‘Gen Z’ wanavyovaa viatu vya Raila kumshughulikia Rais Ruto Kenya

Generation Z (Kizazi Z) ni kundi rika lenye kuhusisha watu waliozaliwa kuanzia mwaka 1996 mpaka 2010. Mwenye umri mkubwa zaidi kutoka Generation Z ana miaka 28 na mdogo kabisa miaka yake ni 14. Wakati mwingine, Generation Z huitwa Zoomers.

2024 ni mwaka ambao waliozaliwa mwaka 2006 wanatimiza umri wa miaka 18. Ni sawa kusema walioliona jua mwaka wa 10 ndani ya Generation Z, mwaka huu wanahama daraja la utoto na kuingia utu uzima.  Inaleta tafsiri kuwa Generation Z ni kundi muhimu la kutazama katika kuijenga kesho ya taifa na dunia.

Tafsiri ni kwamba watu wengi wa makamo katika dunia ya sasa walizaliwa Karne ya 20. Na katika uzao wa Karne ya 20 kuna vizazi tofauti. Waliozaliwa kabla ya Vita Kuu ya Pili ya Dunia (Second World War) wanaishia, wengi ni wa baada ya Second World War.

Tanzania ilipata kuwa na marais watatu tu waliozaliwa baada ya Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia, lakini kabla ya Vita Kuu ya Pili ya Dunia. Ni Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere (Rais wa kwanza) mwaka 1922-1999, Rais wa Pili, Ali Hassan Mwinyi (mwaka 1925 - 2024) na aliyemfuatia, Benjamin Mkapa aliyezaliwa mwaka 1938 na kufariki dunia mwaka 2020.

Rais wa nne, Jakaya Kikwete (mwaka 1955 mpaka sasa) na wa tano, Dk John Magufuli aliyezaliwa mwaka 1958 na kufikwa mauti mwaka 2021, ni kizazi cha baada ya Second World War lakini waliozaliwa kabla ya mwaka 1960. Ni kizazi ambacho huitwa Baby Boomers. Kwamba ni kizazi cha wakati wa kasi kubwa ya uzazi, kufuatia utulivu wa baada ya misukosuko ya vita.

Rais Samia Suluhu Hassan alizaliwa Januari 1960. Watu waliozaliwa mwanzoni mwa miaka ya 1960 hadi mwanzoni mwa miaka ya 1980 huitwa Kizazi X (Generation X) au Gen X. Kwa Marekani, kundi hili huitwa Kizazi cha MTV (MTV Generation) kwa sababu kituo cha runinga cha MTV kilianza kazi mwaka 1981.

Kuna kizazi kinachofuata baada ya Gen X, hicho kinaitwa Millennial. Wahusika wa kizazi hiki ni wale ambao walizaliwa mwanzoni mwa miaka ya miaka ya 1980, lakini waliokuwa na chini ya umri wa miaka 11 mwaka 1993, kisha kutimiza umri wa utu uzima, yaani miaka 18 ndani ya Milenia ya tatu.

Hayo ndiyo makundi ya vizazi vya Karne ya 20. Kwa nyongeza ni kuwa Baby Boomers na Gen X ni watoto wa wazazi waliozaliwa Karne ya 19 mpaka muongo wa pili wa Karne ya 20, yaani baada ya Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia. Wakati Millennial ni watoto wa Baby Boomers, vilevile kuna Millennial ambao ni watoto wa Gen X.

Generation Z kwa asilimia kubwa ni watoto wa Gen X, vilevile kuna wachache kutoka Millennial na Baby Boomers. Hii inamaanisha kuwa Generation Z ni watoto wa makundi rika ya mwisho ya Karne ya 20. Vyovyote unavyoweza kutafsiri, Generation Z ni kundi rika lenye uelekeo wa kuongoza makundi mengine duniani kote, ndani ya miaka mitano ijayo.

Marekani, Generation Z inashika nafasi ya tatu kwa idadi ya watu, nyuma ya Millennial na Baby Boomers. Vivyo hivyo kwa UK. Hizo ni takwimu za mwaka 2023. World Economic Forum, walichapisha ripoti mwaka 2021, yenye kuonesha Millennial inaongoza, lakini tangu mwaka 2018, iliripoti ujio wa kasi wa Generation Z kuongoza kwa idadi ya watu kuliko makundi rika mengine.


Generation Z Kenya

Mei 9, 2024, Muswada wa Fedha 2024 Kenya, uliwasilishwa bungeni kwa mara ya kwanza. Muswada huo, pamoja na mambo mengine umebeba mapendekezo ya kuongeza kodi na ushuru. Hii inajumuisha asilimia 1.5 ya kodi ya kidigitali kwa majukwaa ya ndani yenye kutoa huduma kama ajira kwa njia ya intaneti, ukodishaji, uuzaji wa chakula na usafiri.

Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) kwa baiskeli za umeme, mabasi, nishati za solar na betri za lithium-ion, ni mambo ambayo yamejumuishwa kwenye muswada. Utambulisho wa asilimia 16 VAT kwenye ununuzi wa mikate, usafirishaji wa sukari, huduma za kifedha, miamala ya sarafu za kigeni na asilimia 2.5 ya kodi ya umiliki wa magari, ni masuala yaliyoibua utata mkubwa ndani ya muswada huo.

Muswada wa Fedha Kenya 2024 una kurasa tano. Vijana wa Kenya ambao wamejipambanua kuwa ni Generation Z, wameingia barabarani kuupinga, kwa hoja kwamba endapo utapitishwa kuwa sheria, utazidi kuyafanya maisha kuwa magumu.

Generation Z wanataka muswada huo ufutwe ndipo wasitishe maandamano. Wakati huohuo, Ikulu Kenya, imeshatoa taarifa ya kufutwa baadhi ya kodi zenye kuleta mgongano, mfano asilimia 16 ya VAT katika ununuzi wa mikate, vilevile kodi ya umiliki wa gari.

Taarifa ya Ikulu Kenya, ilibainisha kwamba mabadiliko mengine yaliyofanywa kwenye Muswada wa Fedha 2024 ni kuondoa kodi ya usafirishaji wa sukari, huduma za kifedha, miamala ya ubadilishaji fedha za kigeni, kuondolewa kwa ongezeko la ada ya utumaji wa fedha kwa njia ya siku na ushuru wa bidhaa kwenye mafuta ya mimea pia umeondolewa.

Kwa nini Generation Z?

Muswada wa Fedha Kenya 2024 umekuwa sababu. Mwangwi unaotoka nyuma ya maandamano ya Generation Z umekuwa ukigusa maeneo matano yenye kuigusa moja kwa moja jamii, hasa vijana. Namba moja ikiwa ni ugumu wa maisha. Gharama za maisha zipo juu, hivyo kuumiza vijana wengi.

Ukosefu wa ajira, vilevile vijana wengi kufanya kazi za kuungaunga (underemployment), ni sababu nyingine ambayo imesababisha mwamko wa vijana kuingia barabarani kupinga kuswada huo. Hili ni eneo ambalo linahitaji mkazo mkubwa.

Generation Z ni kundi rika lenye wasomi wengi vijana kuliko mengine yote. Asilimia kubwa ni wale ambao wamefika vyuo vikuu na kutunukiwa angalau shahada moja. Wanaondoka vyuoni wakiwa na matumaini makubwa ya kupata ajira, lakini mtaani wanakuta patupu.


Kwa kifupi, Generatio Z ni kundi lenye vijana wengi ambao wanajihisi hawana cha kupoteza. Wamesoma vizuri, maana mazingira ya ukuaji wao yana upendeleo mkubwa kielimu. Wamezaliwa na kukua katika nyakati za mapinduzi makubwa ya kiteknolojia na Tehama. Wanaijua dunia, wanazijua harakati, wanatambua haki zao, halafu hawana cha kupoteza.

Rushwa ni kipengele kingine kikubwa. Maisha ni magumu mtaani, ajira hamna, vipato ni vya kuungaunga. Vijana wa Generation Z wanaumizwa na habari za rushwa na kashfa za viongozi kujilimbikizia mali. Kisha, wanaona muswada wa fedha ambao unatoa ahadi ya kuyafanya maisha kuwa magumu zaidi.

Katika maandamano, kuna matamshi na matendo ya waandamanaji ambayo yanaashiria changamoto ya afya ya akili. Kuna kijana aliamua kutokomea na farasi wa polisi. Wakati unashangaa maneno na matendo, usiache kujenga tafakuri kuwa vita ya ajira na presha za kimaisha, huwa na matokeo yenye kuutikisa ubongo. Hilo huleta changamoto ya afya ya akili.

Viatu vya Raila

Rais wa Kenya, William Ruto, alizaliwa Desemba 21, 1966. Yeye ni Generation X. Waandamaji wa Generation Z ni rika la watoto wa Ruto. Ni sahihi kusema kuwa siasa zimebadilika, wanaomtesa Ruto ni watoto wake. Hao ndiyo wanamwita majina mabaya, likiwemo Zakayo (mtoza ushuru), ambalo na yeye mwenyewe analitambua.

Ruto, alikula kiapo kuiongoza Kenya Septemba 13, 2022. Bajeti ya kwanza kupitishwa na serikali yake mwaka 2023, ilikumbwa na misukosuko ya utekelezaji. Kiongozi wa upinzanj Kenya, Raila Odinga, alihamasisha maandamano yasiyo na kikomo kutaka Ruto ashushe gharama za maisha na aruhusu ukaguzi wa seva za Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC).

Maandamano hayo yaliyoitishwa na Raila, yaliipeleka puta Serikali ya Ruto. Ilimlazimu Ruto, ambaye awali alitangaza kutoketi na Raila wazungumze, kubadili msimamo na kufanya mazungumzo ambayo yalirejesha utulivu.

Februari 2024, Raila alianza mchakato wa kuwania uenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika (AUC). Misheni hiyo ya Raila inaungwa mkono na Ruto. Wengi wanaamini kuwa Ruto alikimbilia kumuunga mkono Raila kwenda Umoja wa Afrika, akiamini ingekuwa nafasi kwake kuongoza nchi kwa amani.

Kwamba, Kenya bila ushawishi wa Raila, isingekuwa na hekaheka za maandamano. Hata sasa, Raila akiwa amejielekeza kuwania kiti AU, amekuwa kimya, lakini bajeti ya pili ya Serikali ya Ruto inapitia moto mkali. Raila yupo kimya, ila maandamano yapo.

Raila alizaliwa Januari 7, 1945. Raila ni Baby Boomer. Kimpangilio, Generation Z ni wajukuu wa Baby Boomers. Hii ni sawa na kusema, Raila yupo kimya, lakini wajukuu zake wamevaa viatu vyake na wanakiamsha Kenya. Mateso ya urais kwa Ruto yapo palepale. Zaidi, Ruto ameshakubali kukutana na waandamanaji, Generation Z.


Mateso ya Ruto

Kikubwa kinachomtesa Ruto ni mguu alioingilia Ikulu Kenya. Alikuwa Naibu Rais, lakini akajitenga na changamoto za wakati wa uongozi wa Rais Uhuru Kenyatta, wakati yeye ndiye alikuwa msaidizi mkuu. Akahakikisha propaganda zinashika mpini. Akasema, hali ngumu ya maisha ya Wakenya ilisababishwa na mwafaka baina ya Uhuru na Raila.

Ruto alijenga ahadi kwa Wakenya bila uhalisia. Alisema, endapo angechaguliwa kuwa Rais wa Kenya, gharama za maisha zingeshuka na uchumi wa nchi ungejengwa kuanzia kwa watu wa chini kwenda juu. Baada ya kila tambo na propaganda anuwai, Ruto ndiye Rais sasa.

Wananchi wa Kenya hawaoni kile walichoahidiwa. Zaidi, wanaona maisha yamekuwa magumu kuliko nyakati za Uhuru. Si kwamba Ruto ndiye anasababisha maisha yawe magumu, bali mazingira ya nchi na mzunguko wa dunia. Hata hivyo, Wakenya hawana muda wa kumwelewa. Waliambiwa maisha yangekuwa nafuu na hayawi.

Ruto anateswa zaidi na mguu alioingilia. Ni ushuhuda jinsi karma inavyodai madeni yake. Inashabihiana na msemo "what comes around goes around", kama alivyoandika Eddie Stone, katika kitabu chake kinachoitwa "Donald Writes No More", ambacho ni chapisho la mwaka 1974.