Prime
Wabunge CCM mtegoni

Muktasari:
- CCM imetoa ratiba ya uchukuaji na urejeshaji fomu za kugombea udiwani, ubunge na uwakilishi kuanzia Mei 1 hadi 15, 2025, kwa ajili ya uchaguzi mkuu wa Oktoba, hatua inayochukuliwa mapema kabla ya kuvunjwa kwa Bunge Juni 27, 2025
Dar es Salaam. Chama cha Mapinduzi (CCM) kimewatega wabunge wake, baada ya kutangaza mchakato wa kuchukua na kurudisha fomu za kuwania nafasi hiyo kabla ya kuvunjwa kwa Bunge Juni 27, 2025.
CCM imetangaza kufungua pazia la uchukuaji na urejeshaji fomu za ubunge, udiwani na nafasi zote za viti maalumu kuanzia Mei mosi hadi 15, 2025, huku ukomo wa wabunge walio madarakani ukiwa Juni 27.
Uamuzi huo wa CCM umefikiwa wakati ambao chama hicho kimefanya mabadiliko kuhusu mfumo wa kuwapata wagombea.
Mbali na hilo, sasa ni wagombea watatu pekee watakaopigiwa kura ya maoni, tofauti na awali ambapo hata wagombea 20 au 40 waliruhusiwa kushiriki moja kwa moja kwenye kura ya maoni.
Kwa utaratibu wa sasa, utafanyika mchujo ili kuwapata watatu kabla ya hatua nyingine kufuata.
Pia, kutakuwa na raundi mbili za vikao vya uteuzi, uchukuaji fomu ukianza kwa kila nafasi za ubunge na udiwani, ili kuteua majina matatu.
Kisha wagombea watatu waliopatikana kwa mchujo kabla ya kura ya maoni, watapigiwa kura kwa utaratibu wa vikao vingine vitakavyopangwa kwa kuzingatia kura ya maoni.
Kwa utaratibu huo, inaelezwa kuwa mlolongo mrefu ili kupata majina matatu yatakayopigiwa kura umelazimisha mchakato kuanza mapema ili kuendana na ratiba ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC).
Kwa mujibu wa wadau wa masuala ya siasa, ni mtego kwa watakaotaka kutetea nafasi zao, kwa kuwa wataingia kwenye kinyang'anyiro cha mchakato ndani ya CCM bila kuwa na kiinua mgongo ambacho kwa miaka mingine baadhi wamekuwa wakikitumia kwa shughuli za siasa.
Hii ni kwa sababu kiinua mgongo hutolewa baada ya Bunge kuvunjwa. Kwa ratiba ilivyo, Bunge litavunjwa Juni 27, 2025, na kama taratibu zitawahi basi kiinua mgongo kinaweza kutoka mapema Agosti. Wakati huo mchakato wa ndani wa CCM unaweza kuwa umemalizika.
Taarifa ya CCM
Katika taarifa iliyotolewa na Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Amos Makalla, uchukuaji na urejeshaji fomu za ubunge, ujumbe wa Baraza la Wawakilishi na udiwani utaanza Mei mosi hadi 15, 2025.
Kwa mujibu wa Makalla, wanaoutaka ubunge na ujumbe wa Baraza la Wawakilishi watachukua na kurudisha fomu kwa Katibu wa CCM wa wilaya husika.
Kwa nafasi za viti maalumu kupitia Umoja wa Wanawake (UWT), NGO, wafanyakazi, wasomi na wenye ulemavu, fomu zitachukuliwa na kurudishwa kwa Katibu wa UWT wa mkoa husika.
Taarifa inaeleza wanaotaka nafasi ya viti maalumu kupitia Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM), watachukua na kurudisha fomu kwa Katibu wa UVCCM wa mkoa husika.
“Watakaogombea nafasi za viti maalumu kupitia Jumuiya ya Wazazi, watachukua na kurudisha fomu kwa Katibu wa wazazi wa mkoa husika,” imeeleza taarifa.
Kwa wanaotaka udiwani wa kata au wadi, fomu watachukua na kurudisha kwa Katibu wa CCM wa kata au wadi husika, huku wanaogombea udiwani wa viti maalumu watachukua na kurudisha fomu kwa Katibu wa UWT wa wilaya husika.
Kwa nafasi ya urais, chama hicho kimeshawateua wagombea wake katika mkutano mkuu wa CCM uliofanyika kuanzia Januari 18 hadi 19, 2025. Rais Samia Suluhu Hassan aliteuliwa kupeperusha bendera ya chama hicho, huku Dk Emmanuel Nchimbi ambaye kwa sasa ni Katibu Mkuu wa CCM akiteuliwa kuwa mgombea mwenza. Rais Hussein Mwinyi naye alipitishwa kuwa mgombea urais upande wa Zanzibar.
Tafsiri mbili
Akizungumzia hatua hiyo ya CCM, mchambuzi wa masuala ya siasa, Dk Faraja Kristomus amesema kuna tafsiri mbili za kutangazwa mchakato huo kabla ya Bunge kuvunjwa.
Katika tafsiri ya kwanza, amesema inawezekana CCM imeona itangaze mapema ili kuwakata nguvu wabunge aliowaita wakorofi katika Bunge la Bajeti.
“Wabunge wengi watakuwa wa kuunga mkono kila hoja ya Serikali ili kuepuka tishio la kukatwa majina yao kwenye mchakato wa kura ya maoni endapo wataonyesha upinzani kwa bajeti ya Serikali," amesema.
Kwa tafsiri nyingine, amesema inawezekana uongozi wa juu wa chama hicho umeamua kukabiliana na kiwango kikubwa cha rushwa wakati wa uchaguzi na kukosekana usawa kwenye mchakato.
“Hili limekuwa likitokea miaka ya nyuma, mchakato ukishaanza baada ya kuvunjwa kwa Bunge na wabunge kupokea kiinua mgongo huwa na nguvu kubwa ya kifedha ili kurahisisha mchakato wa kisiasa, hivyo kupita kwenye kinyang'anyiro kwa madai ya rushwa,” amesema.
Iwapo mchakato wote utafanyika kabla ya kuvunjwa kwa Bunge, amesema utaweka usawa kwa sababu wote wanaokwenda kugombea watakuwa hawana fedha nyingi za kuwahonga wajumbe.
Hatua hiyo amesema inaweza pia kuwa imelenga kuwajua mapema watumishi wa umma na walio katika nafasi za uteuzi wenye nia ya kugombea ili nafasi zao zijazwe haraka.
“Chama kinawataka makada wao walioko kwenye nafasi za uteuzi wajulikane mapema ili nafasi zao zijazwe na wengine kuliko kusubiri hadi Juni wakati wa kuvunjwa kwa Bunge,” amesema.
Kwa kufanya hivyo, amesema itajulikana mapema kuhusu wakuu wa mikoa, wa wilaya na wakurugenzi wanaowania ubunge.
Suala la matumizi ya fedha limekuwa likikemewa na viongozi mbalimbali wa CCM, akiwemo Dk Nchimbi na Makamu Mwenyekiti wa CCM- Bara, Stephen Wasira ambaye alisema watakaobainika, hatua zitachukuliwa, kwani lengo ni kuhakikisha wanampata mgombea asiye na mawaa.
Ni mtego
Mwanazuoni wa historia katika Chuo Kikuu cha Bonne nchini Ujerumani, Philemon Mtoi amesema kilichofanyika ni mtego kwa wabunge walio madarakani.
Mtoi amesema mchakato wa kipindi hiki ni mgumu kwa walalahoi, akidai hawatamudu gharama za kampeni.
Kwa mtazamo wake, uamuzi wa CCM utapunguza malalamiko ya rushwa katika mchakato wa ndani wa uteuzi wa wagombea.
Hata hivyo, amesema: “Ubunge hapa kwetu ni fursa ya kutengeneza fedha zaidi, hivyo wenye nazo watatumia zaidi na ambao hawana na chao hakipo.”
Mtoi amesema uchaguzi ni mchakato wa kidemokrasia, hivyo wajumbe wengi kwenye jimbo wanaweza kushiriki kutokana na uamuzi huo.
Mhadhiri wa Sayansi ya Siasa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa Mohammed Bakari amesema kwa sababu mchakato wa kumpata mgombea urais na makamu wake umefanyika mapema, inaweza kuwa sababu ya kufanya hivyo kwa nafasi za ubunge na udiwani.
“Sababu nyingine kubwa ninayoiona ni vuguvugu la Chadema la No reforms, no election, hivyo hatua ya CCM kuanza mchakato mapema ni kuuthibitishia umma kwamba uchaguzi utakuwepo,” amesema.
Amesema athari kwa mchakato huo kuanza mapema ni kuwapa wasiwasi wabunge walio madarakani, wakitumia muda mwingi kuwaza kuhusu washindani wao wa kura ya maoni.
“Kujiamini kwao kutapungua kwa sababu wataona wameshaanza kuwa challenged (kupata upinzani) au kupata taarifa za nani na nani amechukua fomu,” amesema.
Amesema kipindi kati ya kuvunja Bunge na uchaguzi, wabunge hukosa utulivu, wakiwamo mawaziri na naibu mawaziri.
“Unakuta mawaziri na naibu mawaziri wengi ni wabunge, wanahaha kwenye michakato ya uteuzi kuwania ubunge. Kuna hekaheka kubwa na utendaji unashuka,” amesema.
Hata hivyo, amesema mchakato unapoanza mapema, wapigakura watawafahamu wagombea na kuwafuatilia ili kuwajua kwa undani.
Dk Richard Mbunda kwa upande wake amesema ingawa bado tarehe ya kura ya maoni haijatajwa, tafsiri ya hatua hiyo ya CCM ni kuwa mbunge aliye madarakani anaweza kuwa na nafasi ya kipekee ya kuwafikia wajumbe.