Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

‘Vifaa vya maabara Shule ya Longido Samia vifungwe’

Muktasari:

  • Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko amesema lengo la Serikali ni kuzalisha wanasayansi na siyo wachoraji wa 'burnsen burner'.

Longido. Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko ameagiza kufungwa kwa vifaa vya maabara ya kemia na baiolojia katika Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Longido Samia ili wanafunzi waanze mafunzo kwa vitendo, sambamba na lengo la Serikali la kuimarisha elimu kwa kujenga maabara na kukuza uzalishaji wa wanasayansi.

Dk Biteko ametoa agizo hilo leo, Alhamisi Aprili 24, 2025, katika siku yake ya pili ya ziara yake  mkoani Arusha kuelekea maadhimisho ya miaka 61 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.

Shule hiyo, iliyojengwa kwa zaidi ya Sh4.4 bilioni, tayari imepokea baadhi ya vifaa vya maabara wiki mbili zilizopita, lakini havijafungwa kutokana na kutokamilika kwa ufungaji wa makabati.

Amesisitiza kuwa Serikali imewekeza katika elimu, hasa kwa watoto wa kike, kwa kujenga miundombinu ya kisasa kama vile maabara, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kuzalisha wataalamu wa sayansi nchini.

Hivyo, amewataka viongozi wa Mkoa wa Arusha, akiwemo Mkuu wa Mkoa, Paul Makonda kufuatilia kwa karibu kuhakikisha vifaa hivyo vinafungwa na maabara zinaanza kutumika mara moja.

Ameonya kuwa haitakiwi wanafunzi kuendelea kuchora vifaa vya maabara kama vile 'Bunsen burner' badala ya kuvitumia kwa vitendo, huku akisema hayo ni mambo ya zamani.

“Maabara zimejengwa vizuri lakini hazijaanza kutumika. Nimemuelekeza Mkuu wa Mkoa na Mkurugenzi wa Halmashauri kufuatilia jambo hili kwa karibu. Vifaa vimenunuliwa, hatutaki viwepo tu stoo watoto waanze kujifunza kwa vitendo sasa hivi,” amesema Dk Biteko.

Aidha, kufuatia ombi la Mkuu wa shule hiyo, Dk Biteko ameagiza mchakato wa kufunga mfumo wa nishati safi ya kupikia ukamilike ndani ya wiki moja, kwa gharama ya Sh17 milioni.

Awali, Mkuu wa Shule hiyo, Ester Kobelo alimweleza Dk Biteko   kwamba, shule ina wanafunzi 310, wakiwemo 120 wa kidato cha kwanza na 190 wa kidato cha tano na ujenzi wa awamu ya pili, ikiwemo bwalo na maabara ya fizikia, unatarajiwa kukamilika Mei 30, 2025.

Amesema miongoni mwa changamoto kubwa ni ukosefu wa nishati safi ya kupikia na uhaba wa samani kwa ajili ya bwalo la chakula. Aliiomba Serikali kusaidia kutatua changamoto hizo.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda amewahimiza wanafunzi wa shule hiyo kusoma kwa bidii na kuwaheshimu wazazi wao, huku akisisitiza kuwa shule hiyo iwe mfano wa kuigwa katika elimu mkoani humo.

Akizungumza kwa niaba ya wanafunzi wenzake, Doreen Deogratias ameshukuru Serikali kwa kujenga shule ya kisasa yenye mabweni na kueleza kuwa wanafunzi wanathamini fursa hiyo.