamtambui Makamu wa Kwanza wa Rais, Othman Masoud Othman.
“Hii ina maana gani? Yaani anamtambua Dk Mwinyi na Hemed Suleiman Abdulla (Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar). Sasa tuamini vipi katika kauli ya waziri anayesema hivi na Rais yupo? Hakuna mtu yeyote aliyesema hayo ni maneno yake (waziri)” alisema.
Duni alisema lugha zinazotolewa na baadhi ya viongozi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) na Serikali zinaidhalilisha ACT-Wazalendo, ndiyo maana Othman alisema itafika mahali chama hicho, kitajitoa ndani ya SUK.
Juzi akihutubia katika mkutano wa hadhara uliofanyika Mtoni Kidatu, Othman ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa ACT-Wazalendo Zanzibar, alisema waliingia SUK kwa masharti na malengo maalumu, na iwapo wakiona hayatekelezwi wataondoka bila kuambiwa na mtu yeyote.
Othman alisema wapo wanaoshangaa kuhusu hatua yao ya kuikosoa Serikali wakati wapo ndani ya SUK, akisema ndiyo wajibu wao wa kuwasemea wananchi na wasichukuliwe kama maadui au mahasimu.
“Wanachama mlituambia tubaki kwenye SUK kwa masharti, iwapo yale tunayoyasimamia ambayo ndiyo dhamira yetu kuona yanatekelezwa. Tuliingia SUK na zana zetu, tukitaka kutoka tutatoka na zana zetu, hakuna mtu wa kutuambia wala kutupa maarifa,” alisema Othman.
Katika hilo la kujitoa SUK, Duni alisema: “Ila tupo ‘serious’ (tupo makini) ninyi sikilizeni tu siku zinakuja.
Kauli ya CCM
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM Zanzibar, Khamis Mbeto alisema malalamiko yote ya ACT-Wazalendo hayana msingi.
Alisema Taifa lolote linaongozwa kwa Katiba na sheria, huku akihoji wanaotakiwa kulipwa fidia ni kwa kosa lipi, wakati Dk Mwinyi hakuwa Rais.
“Unapozungumzia uwanja sawa wa siasa ni upi? Mbona wanafanya mikutano ya hadhara na kuwatukana viongozi wa Serikali kuwa ni wezi na walaji, halafu muda huohuo unataka kupewa heshima wakati kiongozi mkuu humheshimu,” alisema na kuongeza:
“Hawa ni waongo, wanatafuta huruma, hivi unaposema Othman haheshimiwi wakati yupo kikatiba, si kweli. Ndiyo maana baada ya Rais, anatajwa yeye wakiwa wote katika shughuli,” alisema Mbeto.
Alisema muundo wa ZEC una makamishna kwa uwakilishi sawa wanaotoka vyama vya CCM na ACT- Wazalendo.
Alisema Faina ni mtendaji tu ila uamuzi unatolewa na makamishna wa tume.
“Dk Mwinyi anafuata Katiba, hayo mengine ni hisani,” alisema Mbeto.
Mwaka 2022 chama hicho, kiliitisha maoni kwa wanachama wake kuhusu mwenendo wa SUK, iwapo kijitoe au kiendelee kubaki.
Wanachama wa ACT-Wazalendo walishauri kubaki ndani ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa.
Mchakato wa ukusanyaji maoni uliendeshwa na Othman, msingi wa jambo hilo ulitokana na hatua ya Rais Mwinyi kumteua Faina kuwa Mkurugenzi wa ZEC.
Maoni ya wachambuzi
Hali ikiwa hivyo, baadhi ya wachambuzi wa siasa waliozungumza na gazeti hili jana walisema hatua ya ACT-Wazalendo kutaka kujitoa SUK huenda inachangiwa na joto la kisiasa.
Na kwa upande mwingine walisema huenda kinatikisa kibiriti kuelekea katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.
Mchambuzi wa masuala ya siasa nchini, Kiama Mwaimu alisema Taifa linaelekea katika chaguzi na kila chama cha siasa kinataka kupata mtaji wa wanachama ili kuwa imara zaidi, hivyo wanachokifanya ACT-Wazalendo ni kutishia.
“Lakini kwa jinsi ninavyoona viongozi hawana njia nyingine, labda wakubali kujitoa ndani ya SUK ili kuonekana mbele ya watu wamejitoa sadaka. Kama wakibaki hadi uchaguzi watakuwa na mazingira magumu,” alisema.
“Wakitaka kupata uhalali wa wanachama na wananchi wa Zanzibar, basi wajitoe kweli ndani ya SUK, si wana sababu matakwa yao kutotimizwa? Si kungoja hadi uchaguzi ujao wataonekana waongo machoni mwa watu,” alisema Mwaimu.
Mchambuzi mwingine wa siasa, Ali Makame, alidai sababu za ACT-Wazalendo kutaka kujitoa ndani ya SUK ni kuwa hawana hoja ya kuuza kwa Wazanzibari.
Alisema baadhi ya vyama vya siasa vimezoea ili kujijenga lazima viikosoe Serikali hata kama inafanya kazi vizuri.
“Hiki wanachokifanya ni kutikisa kibiriti kwa Serikali au CCM ili kuonekana Zanzibar inarejea katika hali ya siasa ya sintofahamu, lazima ACT-Wazalendo wajifunze kuleta mfumo mpya kufanya siasa ili kuendana na wakati,” alisema Makame.
Naye, Dk Richard Mbunda, alisema mantiki ya kuwapo ndani ya SUK ni kugawana madaraka, kila mmoja awe na nafasi ya kimamlaka ya kutawala, lakini kwa Zanzibar haitoi fursa hiyo bali mmoja anakuwa yupo tu.
“Hata nafasi za uwaziri wanazopewa ni chache, lakini haziwafanyi kuwa na ushawishi mkubwa ndani ya SUK, ndiyo maana kumekuwa na mvutano wa muda mrefu katika suala hili,” alisema Dk Mbunda, ambaye ni Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).
Dk Mbunda alisema hatua ya ACT-Wazalendo ni mpango mkakati wa kusukuma ajenda kwa wahusika kuboresha, na namna nzuri ya kuendesha Serikali ya Umoja wa Kitaifa.
“Lakini kwa sababu uchaguzi unakaribia na ACT hawapendi kuonekana wamebweteka kwani wanaangaliwa na vyama vingine kama sehemu ya Serikali, ndiyo maana wanapambana kuonyesha wao ni wapinzani,” alisema.
Alisema: “Kwa hiyo ni mpango mkakati wao (ACT), lakini kujitoa si suluhisho kwa sababu ukijitoa Serikali haitasimama itajiendesha tu, kikubwa wapambane ili kupata fursa bora zaidi”.
Kwa upande wake, mchambuzi wa masuala ya siasa, Enzi Talib Abood alisema huenda chama hicho kikajitoa ndani ya SUK.
Alisema endapo ACT-Wazalendo ikijitoa ndani ya SUK, uchaguzi mkuu wa 2025 utakuwa mgumu zaidi.
“Sishangai wanavyozungumza watatoka. Wanaweza kutoka kweli, sikiliza kauli za Jussa (Ismail-mjumbe wa kamati kuu ACT-Wazalendo), Mansoor Himid (mwanachama), Juma (Duni Haji-Mwenyekiti ACT) kisha anachokisema Othman, ambaye akiwa kwenye majukwaa anazungumza vingine lakini akiwa serikalini anazungumza vingine.
“Ukifanya uchambuzi wa siasa kwa hali ya Zanzibar, nionavyo kuna uwezekano mkubwa wa ACT kujitoa, lakini wanangojea karibu na uchaguzi ili kutengeneza mshtuko kwa Wazanzibari,” alisema.
Talib alisema kauli ya ACT-Wazalendo ya mara kwa mara maana yake wameshajiandaa kutoka.