Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

INATIA HURUMA: Kada CCM aliyemwagiwa tindikali afanyiwa upasuaji wa macho

Moshi. Kada wa Chama cha Mapinduzi (CCM), mkoa wa Kilimanjaro, Idrisa Moses maarufu ‘Makishe’ aliyemwagiwa kimiminika kinachodaiwa ni tindikali, amefanyiwa upasuaji wa macho yote mawili na moja limeonyesha dalili ya kuona vizuri.

Akizungumza kwa simu na Mwananchi leo Alahamisi Aprili 24, 2025 kutoka hospitali alikolazwa na kufanyiwa upasuaji huo, kada huyo amesema madaktari bingwa wa macho wamemweleza kuwa Jicho moja ndio litaona vizuri kama lilivyokuwa mwanzo.


“Kwa kweli nawashukuru sana madaktari bingwa hapa nilipolazwa. Wamenifanyia oparesheni ya macho yote mawili, moja ndio liko active (liko vizuri). Hili lingine halina mategemeo ni la kutoa na kuweka lingine,” amesema kada huyo wa CCM.

“Baada ya siku 90 nitarudi tena hapa hospitali ili kuli shape (kuliweka vizuri) hili linaloona vizuri ila hili moja madaktari wanasema asilimia 80 ni kutoa na kuweka lingine. Mdomo inabidi nisubiri miezi 12 ipite tangu ndio warekebishe.”

“Kwa kweli namshukuru Mungu hili Jicho moja baada ya upasuaji uliofanyika sasa linarudi kama ilivyokuwa kabla ya kumwagiwa tindikali. Nawashukuru wadau wote walionipambania na wanaoendelea kunipambania. Mungu atawalipa,”ameeleza.

Kada huyo ambaye hakutaka kuweka wazi hospitali ambayo upasuaji huo umefanyika Aprili 14,2025, ameziomba mamlaka za uchunguzi kuvaa viatu vyake kutokana na hali aliyonayo na kufanya uchunguzi utakaosaidia kuwanasa waliohusika.

Ingawa hadi sasa hakuna mtu anayehusishwa moja kwa moja na tukio hilo, lakini minong’ono iliyopo Jimbo la Moshi mjini ni kuwa tukio hilo linahushwa na vita ya kuusaka ubunge wa Jimbo hilo katika uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba 2025.


Aisubiri kwa hamu THBUB

Akizungumzia taarifa kuwa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB), imeahidi kuchunguza tukio hilo ambalo limeacha maswali mengi mjini Moshi, kada huyo amesema amepokea kwa furaha na kwa matumaini kauli ya THBUB.

Machi 5,2025, Makishe aliiandikia Tume hiyo akiiomba itumie mamlaka yake ya Kikatiba kuchunguza tukio hilo na kuondoa wingu zito lililogubika na kueleza kuwa ana imani Tume hiyo itapata jambo la kuuambia umma ni nani wanaohusika.

Mwenyekiti wa THBUB, Jaji mstaafu Mathew Mwaimu alipoulizwa na Mwananchi alijibu kwa kifupi:-

"Tumeipokea (barua) na hatua za awali tumeona ni suala ambalo linatupasa kufuatilia na kulifanyia uchunguzi. Nimeshatoa maelekezo."

Katika barua hiyo, kada huyo amedai kwa jinsi sura yake ilivyoharibika, hata watoto wake wadogo, mmoja anayesoma shule ya awali  na mwingine anayesoma darasa la kwanza wanaogopa kumsogelea isipokuwa kama amevaa miwani.

“Ninakuandikia (mwenyekiti) barua hii nikitambua majukumu iliyonayo Tume kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 Ibara ya 130,” ameeleza kada huyo katika barua hiyo ambayo THBUB imekiri kuipokea.

Ibara hiyo imeainisha majukumu ya Tume kuwa ni pamoja na (b), kufanya shughuli za kupokea malalamiko ya uvunjaji wa haki za binadamu kwa jumla.

Lakini ibara ndogo ya (c), Tume itafanya uchunguzi juu ya mambo yanayohusu uvunjaji wa haki za binadamu na ukiukwaji wa misingi ya utawala bora.

“Ni kutokana na majukumu hayo mazito ya Kikatiba, ninakuandikia barua hii ili Tume yako ifanye uchunguzi huru wa tukio langu la kumwagiwa tindikali,” aliandika kwenye barua hiyo.

Makishe amesema anatambua Ibara ya 130 ya Katiba haizuii Tume kufanya uchunguzi wowote hata kama jambo linachunguzwa na chombo kingine na kusema yapo matukio ilishayachunguza licha ya kuwa polisi nao walichunguza.

Mifano ni kifo cha mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), Nusura Abdalah ambaye kifo chake kilizua utata lakini kwa sasa THBUB inachunguza matukio ya kupotea na kutekwa kwa watu nchini, ambayo polisi nao wanachunguza.

Makishe katika barua hiyo, alisema amesukumwa kuiomba tume kuchunguza kutokana na uzito na mazingira ya tukio lenyewe ili tume ifanye uchunguzi huru wa kufahamu nini kilitokea, nani walifanya hivyo na sababu za kufanya hivyo.

“Dalili za awali zinadai uwepo wa genge la wenye nguvu kifedha. Ninasema hivyo kwa sababu kushambuliwa kwangu kulikuja saa chache toka kutokee majibishano katika group la Whatsapp ambalo nilipata vitisho,” amedai.

“Ni nadharia inayotumika katika jinai (criminology) kwamba kama kuna mtu anapata matatizo, iwe kifo au kuumizwa vibaya kama ilivyonitokea, mshukiwa au washukiwa wa kwanza wanakuwa wale waliotoa vitisho dhidi ya mtu huyo.

“Dalili za nani wanaweza kuwa walisuka, kufadhili na kutekeleza uhalifu huu ziko wazi na niko tayari kuwaeleza wachunguzi utakaowatuma, ili kuonyesha kuwa harakati za kuwania ubunge 2025 ndio kiini cha mimi kumwagiwa tindikali.


“Nitafurahi sana kukutana na makamishina wa Tume hii ambayo nina imani kubwa nayo kwa sababu inaongozwa na Jaji,”alisema Makishe alipozungumza na Mwananchi leo Aprili 24, alipokuwa anaelezea kuhusu upasuaji wa macho yake yote mawili.


Tukio lilivyotokea

Baada ya tukio hilo kutokea, Septemba 2024 na video za kada huyo akipatiwa huduma ya kwanza katika mitandao ya kijamii, Kamanda wa Polisi mkoa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa alitoa taarifa kuwa Polisi wameanzisha uchunguzi.

Kamanda Maigwa alinukuliwa akiwaambia wanahabari kuwa siku ya tukio, Makishe ambaye ni dereva bodaboda akiendesha pikipiki yake aina Sinorai namba MC 854 DCB alikodishwa na mtu asiyemjua saa 2:00 usiku kutoka kijiweni kwake.

Mtu huyo alimtaka ampeleke eneo la Njoro katika Manispaa ya Moshi.

Kwa mujibu wa RPC Maigwa, baada ya kufika hilo, abiria aliyembeba alimwambia asimame ili amchukue mwenzake ndipo alipojitokeza kijana mwingine ambaye alimwagia kimiminika hicho usoni na kumpora pikipiki yake hiyo aina ya Sinorai.

Baadaye pikipiki hiyo ilipatikana imetelekezwa na watu hao katika msitu wa Njoro ambao hauko mbali na eneo la tukio na Desemba 2024, polisi walimrudishia Makishe simu yake na pikipiki hiyo wakati wakiendelea na uchunguzi.