Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Serikali yaonya watakaohujumu vifaa vya chanjo, utambuzi wa mifugo

Muktasari:

  • Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Agnes Meena amesema hayo Julai 5, 2025 wakati akizungumza na wafugaji wakati wa uhamasishaji wa kampeni hiyo katika Halmshauri ya Wilaya ya Kilwa.

Wizara ya Mifugo na Uvuvi imetoa onyo kwa maofisa na watalaamu wanaotekeleza Kampeni ya Kitaifa ya Chanjo na Utambuzi wa Mifugo kutotumia vifaa vya chanjo kujinufaisha kibiashara na badala yake vitumike kuchanja mifugo kama ilivyokusudiwa na serikali.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Agnes Meena amesema hayo Julai 5, 2025 wakati akizungumza na wafugaji wakati wa uhamasishaji wa kampeni hiyo katika Halmshauri ya Wilaya ya Kilwa.

 Amesema Serikali imeachangia nusu ya gharama kwa chanjo ya mifugo kote nchini hivyo wataalamu wasitumie vifaa vya chanjo kwa manufaa yao wenyewe bali vitumike kama ilivyokusudiwa na Serikali na siyo kibiashara.

"Nipende kuwahimiza viongozi na Watalaam kuhakikisha kuwa hizo chanjo  tulizotoa, kila kitu kitumike kama ilivyopangwa, tusianze biashara, kuku wote watachanjwa bure lakini ng'ombe, mbuzi na kondoo mfugaji utachangia kidogo," amesema Meena.

Meena amesema kampeni hiyo baada ya kuzinduliwa na Rais Samia Suluhu Hassan mkoani Simiyu serikali kupitia wataalamu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi pamoja na halmashauri zimekuwa zikitekeleza kampeni hiyo na kuwahimiza viongozi na wataalam wa halmashauri zote nchini kuendeleza kampeni hiyo.

Aidha, Katibu Mkuu amesisitiza kuwa  sasa ni wakati mwafaka kwa wafugaji kulima malisho ya mifugo na kushirikiana katika uchimbaji wa mabwawa ya maji ya kunyweshea mifugo ili kuendana na ufugaji wa kisasa  na wenye tija.

Daktari wa Mifugo kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dk Daniel Mdetele amesema baada ya kutambua magonjwa yanayoathiri mifugo na mazao yake katika masoko ya kimataifa, wizara ilianisha magonjwa kumi na tatu ya kipaumbele na  kuchukua  hatua za kukabiliana nayo ikiwemo utoaji wa chanjo kwa mifugo yote nchini

"Baada ya kutathimini na kupata magonjwa 13 ya kipaumbele serikali imechukua hatua za kukabiliana na magonjwa hayo kwa  kuogesha mifugo yote kupitia majosho  yetu lakini pia kwa kutoa chanjo ambayo itaenda kutokomeza magonjwa yanayoathiri mifugo ikiwemo  homa ya mapafu kwa ng'ombe, sotoka ya mbuzi na kondoo na kwa upande wa kuku ugonjwa mdondoo," amesema Dk Mdetele.

Akisoma taarifa ya utekelezaji wa chanjo daktari wa mifugo wa  Wilaya ya Kilwa, Nyalekwa Mashimo alisema wilaya hiyo ilipokea  chanjo za mdodoo wa kuku 300,000 na hadi Juni 30 mwaka huu jumla ya kuku elfu thelathini zimechanjwa ikiwa ni sawa na asilimia 10 ya chanjo ya kuku iliyopokelewa.

Katika hatua nyingine, mfugaji Donald Mbuli wa Kijiji cha Matandu kilichopo katika halmashauri ya Kilwa amesema kwa sasa ana ng'ombe wasiopungua 800 hivyo ujio wa chanjo hiyo utamsaidia  kuikinga mifugo yake na magonjwa pamoja na kuongeza thamani ya biashara ya mifugo hiyo.