UCHAMBUZI: Rais John Magufuli atangaze mshahara na marupurupu yake

Rais John Magufuli
Muktasari:
Wakati akizungumza na wazee wa Dar es Salaam, kwenye ukumbi wa Diamond Jubilee, Rais John Magufuli aliwaamuru mawaziri, naibu mawaziri, naibu spika na makatibu wakuu wachangie sh1 milioni kutoka kwenye mshahara wao wa mwezi. Pia, alieleza kuwa yeye mwenyewe, makamu wa rais na waziri mkuu watachangia Sh6 milioni kila mmoja ili zifike Sh100 milioni kusaidia changamoto za elimu bure Mkoa wa Dar es Salaam.
Rais Magufuli amejipambanua kuwa kiongozi anayeguswa na matatizo ya wanyonge, hapendi makuu, anahimiza ukusanyaji wa mapato ya Serikali na matumizi mazuri ya fedha za umma. Hata hivyo Watanzania hawajui mshahara wake ni kiasi gani?
Wakati akizungumza na wazee wa Dar es Salaam, kwenye ukumbi wa Diamond Jubilee, Rais John Magufuli aliwaamuru mawaziri, naibu mawaziri, naibu spika na makatibu wakuu wachangie sh1 milioni kutoka kwenye mshahara wao wa mwezi. Pia, alieleza kuwa yeye mwenyewe, makamu wa rais na waziri mkuu watachangia Sh6 milioni kila mmoja ili zifike Sh100 milioni kusaidia changamoto za elimu bure Mkoa wa Dar es Salaam.
Ikiwa Sh6 milioni zitakatwa katika mshahara wake wa mwezi mmoja ni wazi mshahara wake na ule wa makamu wake na waziri mkuu ni zaidi ya sh6 milioni kwa mwezi.
Mishahara na marupurupu ya viongozi wa Tanzania haipo wazi. Watanzania hawajui kila mwezi rais, makamu wa rais na viongozi wakuu wa Serikali wanalipwa kiasi gani? Malipo ya wabunge pia, hayako wazi? Inasemekana mshahara wa mbunge katika Bunge lililopita ulikuwa Sh3.4 milioni kila mwezi. Pia, mbunge alilipwa Sh8.2 milioni nyingine kama posho ya jimbo, gharama za ofisi, mafuta na malipo ya wasaidizi wake na dereva.
Anapohudhuria kikao cha Bunge alilipwa posho ya Sh80,000 za kujikimu, Sh50,000 mafuta ya gari naSh200,000 za kuhudhuria kikao cha Bunge jumla Sh330,000 kwa siku. Posho ya siku moja ya Mbunge ni zaidi ya mara mbili ya kima cha chini cha mshahara wa Serikali kwa mwezi mzima ambacho ni Sh150,000. Mishahara inakatwa kodi, marupurupu hayakatwi kodi.
Mwaka 2013, Zitto Kabwe wakati huo akiwa Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) katika mkutano wa kujenga chama chake uliofanyika Igunga alieleza kuwa Rais analipwa Sh384 milioni kwa mwaka sawa na Sh32 milioni kwa mwezi. Malipo haya hayakatwi kodi yoyote. Waziri Mkuu analipwa mshahara na marupurupu yanayofikia Sh26 milioni kwa mwezi. Gharama za chakula, nyumba ya kuishi na usafiri wa viongozi wakuu zinalipwa na Serikali.
Gazeti la Mwananchi la Julai 27 2015, lilitoa taarifa iliyoandikwa katika mtandao wa African Review kuwa Rais Kikwete ni wa nne miongoni mwa marais wa Afrika kwa kupata mshahara mkubwa. Taarifa hiyo ilieleza kuwa Rais Jakaya kikwete analipwa dola za Marekani 192,000 kwa mwaka sawa na dola 16,000 kwa mwezi.
Kwa kukadiria thamani ya dola moja ni Sh2,000, mshahara na marupurupu ya kila mwezi ni sawa na sh 32milioni kama alivyoeleza Zitto mwaka 2013.
Taarifa ya Ikulu ilikanusha vikali habari zilizochapishwa katika gazeti la Mwananchi. Ikulu ilieleza kuwa “Habari hizi siyo za kweli. Ni uongo na uzandiki. Ni uzushi mtupu na ni uzushi wa hatari...”
Mshahara wa Rais wa Tanzania kwa mwezi ni wa chini kiasi cha kwamba unazidiwa, tena kwa mbali, na mishahara wanayolipwa baadhi ya watendaji wakuu wa baadhi ya taasisi za umma nchini.” Hata hivyo, Ikulu haikueleza mshahara wa Rais na marupurupu yake ni kiasi gani?
Katika mjadala wa mshahara wa Rais, Naibu Spika wa Bunge lililopita ambaye ndiye Spika wa sasa alinukuliwa akieleza kuwa mshahara wa mtu ni siri yake. Waziri wa Nchi Katika Ofisi ya Rais, Menejimenti ya utumishi wa Umma wa wakati huo alisema kuwa ni kosa kutangaza mshahara wa Rais.
Kifungu cha 43 (1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano inaeleza kuwa “Rais atalipwa mshahara na malipo mengineyo, na atakapostaafu atapokea malipo ya uzeeni, kiinua mgongo au posho, kadri itakavyoamriwa na Bunge, na mshahara na malipo hayo mengineyo, malipo ya uzeeni na kiinua mgongo hicho vyote vitatokana na Mfuko Mkuu wa Hazina ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano na vitatolewa kwa mujibu wa masharti ya ibara hii.” Hata hivyo, wabunge wengi hawajui mshahara na marupurupu ya Rais.
Rais Magufuli amejivisha joho la kuwa Rais wa wanyonge. Anawajibika kuwaeleza Watanzania mshahara na marupurupu yake. Ikiwa mshahara ni mkubwa achukue hatua za kuupunguza kama alivyofanya Mwalimu Nyerere mwaka 1965.
Hata hivyo, kifungu cha Katiba cha 43 (2) kinaeleza “Mshahara na malipo mengineyo yote ya Rais havitapunguzwa wakati Rais atakapokuwa bado ameshika madaraka yake kwa mujibu wa masharti ya Katiba hii.” Katiba hii kweli haifai kabisa. Rais Magufuli akitaka kupunguza mshahara wake itabidi kwanza abadilishe kifungu hiki cha katiba. Anaweza kujitolee mchango wa kudumu utakaokatwa toka mshahara wake kusaidia sekta ya afya au elimu.
Ili kuimarisha utawala bora ni muhimu uongozi ulio madarakani utumie mamlaka waliopewa kwa manufaa ya taifa. Mishahara na marupurupu ya viongozi yawe wazi na yaamuliwe na kupangwa na taasisi iliyo huru. Kuweka utaratibu ulio wazi wa kuamua mishahara na marupurupu ya viongozi wa umma wakiwamo Rais na Makamu wake, mawaziri, wabunge, majaji, makatibu wakuu ni muhimu katika ujenzi wa utawala bora, uwajibikaji na uwazi wa viongozi wa umma kwa wananchi wanao waongoza.
Utaratibu wa kupanga na kulipa mishahara ya viongozi wa umma unaonyesha maadili ya jamii kuhusu uwepo wa utawala bora. Utawala bora unahitaji muhusika asifanye maamuzi yenye masilahi kwake binafsi. Rais asijipangie mshahara na marupurupu yake. Wabunge wasijipangie mishahara na marurupu yao. Tume huru ya Mishahara na marupurupu ya Viongozi ndiyo iwe na jukumu la kuchambua na kupanga mishahara na marupurupu ya viongozi.
Rasimu ya Katiba
Rasimu ya Katiba ya Jaji Warioba ilipendekeza kwenye kifungu cha 85 kuwa “Rais atalipwa mshahara na malipo mengineyo kama yatakavyoainishwa na Tume ya Utumishi wa Umma na atakapostaafu atapokea malipo ya uzeeni na stahili nyingine kutoka Mfuko Mkuu wa Hazina ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano.”
Katiba inayopendekezwa imetupilia mbali pendekezo la Tume ya Jaji Warioba na wamerejesha utaratibu uliopo katika katiba ya zamani.
Pendekezo la Rasimu ya Katiba ni afadhali kuliko hali ilivyo sasa. Hata hivyo, Tume ya Utumishi inafanya kazi chini ya Rais na haitakuwa na uhuru wa kutosha kupanga mshahara wa Rais bila woga na kuzingatia hali halisi ya Tanzania na wastani wa kipato cha wananchi wake.
Ni vyema Katiba ikatamka wazi kuwapo kwa tume huru ya mishahara na marurupu ya viongozi. Katiba ya Kenya ina Tume ya Mishahara na Marupurupu (The Salaries and Remuneration Commission) ambayo kazi yake ni kupanga mishahara na marupurupu ya kada na viongozi wa juu.
Kwa sasa Rais Magufuli atangaze mashahara na marupurupu yake na kama mapato yake ni Sh32 milioni kwa mwezi, basi ajitolee alau nusu ya mapato hayo kuchangia elimu na afya ya wanyonge. Hatua hii itaimarisha taswira inayojengeka barani Afrika kuwa yeye ni Rais wa wanyonge.
Mwandishi ni mchambuzi wa masuala ya uchumi na siasa. [email protected]