Vikombe viwili vya chai huongeza uwezekano wa kubeba ujauzito

Tunaambiwa chai ni kinywaji cha pili kikuu na mashuhuri duniani baada ya maji. Kinywaji hiki kina ladha za aina mbalimbali na mara nyingi hunyweka ikiwa ya moto, lakini wapo pia ambao huinywa ikiwa na uvuguvugu.
Licha ya kutumika zaidi kama kifungua kinywa, lakini je chai inamanufaa yoyote kwa afya ya binadamu?
Utafiti uliofanywa na Chuo Kikuu cha Marekani cha Boston unasema unywaji wa chai vikombe viwili kwa siku humuongezea mwanamke uwezekano wa kupata ujauzito.
Katika utafiti uliohusisha wanawake 3,600 umeonyesha wale wanaokunywa vikombe viwili vya chai kwa siku, wana asilimia 27 ya kupata ujauzito ikilinganishwa na wanawake ambao hawanywi chai.
Pia, utafiti huo umeonyesha wanawake wanaotumia vinywaji baridi vya aina mbili kwa siku, hupunguza uwezekano wao wa kushika mimba kwa asilimia 20 na haijalishi kama vinywaji hivyo vina sukari au la.
Mtafiti Mkuu, Profesa Elizabeth Hatch anasema alifanya utafiti huo ili kutaka kujua kama kuna uhusiano wowote wa kemikali aina ya caffeine inayopatikana kwenye chai, kahawa na uwezo wa kushika mimba kwa wanawake.
Utafiti huo uliofanywa kwa kuwahusisha wanawake wa kutoka Denmark kutokana na nchi hiyo kuwa na mfumo wa kuwapa namba za uraia wa kudumu raia wao wakati wa kuzaliwa, ulimpatia urahisi Profesa Hatch kuwafuatilia kwa njia ya tovuti ndani ya mwaka mmoja.
“Hatujui wanawake hawa walikuwa wakinywa chai ya aina gani, hatujui kama walikunywa chai bila kuongeza kitu kingine kwenye kinywaji hicho. Kama waliongeza maziwa au limao hatujui, bali inaonekana kuna uhusiano wa caffeine na uwezo wa kushika mimba au uwezo huo umetokana na mfumo wa maisha wa wanawake hao au ni kutokana na virutubisho vya chai hiyo,” anasema profesa huyo.
Pia, katika utafiti huo, wanawake waliambiwa waaandike kiwango cha chai ya kijani (green tea) au chai ya tiba (herbal tea) wanayokunywa kwa siku, lakini hakukuwa na uhusiano wowote ulionekana kati ya chai ya kijani wala chai ya tiba katika kuongeza uwezo wa kushika mimba kwa mwanamke.
Hata hivyo, baadhi ya watafiti wanasema chai imetengenezwa ili kukabiliana na maradhi ya aina zote, yakiwamo ya saratani na moyo.
Wanasema mara nyingi watu hufikiria chai husaidia pia kuzuia usingizi kwa sababu ina caffeine.
Ni kweli, kwa asili yake, majani ya chai yana caffeine, lakini wataalamu wa chakula na tiba lishe wanasema hutegemeana na uchakataji wake wa nyongeza hadi kuwa chai ya kijani ambayo huwa na kiwango kidogo cha caffeine au chai nyeusi ambayo huwa na kiasi kingi cha caffeine kinachokuwamo ndani yake.
Hivyo basi, chai zote isipokuwa zile zilizoondolewa caffeine zina kiwango fulani cha caffeine ndani yake. Kwa kulinganisha na kahawa, caffeine iliyomo kwenye chai ni ndogo. Kikombe kimoja cha chai kina takribani miligramu 40 za caffeine na kikombe kimoja cha kahawa nyeusi kina takribani miligramu 90.
Hata hivyo, Profesa Hatchi anasema utafiti zaidi unahitajika ili kujua kama chai ya kijani ndiyo husaidia wanawake kupata ujauzito au la.
Anasema ufuatiliaji zaidi utaweza kubaini pia hata ukubwa wa watoto wanaozaliwa na wanawake hao wanaokunywa chai vikombe viwili kwa siku.
“Pia kufahamu kama walibeba ujauzito huo kwa muda mrefu zaidi ya ule wa kawaida wa kujifungua au muda mfupi na kujifungua watoto njiti au hata kama mimba zao ziliharibika,” anasema profesa huyo.
Bingwa wa tiba za uzazi wa kituo cha Care Fertility Centre kilichopo Nottingham Jijini London, Uingereza, anasema; “Kuna virutubisho maalumu kwenye chai vinavyosaidia utungaji wa mimba. Chai huwa na kemikali nyingi aina ya anti-oxidants ambazo ni nzuri kwa uzazi kwa wanaume na wanawake, lakini nadhani kwa wanawake wanaohitaji mtoto ni vizuri kunywa chai kwa kiwango cha wastani.”
Naye Laurence Shaw, Mkurugenzi wa kituo cha uzazi cha Bridge Fertility Centre kilichopo London anasema, “Wanawake wenye miaka zaidi ya 35 wanaojaribu kushika mimba ni bora watafute ushauri kutoka kwa madaktari na si kunywa vikombe 10 vya chai eti kwa sababu wanataka mtoto.”
Ni bora tusubiri matokeo zaidi ya wanawake ambao wamepata ujauzito wakati wa utafiti huu ili tupate majibu ya uhakika kuhusu maendeleo yao baada ya kushika ujauzito.