Namna ‘Gen Z’ wanavyopambania mabadiliko nchini Kenya  

Baadhi ya waandamanaji wa kupinga muswada wa sheria ya bajeti mpya nchini Kenya. Picha na Mtandao

“Najivunia vijana wetu” ni kauli ya Rais wa Kenya, William Ruto kuhusu maandamano ya vijana, maarufu kama Gen Z ya kupinga Muswada wa Fedha wa 2024 ambao umeshapitishwa na Bunge.

Licha ya maandamano hayo, muswada huo umepitishwa kwa wabunge 204 waliopiga kura kuunga mkono, huku wengine 105 wakiupinga.

Rais Ruto akizungumza wakati wa ibada leo Jumapili Juni 23, 2024 katika Kanisa la Nyahururu, amesema Serikali imewasikia vijana na iko tayari kufanya mazungumzo nao.

Wakati Ruto akitoa kauli hiyo, Waziri Mkuu wa Kenya, Musalia Mudavadi ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Nje amesema; “Hao watu wanaokataa Muswada wa Sheria ya Fedha, kama utakataliwa na Serikali, kitu kingine watakachozungumza ni kupiga kura ya kutokuwa na imani, hivyo Serikali iondoke madarakani tufanye uchaguzi mpya. Usidhani kama ni utani, mpango wao ni kumng’oa Ruto, usichukulie kiwepesi.”

Pia, mwanasiasa Martha Karua amesema; “Gen-Z itamaliza mapambano ya ukombozi wa Kenya.”

Mbunge wa Kapsenet, Oscar Sud amesema;  “Sisi sote lazima tukubali na kujifunza kutoka kwa Gen-Z. Hawana ukabila na wameungana kwa jambo moja la kuwa na Kenya iliyo bora.

“Tunakoelekea lazima tuwe imara kuingiza mawazo yao kwenye muswada ujao wa sheria ya fedha na sera zinazowaumiza.”

Hata hivyo, Ruto amesema maandamano ya kupinga muswada wa sheria ya fedha yanayoongozwa na kizazi cha vijana wenye umri mdogo (Gen-Z) ni njia ya kuifanya Serikali yake kushirikiana nao kujenga nchi bora.

Gen-Z wamekuwa wakitumia mtandao wa TikTok kushiriki maandamano katika maeneo mengi ya nchi, tofauti na vijana wa nchi za Mashariki ya Kati Desemba 17, 2010, maarufu ‘Arab Spring’ waliotumia mtandao wa X zamani twitter kuwasiliana kufanya maandamano.

Maandamano ya Mashariki ya kati yalianzia nchini Tunisia baada ya kijana muuza matunda ‘machinga’, Mohamed Bouazizi kujitoa muhanga kwa kujichoma moto mbele ya ofisi za halmashauri, akilalamika kuchukuliwa bidhaa zake.

Ruto amepongeza mpango (maandamano) unaofanywa na vijana na kuyataja kuwa ni kauli yao ya kuhusika katika ulingo wa siasa. Amesifu kama wajibu wao wa kidemokrasia.

Aidha, mkuu huyo wa nchi amebainisha kuwa Serikali iko tayari kuwashirikisha vijana katika mazungumzo na kubaini mambo yanayowasumbua vijana.

“Napenda kuwapongeza vijana wetu kwa kujitokeza na kujali mambo ya Kenya, wamefanya wajibu wa kidemokrasia kusimama na kutambulika, tunakwenda kufanya mazungumzo na vijana, tunakwenda kuwashirikisha. Wamejitokeza na wametambuliwa.

“Ninajivunia sana vijana wetu. Wamesonga mbele, bila kabila na kwa amani,” amewongeza Ruto.

Amesema Serikali imetenga Sh10 bilioni kwa Hazina ya Maendeleo ya Maeneo Bunge (CDF) katika bajeti ya mwaka wa kifedha wa 2024/2025 ambazo zingetumiwa kuendeleza masilahi ya vijana.

Ruto amesema kuwa Serikali itakuwa ikitenga rasilimali zaidi kwa ajili ya CDF na kwa Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HELB).

Amesema ili kukabiliana na ukosefu wa ajira, Serikali imelenga katika uundaji wa Vituo vya TEHAMA, ili kutoa nafasi zaidi za kazi nchini.

“Vijana wetu wamejitokeza kufanya mambo ya nchi yao, wametimiza wajibu wa kidemokrasia kusimama na kutambulika, nataka niwaambie tunakwenda kufanya mazungumzo nanyi, ili tubaini masuala yenu, tunaweza kufanya kazi pamoja kama Taifa na kuboresha masuala yenu.

"Ninajivunia sana vijana wetu. Wamesonga mbele bila kabila, wamepiga hatua kwa amani na ninataka kuwaambia tutashiriki, ili kwa pamoja tujenge Taifa bora," amesema Ruto na kuongeza;

"Ninachotaka kuwatia moyo ni kwamba hatuna wasiwasi kuhusu masuala yao."

Ameongeza kuwa katika mwaka ujao wa fedha, wametenga fedha kwa ajili ya kutengeneza fursa za ajira kwa vijana na pia kuwawezesha kupata elimu ya chuo kikuu.


Msemaji wa Serikali

Wakati Ruto akisema hayo, Msemaji wa Serikali, Mwaura ameonya kuwa;

"Tunataka nchi yenye nguvu na hatuwezi kuivuruga nchi hii kama vile Libya na ‘Arab Spring’ nchini Misri. Tusiende upande huo kwa sababu hatuwezi kujihusisha. Ikiwa kweli tunataka kujihusisha, hebu tukae chini na tuzungumze."

Maandamano ya Gen-Z yalianza jijini Nairobi yakaendelea hadi Mombasa na maeneo mengine mbalimbali ya nchi yalijiunga na maandamano hayo yakiwemo Kisii, Kisumu, Nakuru, Nyeri na Nanyuki.


 Kinacholalamikiwa na Gen-Z

Gen-z ni vijana waliozaliwa baada ya 1997, pia wanajulikana kama kizazi cha "wazaliwa wa kidijitali" kwa sababu walizaliwa wakati wa mtandao. Gen ni generation na 'Z' inamaanisha "Zoomer", kwani hiki ndicho kizazi cha kwanza kinachojulikana 'kukuza' mtandao.

Kifungu cha 260 cha Katiba ya Kenya kinafafanua kijana kama mtu mwenye umri kati ya miaka kumi na minane (18) na miaka thelathini na nne (34).

Kenya ina vijana zaidi ya asilimia 80 ya watu wenye umri wa miaka 35 na chini. Ongezeko la vijana limekuwa jambo la kimataifa na Kenya nayo pia

kulingana na ripoti ya 2022 ya Ofisi ya Kitaifa ya Takwimu ya Kenya, kiwango cha ukosefu wa ajira miongoni mwa vijana wenye umri wa miaka 20-24 ni cha juu sana, kikiwa karibu asilimia  22.6. Kuchanganyikiwa huku kwa uchumi kumechochea ushiriki wa Gen-Z katika maandamano hayo.

Kwa mfano, maandamano ya nchi nzima dhidi ya muswada wa fedha wa 2024/2025 yalishuhudia kujitokeza kwa wingi kwa vijana.

Waliingia barabarani, wakiwa na mabango na hashtag, wakitaka utawala bora na mageuzi ya kiuchumi.

                                                                                                                                        

Kilichotokea Mashariki ya Kati

Maandamano katika nchi za Kiarabu yalichochewa na kujitoa mhanga kwa mfanyabishara mdogo ‘machinga’ Mohamed Bouazizi Desemba 17 2010 nchini Tunusia, yalisababisha kuondolewa madarakani kwa Rais wa nchi hiyo,  Ben Ali Januari 14,2011 aliyelazimika alipojiuzulu rasmi baada ya kukimbilia Saudi Arabia na hivyo kuhitimisha miaka 23 madarakani.


Misri

Nchini Misri maandamano ya vijana yalisababisha Rais Hosni Mubarak kuondoka madarakani baada ya miaka 30 ya utawala.


Yemen

Nchini Yemen, Rais Ali Abdullah Saleh alilazimika kuachia ngazi.


Bahrain

Maandamano makubwa ya kudai mageuzi ya kisiasa na kiuchumi yalizuka nchini Bahrain katikati ya Februari 2011, yakiongozwa na wanaharakati wa haki za binadamu wa Bahrain na wanachama wengi waliotengwa wa Kishia nchini Bahrain.

Maandamano yalizimwa vikali na vikosi vya usalama vya Bahrain, vikisaidiwa na kikosi cha usalama cha Baraza la Ushirikiano la Ghuba (kilichojumuisha takriban wanajeshi 1,000 kutoka Saudi Arabia na maofisa wa polisi 500 kutoka Umoja wa Falme za Kiarabu).

Baada ya maandamano hayo, viongozi wa waandamanaji walitiwa hatiani kwa kuipinga Serikali na kutiwa gerezani, mamia ya wafanyakazi wa Kishia walioshukiwa kuunga mkono maandamano hayo walifukuzwa kazi na misikiti ya Shi’i ikabomolewa na Serikali.


Libya

Nchini Libya, maandamano dhidi ya utawala wa Muammar al-Gaddafi yaliongezeka haraka na kuwa uasi wa kutumia silaha.

Wakati vikosi vya waasi vilipoonekana kukaribia kushindwa, Umoja wa Kujihami wa nchi za Magharibi (NATO) ulianzisha mashambulizi ya anga dhidi ya vikosi vya Qaddafi.Hata hivyo, Gaddafi baadaye aliuawa huko Sirte Oktoba 2011.


Syria

Nchini Syria yalifanyika maandamano ya kutaka Rais ajiuzulu. Hata hivyo ,kiongozi huyo hakuweza kung’olewa madarakani.


Nchi nyingine

Athari za vuguvugu la Arab Spring zilionekana kwingine kote Mashariki ya Kati na Afrika Kaskazini, huku nchi nyingi za eneo hilo zikikabiliwa na angalau maandamano madogo ya kuunga mkono demokrasia.

Nchi hizo ni Algeria, Jordan, Morocco na Oman ambazo watawala walitoa makubaliano mbalimbali, kuanzia kufukuzwa kazi kwa maofisa wasiopendwa na mabadiliko ya katiba, ili kukomesha kuenea kwa vuguvugu la maandamano katika nchi zao