CCM, Zaeca kushirikiana kuwabana watoa rushwa kwenye mchakato wa uchaguzi

Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Dk Mohammed Said Dimwa akizungumza na Kamati za siasa za Mkoa wa Mjini kichama katika mwendelezo wa ziara ya sekretarieti ya kukagua uhai wa chama.
Muktasari:
- Kila jimbo kimeanza kuweka watu wa maadili wa chama hicho kwa kushirikiana na Mamlaka ya Kuzuia Rushwa na Uhujumu Uchumi (Zaeca).
Unguja. Chama Cha Mapinduzi (CCM), Zanzibar kimesema kimeandaa mkakati mkali wa kukabiliana na vitendo vya rushwa katika kipindi chote cha mchakato wa uchaguzi ndani ya chama.
Naibu Katibu Mkuu CCM Zanzibar, Dk Mohammed Said Dimwa ametoa kauli hiyo leo Aprili 13, 2025 alipokuwa akizungumza na kamati za siasa za mkoa wa mjini kichama ikiwa ni mwendelezo wa ziara ya kukagua uhai na kuelezea mabadiliko ya chama na namna ya kupata wagombea na kura za maoni.
Amesema, chama kimeanza kuweka watu wa Mamlaka ya Kuzuia Rushwa na Uhujumu Uchumi Zanzibar (Zaeca) na watu wa maadili katika kila jimbo kwa lengo la kuzuia rushwa, hivyo ni vyema wakijiepusha kwani hatua kali za kinidhamu zitachukuliwa.
"Mimi nina msimamo thabiti, Mungu amenijaalia ninachukia sana rushwa, kwani katika uchaguzi ni mbaya sana hivyo sio tu kutoa rushwa huko hata mtu asithubutu kuja kwangu katika mazingira ya aina hiyo,” amesema Dk Dimwa.
Ameeleza kwamba, atawashughulikia viongozi wote ambao sio waadilifu na wenye nia ya kula rushwa kwa lengo la kuwakandamiza watu wengine.
Dk Dimwa amesema lazima washirikiane kupinga rushwa katika chama ili kuwapata viongozi makini ambao watachagulia kwa haki bila ya upendeleo.
Naye Katibu wa Nec, Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM Zanzibar, Khamis Mbeto Khamis amesema kila mwana CCM anayehisi ana sifa za kugombea basi akagombee na sekreterieti haitamuonea mtu itatenda haki.
“Tunataka viongozi watakaokwenda kuwasaidia wananchi na chama kwa ujumla na katu hatutampendelea wala kumuonea mtu,” amesema.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Mjini, Hamid Said Mbwana amewataka wenye nia ya kuchukua fomu i muda ukifika wakachukue na kurudisha kwa salama, kutaratibu na kupunguza hodi kwa wajumbe.
"Tangu tarehe ya kuchukua fomu ilipotangazwa kumekuwa hapakaliki, hodi zimekuwa nyingi kwa wajumbe, naombeni mtulie wakati ukifika mtafanya hivyo,” amesema.
Chama hicho kimeshatangaza utaratibu wa kuchukua fomu kwa ngazi za ubunge, uwakilishi na udiwani kuanzia Mei mosi, 2025 hadi 15, kwa mwanachama yeyote mwenye sifa achukue fomu kuwania nafasi hizo.