Maandamano kupinga kodi mpya Kenya yashika kasi

Muktasari:

  • Balozi wa Tanzania nchini Kenya, Dk Bernard Kibesse ameiambia Mwananchi  Digital kuwa hakuna madhara yaliyoripotiwa kuwapata Watanzania waishio nchini humo.

Dar es Salaam. Maelfu ya waandamanaji wa Kikundi cha Gen-Z, wengi wao wakiwa vijana wameingia barabarani nchini Kenya kupinga ongezeko la kodi huku wakipuliza filimbi na kuimba nyimbo zinazoonyesha hasira wa dhidi ya Serikali.

Leo Alhamisi Juni 20 2024, wakati maandamano hayo yakiendelea nchini humo, Balozi wa Tanzania nchini Kenya, Dk Bernard Kibesse ameiambia Mwananchi  Digital kuwa hakuna madhara yaliyoripotiwa kuwapata Watanzania waishio nchini humo.

“Uzuri tahadhari ilitolewa mapema na watu waliamua kuzingatia hatua za kiusalama kwa kila mmoja wao. Watu walishauriwa wasiende maeneo yenye mchangamano hasa ya kibiashara au safari zisizo za msingi katika eneo hilo,” amesema Balozi Kibesse.

Mmoja wa Watanzania waishio nchini humo, Magreth Samson amesema hali ni mbaya mitaani kwa kuwa kuna makabiliano makali kati ya polisi na waandamanaji, hata hivyo amebainisha kuwa amejihifadhi sehemu salama.

Polisi katika mji mkuu wa Nairobi wamefyatua mabomu ya machozi na kurusha maji ya kuwasha dhidi ya makundi ya waandamanaji karibu na Bunge la nchi hiyo, lakini mbali na makabiliano hayo, kitendo chao cha kutaka kuzingira bungeni kilikuwa cha amani.

Maandamano hayo yalianza jijini Nairobi Jumanne Juni 18, 2024 kabla ya kuenea kote nchini Kenya leo.

Waandamanaji hao wamedai kutoridhika na sera za kiuchumi za Rais William Ruto katika nchi inayokabiliana na kupanda kwa gharama ya maisha.

Saa chache baada ya maandamano ya Jumanne yaliyoshuhudia mamia ya vijana wakikabiliana na polisi, Serikali ilikubali kufanya makubaliano na kupunguza nyongeza ya kodi kadhaa zilizowekwa kwenye muswada mpya wa fedha.

Hata hivyo, Serikali bado ina nia ya kuendelea na ongezeko la kodi na imetetea tozo zinazopendekezwa kama zinahitajika kwa ajili ya kujaza hazina yake na kupunguza utegemezi wa ukopaji kutoka nje.

Leo, maandamano yamefanyika kote Kenya huku maelfu wakikusanyika Nairobi, Mombasa, Nakuru na ngome ya upinzani ya Kisumu, kwa mujibu wa waandishi wa habari wa AFP na picha zilizoripotiwa kwenye televisheni.

Mapigano ya pekee yalizuka jijini Nairobi kati ya waandamanaji na polisi waliotumia mabomu ya machozi na maji ya kuwasha kwa waandamanaji waliokuwa wamekusanyika karibu na Bunge lililoanza kujadili muswada huo leo.

Licha ya kuwepo kwa polisi wengi na vizuizi vya barabarani vilivyowekwa pembeni ya barabara kadhaa zinazoelekea bungeni, mamia ya waandamanaji walikusanyika katika vikundi, wakipuliza filimbi na mavuvuzela, wakipeperusha mabango na kuimba: “Ruto lazima aende.”

Ivy, kijana anayetafuta ajira, mwenye umri wa miaka 26, aliiambia AFP kuwa alisukumwa kuandamana kwa mara ya kwanza kwa sababu, anahofia mustakabali wake.

“Muswada huu hauwezi kupita. Muswada huu utatumaliza. Hatuna ajira...hatuwezi hata kufungua biashara, hatuwezi kufanya lolote katika nchi hii,” amesema Ivy.

Mwandamanaji mwingine Bella, amesema alijitokeza kuhakikisha muswada wa fedha unakataliwa.

Mhitimu wa chuo kikuu mwenye umri wa miaka 22, aliiambia AFP kuwa hajafurahishwa na makubaliano ya Serikali mapema wiki hii.

Ofisi ya Rais, Jumanne iliyopita ilitangaza kuondolewa kwa tozo zilizopendekezwa za ununuzi wa mkate, umiliki wa gari pamoja na huduma za kifedha na simu, hivyo kutoa onyo kutoka kwa hazina ya upungufu wa Sh200 bilioni kutokana na kupunguzwa kwa bajeti.

Serikali sasa imelenga kwenye ongezeko la bei ya mafuta na kodi ya mauzo ya nje ili kujaza pengo lililoachwa na mabadiliko hayo, hatua ambayo wakosoaji wanasema itafanya maisha kuwa ghali.

“Wanajaribu tu kutudanganya, kodi ambazo wameondoa kwenye mkate wameongeza mahali pengine,” amesema Bella, akieleza  kuwa hiyo ni kama mbinu ya kuwafumba macho raia.

Chanzo kimoja kutoka bungeni kiliiambia AFP kuwa, kura ya kuamua kuhusu mapendekezo hayo inatarajiwa kupigwa Juni 27, siku tatu kabla ya tarehe ya mwisho ya kupitisha mswada huo.

Kodi hizo zilitarajiwa kuongeza kwa Ksh346.7 bilioni (Dola 2.7 bilioni za Marekani), sawa na asilimia 1.9 ya Pato la Taifa na kupunguza nakisi ya bajeti kutoka asilimia 5.7 hadi asilimia 3.3 ya Pato la Taifa.

Jumanne iliyopita maandamano ya Nairobi yalikuwa na waandamanaji waliovalia mavazi meusi wakikimbizana kama paka na panya na polisi waliofyatua mabomu ya machozi.

Takribani watu 335 wamekamatwa, kwa mujibu wa muungano wa makundi ya kushawishi, Tume ya Haki za Binadamu (KNCHR) na Amnesty Kenya.

“Tumebadilisha mbinu. Leo tutakuwa tumevaa mavazi ya rangi ili kuepuka kujirudia kwa wao kukamata kila mtu mwenye mavazi meusi,” amesema mratibu wa maandamano hayo ambaye aliomba hifadhi ya jina kutokana na kuhofia kuadhibiwa.

Kenya ni mojawapo ya nchi zenye uchumi unaoendelea katika Afrika Mashariki lakini theluthi moja ya watu wake milioni 51.5 wanaishi katika umaskini.

Kwa jumla, mfumuko wa bei umebaki kuwa juu kwa kiwango cha kila mwaka cha asilimia 5.1 kwa Mei, wakati mfumuko wa bei ya vyakula na mafuta ukiwa asilimia 6.2 na asilimia 7.8 mtawalia, kwa mujibu wa takwimu za Benki Kuu ya Kenya.