Twanga Pepeta: Miaka 20 ya uhai wake ikikuza vipaji, kuibua vipya

Mkurugenzi wa Kampuni ya African Stars Entertainment (Asset), Asha Baraka.
Muktasari:
Makundi au bendi za muziki wa dansi ni miongoni mwa mambo yaliyoteka hisia za mashabiki wa burudani nchini tangu uhuru.
Kuzaliwa na kufa siyo tukio linalojitokeza katika maisha ya binadamu pekee bali hata kwa makundi mbalimbali ya kijamii hata burudani.
Makundi au bendi za muziki wa dansi ni miongoni mwa mambo yaliyoteka hisia za mashabiki wa burudani nchini tangu uhuru.
Lakini ukizungumzia muziki huo kihistoria tangu miaka ya 1990 huwezi kuiacha Bendi ya African Stars maarufu Twanga Pepeta.
Bendi hiyo kwa sasa imekuwa ni miongoni mwa bendi kongwe huku ikikutana na changamoto mbalimbali huku ikiwa pia chanzo au ‘mzazi’ wa bendi mbalimbali zilizopo kwenye ulimwengu huo kwa sasa.
Ni miaka 20 imekatika tangu kundi hilo lilipoasisiwa chini ya Kampuni ya African Stars Entertainment (Asset) inayoongozwa na Mkurugenzi wa wake, Asha Baraka.
Katika mahojiano maalumu na Starehe, Asha anaeleza mambo mbalimbali waliyokutana nayo ndani ya miaka 20 ya bendi hiyo.
“Tumekuwa sehemu ya mafanikio kwa bendi nyingi tu, tumeendelea kuwa bora kwa sababu ya kuwa na mtaji wa vipaji vingi vyanamuziki, lakini kwa sasa hatuoni mambo yakisonga mbele katika muziki huo ila tunajaribu kutumia uzoefu tu,” anabainisha Asha.
Ilivyozalisha mafanikio ya wengine
Asha anasema kuwa bendi mbalimbali zimepata mafanikio na majina katika muziki wa dansi kwa mgongo wa Twanga Pepeta.
Anaongeza kuwa Bendi ya Twanga ndiyo mlezi wa waimbaji wakongwe na mashuhuri wa muziki huo nchini wanaotamba kwa sasa.
Anawataja baadhi ya wasanii waliotokea bendi hiyo na kuanzisha nyingine ni pamoja na Banza Stone, Ali Choki, Nyoshi Elisadaat, Msafiri Diofu, Mwinjuma Muumini, Chalz Baba, Khalid Chokoraa,Aldoph Mbinga na Fergason.
“Mwaka 2001, Banza alikwenda kujiunga na Bendi ya TOT Plus na alikuwa msanii muhimu sana kwenye bendi. Lakini kuondoka kwake ikawa nafasi ya kung’aa kwa Ali Choki,” anasema na kuongeza:
“Mwaka huo huo, Aldoph Mbinga akaondoka kwenda kuanzisha Bendi ya Mchinga sound, akiwa ameacha wimbo wa ‘Jirani’ , Fainali uzeeni’ ziliofanya vizuri sokoni.”
Asha anaeleza kuwa miaka mitatu baadaye(mwaka 2004), Ali Choki akapata nafasi ya kuwa mwimbaji muhimu ndani ya Bendi.Hata hivyo, akaondoka pia, kwenda kuanzisha bendi yake (Extra Bongo).
Asha anasema kuwa baada ya kuondoka Choki, Banza alirejea Twanga Pepeta na kutoka na wimbo wa mashairi ya ‘Mtu pesa’.
“Wimbo uliofanya vizuri sana kwenye soko la dansi,” anasema.
Pamoja na kurudi kwa Banza, Asha anasema Twanga ilikuwa na hazina ya kutosha katika vipaji vilivyokuwa havionekani.
Anasema hali hiyo ilitoa nafasi pia ya kuonekana vizuri kwa kipaji cha Msafiri Diofu kupitia uandaaji wa mashairi ya wimbo mpya wa ‘Safari 2005’.
“Diofu na Banza wakapelekwa kuanzisha bendi mpya ya Chipolo Polo iliyokuwa chini ya Kampuni ya Asset,lakini haikufanya vizuri sana, ikapotea na Diofu akarudi Twanga 2009 na kutoa wimbo wa ‘Mwana Dar es Salaam’.
Anasema kuwa kabla ya kipindi hicho, waimbaji wengine kama Super Nyamwela, Chalz Baba, Chokoraa na Kalala walikuwa wameshaanza kupata nafasi ya kung’aa vipaji vyao mwanzoni mwa mwaka 2007/08.
“Waimbaji hao wakaamua kuanza kuangalia maslahi makubwa zaidi nje ya Bendi.Ndiyo wakajitoa na kuanzisha Mapacha watatu kabla ya Chalz Baba kuimalisha bendi ya Mashujaa kwa mwaka 2010,” anasema Asha na kuongeza:
“Kwa hivyo utaona kipindi cha kuanzia mwaka 2001 mpaka 2010 tayari kuna bendi tano zimezaliwa kutokana na vipaji vya Twanga, kila bendi inayojiandaa kutoka lazima iangalie vipaji kutoka Twanga.”
Asha anasema waimbaji hao walikuwa na nafasi ya kuondoka na kurejea kwenye bendi hiyo. “Lakini wamefanikisha kutengeneza albamu 13, albamu ya mwisho iliandaliwa na Kalala Junior kupitia wimbo wa ‘Nyumbani ni Nyumbani’. Anasema kuwa kuondoka na kurudi hutokana na mikataba kati ya bendi na mwanamuziki na kwamba wapo baadhi waliokuwa wakibanwa na mikataba, pia wasiobanwa na mikatana yao.
Vipaji vilivyobakia Twanga
Pamoja na kuwapo kwa wimbi hilo, Asha bado anajivunia nafasi ya kuwa na vipaji vingine vipya akisema vitaendelea kuisimamisha Bendi ya Twanga.
“Ni miaka 20 sasa imepita lakini Twanga bado imesimama, wanaondoka, lakini wapo wanaoibuka. Hakuna aliyefahamu kama kuna kipaji cha Ali Choki baada ya kuondoka Banza,” anasema na kuongeza:
“Waimbaji tulionao sasa ni pamoja na Khaji Ramadhani wa BSS na Jumanne Saidi maarufu ‘J4’. Hakuna aliyejua kama kuna Chalz Baba, Chokoraa walioibuka na kung’ara.”
Sababu za Twanga kutozalisha
Asha anashindwa kuzuia hisia zake akisema zipo sababu mbalimbali ambazo zimesababisha Twanga ishindwe kupanuka zaidi kisoko na kimuziki.
Anataja sababu ya kwanza akisema kuondoka kwa waimbaji muhimu katika bendi hiyo mara kwa mara imekuwa ni sehemu inayoathiri bendi kushindwa kupiga hatua za kimaendeleo.
“Kama waimbaji tunatumia gharama kubwa sana kuwaandaa, tunawapika vizuri lakini akishakomaa tu bendi nyingine zinawachukua, hiyo inaturudisha nyuma sana,” anasema na kuongeza:
“Pili, hakuna chombo au Chama imara kwa wasanii wa muziki wa Bendi, kinachoweza kusimamia na kudhibiti changamoto ya mikataba kwa waimbaji na Bendi.Tatizo bendi zetu hazina umoja kwani kila mtu anajali maslahi yake binafsi.”
Mbali na sababu hizo, sababu nyingine anakiri ukuaji wa soko la muziki wa Bongo fleva, kuathiri soko la muziki huo wa dansi nchini. Anasema mazingira ya ushabiki uliopo kwa sasa katika soko la dansi ni tofauti na ilivyokuwa miaka ya 1999 na mwanzoni mwa 2000.
“Sasa hivi Bongo fleva ni kweli imeleta changamoto,mwanzoni tulivyoanza mwitikio ulikuwa mkubwa zaidi kuliko hivi sasa,” anasema.
Hata hivyo, anatupia lawama kwa vyombo vya habari akisema kutokana na mazingira hayo vimepunguza nguvu ya mchango wake kwa bendi za hapa nyumbani.“Mchango wa media umepungua kwa upande wa kupigwa nyimbo hewani tofauti na awali ilivyokuwa,” anasema.
Kuhusu Chamdata anaongeza akisema haina nguvu yoyote ya kifedha ili kujiendesha na badala yake Basata ambao wanatakiwa kusaidia wamekuwa wakikusanya michango ambayo ilitakiwa kukijenga chama hicho kiuchumi.
Kuyumba kwa tawi lake
Katika kipindi cha kuanzia mwaka 1998 mpaka mwaka 2011, Bendi hiyo ilianza kupata mafanikio baada ya kutengeneza tawi la Bendi mpya iitwayo Chumvi Chumvi, ikiwa chini ya Kiongozi wake Ali Choki.
“Bendi hii ilidumu kuanzia mwaka 1998 mpaka 2001, ikapoteza nguvu na kuundwa upya kwa jina la ‘Tamu Tamu’ ,ikiendeshwa chini ya Mwinjuma Muumini,” anasema na kuongeza:
“Ilipofika mwaka 2006, Bendi hiyo ikapotea na kuzaliwa nyingine iitwayo ‘Madiko diko’ ambayo ilikuwa na waimbaji kama vile Greyson Semsekwa na Rich Maarifa.Haikudumu kwa muda mrefu kabla ya kuanzishwa Bendi ya ‘Chipo polo’ iliyokuwa chini ya Msafiri Diofu na Banza Stone.”
Anaongeza akisema hata bendi hiyo ilidumu kwa miaka mitatu tu(2009/10) kabla ya kupotea na kuundwa upya kwa jina la ‘Vibration’ ikiwa chini ya Muumini na Mau Santiago.
“Kundi la wasanii hao wa ‘Vibration’ likaamua kuondoka na kuanzisha bendi yake ya Mashujaa. “Kwa hivyo chanzo cha kuzaliwa kwa bendi ya mashujaa ndiyo hicho,” anasema Asha.