Sajuki kuzikwa kesho Kisutu, D’Salaam

Waombolezaji wakimfariji mke wa msanii maarufu nchini,Sadick Juma Kilowoko (Sajuki),Wastara (aliyefunikwa) jana nyumbani kwake Tabata Bima,Dar es salaam.Picha na Salhim Shao.
Muktasari:
“Sajuki licha ya kuwa msanii mwenzangu alikuwa pia kama ndugu yangu, kwani hata katika harusi yangu alisimamia yeye. Kifo chake kwa kweli kimenisikitisha sana, ameacha pengo kubwa kwetu sisi wasanii,” alisema Sweya.
TASNIA ya Filamu Tanzania imepata pigo jingine, baada ya msanii wake maarufu, Sadick Juma Kilowoko (Sajuki), kufariki dunia alfajiri ya kuamkia jana katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Dar es Salaam.
Kifo cha msanii huyo kimetokea takriban mwezi mmoja tangu msanii mwingine Sharo Milionea kufariki dunia kwa ajali ya gari na miezi 10 baada ya mwenzao mwingine, Steven Kanumba kuaga dunia ghafla.
Sajuki alifariki dunia siku moja baada ya kuhojiwa katika kipindi cha ‘Mkasi’ kilichorekodiwa na kurushwa na Kituo cha Televisheni cha EATV Jumatatu ya Desemba 31, mwaka jana.
Katika maelezo yake kwenye kipindi hicho ambacho hurekodiwa na kurushwa baada ya muda, Sajuki alieleza kuwa hajapona sawasawa na alikuwa anajiandaa kurudi tena India kwa matibabu zaidi..
Taarifa za kifo cha msanii huyo zilianza kusambaa katika mitandao ya kijamii (facebook), saa 11:00 alfajiri jana na muda mfupi baadaye, Msemaji wa hospitali hiyo, Jeza Waziri alithibitisha kutokea kwa kifo hicho.
“Ukweli ni kwamba Sajuki amefariki dunia. Sisi kama MNH tunasubiri ndugu wa marehemu kwa ajili ya taratibu za mazishi na kuwakabidhi mwili,” alisema.
Baba mzazi wa Sajuki, Juma Kilowoko alisema mazishi yatafanyika Ijumaa katika makaburi ya Kisutu, Dar es Salaam.
“Msiba upo Tabata Bima, lakini mazishi yatafanyika Ijumaa katika makaburi ya Kisutu baada ya taratibu nyingine kukamilika,” alisema. Akizungumzia kifo cha msanii mwenzake, Denis Sweya maarufu kwa jina la Dino alisema Sajuki ameacha pengo kubwa katika tasnia hiyo kwani alikuwa bado ni tegemeo.
“Sajuki licha ya kuwa msanii mwenzangu alikuwa pia kama ndugu yangu, kwani hata katika harusi yangu alisimamia yeye. Kifo chake kwa kweli kimenisikitisha sana, ameacha pengo kubwa kwetu sisi wasanii,” alisema Sweya.
Alisema siku tatu kabla ya kifo chake, alikuwa analalamika kukosa pumzi hivyo kupelekwa hospitalini kwa ajili ya matibabu.
“Lakini sisi wasanii wenzake tulikuwa na mipango ya kumpeleka Sajuki kwenda kupata matibabu nje na tulikuwa katika hatua za mwisho. Kitu kilichokuwa kinasumbua ni gesi kwani alikuwa anashindwa kupumua mwenyewe vizuri na kama unavyofahamu hali ya hewa ya kwenye ndege ingekuwa shida,” alisema.
Sweya alisema wakati wakiwa katika hatua za mwisho za kufanikisha jambo hilo, hali yake ilibadilika ghafla na akafariki dunia.
Alisema mbali na wasanii wenzake kujipanga kumsaidia Sajuki, Serikali pia imetoa mchango mkubwa katika matibabu yake, kwani alikuwa akitibiwa na madaktari wa Rais.
“Serikali imechangia kwa kiasi kikubwa na kwamba madaktari wa Rais walikuwa wapo karibu na Sajuki ili kuhakikisha anakuwa na afya njema, lakini mipango ya Mungu ndiyo hivyo, ametutoka.”
Ilivyokuwa Muhimbili
Mara baada ya kupatikana kwa taarifa za msiba huo, wasanii mbalimbali walifurika katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, huku wengi wakitokwa machozi.
Kundi kubwa la waandishi wa habari lilifika katika wodi aliyokuwa amelazwa marehemu Sajuki kushuhudia kabla ya mwili wake kupelekwa katika chumba cha kuhifadhia maiti. Rais wa Shirikisho la Filamu Tanzania (TAFF), Simon Mwakifwamba amesema wamepokea kwa masikitiko makubwa msiba wa Sajuki na kuwataka wasanii kuwa na ushirikiano katika kipindi hiki kigumu.
Akizungumza kwa niaba ya wasanii wenzake, Mwakifwamba alisema: “Tuko katika kipindi kigumu tunachotakiwa kufanya ni kushirikiana na familia ya marehemu.”