Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

2023 na majaribio magumu ya kidemokrasia kwa Samia

Juzi, Desemba 25, 2023, ilikuwa Sikukuu ya Krismasi. Ni siku ya kumbukumbu ya kuzaliwa Yesu Masiya kwa Wakristo wengi ulimwenguni. Kwa utamaduni wa walimwengu wenye kufuata kalenda ya Gregory, Noel ni mwanzo wa sikukuu za mwisho wa mwaka.

Zimebaki siku nne kuingia mwaka 2024. Inakaribisha tafsiri kuwa mwaka 2023 upo jua la Magharibi. Punde utaagwa na kukaribisha mwingine mpya. Ni kipindi kizuri kuzitafakari siku 365 zinazoelekea tamati.

Tafakuri kuanzia kifo cha mwanadiplomasia Bernard Membe, mwanasheria nguli Nimrod Mkono, mfanyabiashara mashuhuri Mohammed Raza, Kamishna Mwandamizi Msaidizi wa Polisi mstaafu, Zelothe Stephen na Mwenyekiti wa zamani wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (Zec), Jecha Salim Jecha. Wote hao wamefariki mwaka 2023.

Mapinduzi ya kijeshi Niger na Gabon, songombingo la Donald Trump kuhusu mashitaka dhidi yake na kinga aliyonayo, kuelekea uchaguzi wa urais Marekani 2024, mauaji ya raia wasio na hatia Israel na Gaza (Palestina), vita vya kiraia Sudan na India kuipiku China kwa idadi kubwa ya watu duniani, ni mambo ya mwaka 2023 yaliyogonga vichwa kweli.

Mwaka 2023 unaweza kuwa umemgusa kila mtu kwa namna yake. Waziri Mkuu na Makamu wa Kwanza wa Rais mstaafu, John Malecela alimpoteza mwanaye William “Le Mutuz”, Mei 14, 2023. Le Mutuz alikuwa na athari kubwa kwenye mitandao ya kijamii Tanzania.

United Kingdom “UK”, Mfalme wao, Charles III, alitawazwa ufalme Mei 6, 2023. Wataalamu wa hali ya hewa wameutaja mwaka 2023 kuwa wenye joto zaidi kupata kutokea. Dunia haijapata kuwa na joto hili ndani ya miaka 125,000 iliyopita.

Maporomoko ya matope Katesh, Hanang, mabadiliko makubwa ya Baraza la Mawaziri Agosti 30, 2023, kunyanyuliwa upya kwa Paul Makonda kwenye uso wa kisiasa na anguko la Daniel Chongolo, aliyelazimika kujiuzulu cheo cha Katibu Mkuu CCM. Ni tafsiri anuwai ya 2023.


Majaribio ya Samia

Rais Samia Suluhu Hassan aliuanza mwaka 2023 kwa kuruhusu mikutano ya hadhara ya vyama vya siasa. Mtangulizi wake, Dk John Magufuli, alipiga marufuku mikutano na maandamano ya kisiasa tangu mwaka 2016.

Uamuzi huo wa Rais Samia ulifuatia mapendekezo ya Kikosi Kazi kilichoundwa kuchunguza mazingira ya shughuli za kisiasa na kutoa mapendekezo ya namna bora. Januari 3, 2023, siku Rais Samia aliporuhusu mikutano, ilikuwa tabasamu kwa kila mtu. Shangwe kwa wapenda siasa.

Tangu Machi 19, 2021, Rais Samia alipokula kiapo kuongoza Dola ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, nchi ilianza kupumua hewa safi. Uhuru wa maoni ulirejea, wanasiasa wa upinzani walifika Ikulu kuzungumza na Rais Samia. Kutoka Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe hadi Kiongozi wa ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe.

Tamko la Rais Samia Januari 3, 2023, lilitengeneza kilele cha mageuzi makubwa ya kisiasa. Vyama vya siasa kuruhusiwa kufanya siasa waziwazi. Kisha wanasiasa waliokimbia nchi walirejea; Makamu Mwenyekiti wa Chadema, Tanzania Bara, Tundu Lissu, mbunge wa zamani wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema na aliyekuwa Mbunge wa Nyamagana (Chadema), Ezekia Wenje.

Vyama vilianza kufanya mikutano ya hadhara. Chadema walianzia Viwanja vya Furahisha, Mwanza, Januari 21, 2023, ACT Wazalendo waliibukia Zakhem, Mbagala, Dar es Salaam, Februari 19, 2023. Vyama vingine pia vilifanya mikutano.

Septemba 11, 2023, katika mkutano wa Baraza la Vyama vya Siasa na wadau, Rais Samia alitoa hotuba ambayo ungeweza kuitafsiri kuwa alijutia uamuzi wake wa Januari 3, 2023. Rais Samia alikuwa mbogo.

Hotuba ya Rais Samia Januari 3, 2023, alipokuwa anaondoa marufuku ya mikutano ya hadhara kwa vyama siasa, alizungumza akitabasamu, mithili ya mama anayewanasihi watoto wake.

“Kama waungwana, kama wastaarabu, Watanzania wenye sifa ndani ya dunia hii, niwaombe sana ndugu zangu, ruhusa hii tunaitoa twendeni tukafanye siasa za kistaarabu. Siasa za kujenga, zilizopevuka, siyo za kubomoa. Hapa tulipofika tusirudi nyuma,” Rais Samia Januari 3, 2023.

Ilipofika Septemba 11, 2023, Rais Samia alifoka: “Uhuru wa maoni una ukomo wake, siyo tu kisheria hata kibinadamu. Mtu mwenye wazazi, aliyelelewa na kupitishwa kwenye dini, kuna maneno hawezi kutamka. Mtu anatukana mpaka unajiuliza, kinywa hichohicho ndicho anapitishia chakula?”


Tuyaelewe majaribio

Kutoka Januari 3, 2023 mpaka Septemba 2023, ungeweza kuona kuwa Rais Samia alikabiliana na majaribu makubwa ya kisiasa. Bahati mbaya, alibanwa na maneno ya Rais wa pili wa Tanzania, Ali Hassan Mwinyi.

Katika kitabu chake cha “Mzee Rukhsa; Safari ya Maisha Yangu”, Mwinyi ameandika kuwa demokrasia ni jini, ukishalitoa kwenye chupa huwezi kulirejesha. Januari 3, 2023, Rais Samia alilitoa jini kwenye chupa. Ni vigumu kulirejesha.

Hata hivyo, hotuba yake ya Septemba 11, ilidhihirisha kuna mahali aliingia kwenye majaribu ya kutamani kuirejesha nchi kule ambako mtangulizi wake aliipitisha. Kudhibiti mikutano ya hadhara, kuminya demokrasia. Pengine aliwaza kwa msemo wa Kiswahili: “Asiye fadhila hafadhiliki.”

Pengine Rais Samia, alitamani kurudisha tarehe nyuma ili awaze upya kuhusu kuruhusu mikutano ya vyama vya siasa. Bahati mbaya, kwa mzunguko wa kawaida wa sayari, hakuna namna tarehe zinaweza kurudi nyuma.

Kisichopaswa kusahaulika ni kuwa uamuzi wa kuruhusu mikutano ya kisiasa ulikuwa moja ya uamuzi wa busara kufanywa na Rais Samia. Mikutano ya kisiasa ni haki kikatiba na kisheria. Kifungo kilikuwa batili. Ruhusa ilikuwa kurejesha haki. Rais Samia hapaswi kujilaumu kutenda haki.

Taifa linaloongozwa kidemokrasia ni bora kwa sababu linatoa taswira kuwa wananchi wote wana haki sawa katika kuchagua viongozi wao. Taifa la kidemokrasia, huonesha kuwa Serikali inawajibika kwa wananchi.

Wito wa juu kabisa kwa Rais kwenye nchi ya kidemokrasia ni yeye kuwa mvumilivu kuliko wapinzani wake. Aoneshe ukomavu na ustahimilivu zaidi ya wengine. Adhihirishe kiwango cha juu cha uungwana wa kisiasa. Awe na kifua kipana cha kupokea na kusamehe.

Rais katika nchi ya kidemokrasia, anapaswa kuwa na kauli thabiti. Anaposema anaruhusu mikutano, hapaswi baada ya muda akereke na kuifuta. Hiyo itadhihirisha woga wake. Rais anatakiwa kuwa na ngozi ngumu, yenye kumwezesha kupokea mishale pasipo sumu kupenya kwenye moyo na ini.

Hotuba ya Rais Samia Septemba 11, ilimpambanua kuwa mwenye matamanio hadi ya malezi ya Watanzania. Jinsi alivyokuzwa kimaadili, akapitishwa madrasa kusoma dini, akafunzwa ustaarabu wa kuishi na jinsi ya kudumisha uhusiano wa kijamii, anatamani iwe hivyo kwa kila Mtanzania.

Hiyo ndiyo sababu anashangazwa na anaowasema wanatukana. Tena, inaonekana wanamuumiza. Bahati mbaya, Tanzania ni Taifa mchanyato (diverse). Ni mchanganyiko kuanzia jamii za makabila, dini tofauti, madhehebu mbalimbali, wapagani hadi chimbuko la vizazi.

Pamoja na nadharia kuwa Watanzania ni watu wema ila si wakati wote ustaarabu wako unaweza kufanana na wa mwingine. Yupo aliyekuzwa kufokeana na yeyote bila kujali umri. Mwingine alilelewa kwa kuendekezwa hata alipotukana wazazi wake.

Tanzania ni moja; watu wanaua wengine. Matukio ya ubakaji hayajakauka. Watoto wanapiga wazazi wao. Walemavu wa ngozi wanauawa na kukatwa viungo. Ujambazi wa kutumia silaha upo. Rushwa na ufisadi vimeweka makazi ya kudumu. Matendo yote hayo yanafanywa na Watanzania.


Ripoti ya CAG

Rais Samia aliwahi kusema kuwa hahitaji kuongea kwa vishindo ili ujumbe ufike. Hata hivyo, nyakati zinabadilika. Hotuba yake kwenye mkutano wa Baraza la Vyama vya Siasa, siyo tu alihutubia kwa vishindo, bali pia alisimama pembeni ya kitovu cha uvumilivu.

Je, ule upole na uongeaji wake wenye nakshi za utulivu ndiyo hulka yake? Kama ndivyo, basi hulka imebadilika. Ikiwa alikuwa akijitahidi kuuishi uvumilivu, basi ama uvumilivu ulimshinda au alichoka kujitahidi.

Endapo nyakati zilizopita alikuwa anaficha kucha, mwaka 2023 aliamua kuyaacha makucha wazi. Alionesha utayari wa kumrarua yeyote ambaye hatakwenda naye vema. Samia wa mwaka 2023 si yule wa kabla ya urais au wa miaka miwili nyuma!

Aprili 2023, Rais Samia alipopokea ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), hesabu za mwaka 2021/22, kwa mara ya kwanza alionesha ‘umbogo’ wake. Alichukizwa na ubadhirifu na udanganyifu wa wasaidizi wake serikalini.

Kutoka ripoti ya CAG hadi nyongo aliyotema kwenye mkutano wa Baraza la Vyama vya Siasa, bila shaka Rais Samia hawezi tena kusema,“sio mpaka nizungumze kwa vishindo ndio ujumbe ueleweke.”


DP World          

Hakosekani wa kusema kuwa Rais Samia alivumilia mengi. Sakata la Bandari lilipoibuka, mkataba wa baina Tanzania na Dubai, kuhusu Kampuni ya DP World ya Dubai, kuendesha na kuendeleza bandari za Tanzania, Rais Samia alisakamwa kuwa yeye ni Mzanzibari lakini ameuza bandari za Watanganyika.

Baadaye likaja suala la kuunda Tume ya Mipango. Rais Samia aliomba watu wapendekeze majina ya wale ambao inaonekana wanafaa. Aliomba hata wapinzani wapendekezwe, kama wana uwezo na mawazo mazuri.

Lissu, alipotakiwa kutoa maoni kuhusu ombi hilo la Rais Samia, alijibu “hiyo akili ni matope.” Ni kosa kubwa kuamini kwamba hilo jibu halikumuumiza Rais Samia.

Hakuna binadamu mwenye uvumilivu wa kudumu. Hata ajaliwe moyo wa subira kiasi gani, zipo nyakati atatetereka. Hivyo, tukubali kuwa Rais Samia katika mwaka 2023, alijikuta ndani ya majaribu ya kidemokrasia. Hotuba ya Septemba 11, 2023, ilidhihirika kuwa alichokozeka.

Kisha, Katiba, Rais Samia alitaka wananchi waelimishwe kwanza iliyopo kama sehemu ya mchakato wa kuelekea Katiba mpya. Ukiweka mambo mengi pamoja, utabaini kuwa kuna mambo matatu makuu yalimweka Rais Samia kwenye majaribu ya kidemokrasia mwaka 2023.

Mosi, mikutano ya hadhara. Pili, sakata la bandari, tatu ni Katiba. Bahati mbaya aliyonayo Rais Samia ipo kwenye hekima za Rais Mwinyi; demokrasia ni jini, huwezi kulirejesha kwenye chupa.