Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Ushirikina, nidhamu mbaya uwanjani ndiyo soka letu

Muktasari:

Inasikitisha zaidi kwa sababu, miaka hii watu wanakwenda kisayansi kuliko mambo ya ushirikina ambayo naamini hayana nafasi ya kuifanya timu kufanya vizuri kwenye mashindano mbalimbali.

Kweli inashangaza sana kusikia miaka hii bado kuna baadhi ya timu zinaendekeza mambo ya ushirikina katika kutafuta matokeo bora kwenye mashindano. Inasikitisha kwa sababu, wakati wenzetu wanasonga mbele kisayansi, sisi bado tunaendelea kujiweka kwenye mazingira ya ushirikina.

Inasikitisha zaidi kwa sababu, miaka hii watu wanakwenda kisayansi kuliko mambo ya ushirikina ambayo naamini hayana nafasi ya kuifanya timu kufanya vizuri kwenye mashindano mbalimbali.

Ni wazi kwamba, unapoona timu inajihusisha na mambo ya kishirikina kwa lengo la kutafuta ushindi, unapata jibu moja tu kwamba timu hiyo haina uwezo wa kupambana uwanjani.

Timu isiyojiandaa vizuri kwa ajili ya kushiriki kwa mafanikio kwenye mashindano, ni wazi hata maandalizi yake ni ya mashaka. Kama timu imejiandaa vizuri kusaka ushindi, kwa nini sasa itegemee ushirikina?

Katika mchezo wa soka, sote tunaamini kuwa timu iliyojiandaa vizuri na kutekeleza mipango yote mizuri ya ushindani, ndiyo huwa kwenye nafasi kubwa ya kufanikiwa kuliko kinyume chake.

Ina maana kwamba, timu ambayo haijajiandaa vizuri kutengeneza ushindani kwenye mashindano ndiyo ambayo hutegemea zaidi miujiza kushinda ikiwa ni pamoja na kujiingiza kwenye mambo ya ushirikina.

Mwishoni mwa wiki hii, Bodi ya Ligi Kuu Tanzania Bara iliziadhibu timu mbalimbali pamoja na wachezaji wa timu kadhaa kutokana na vitendo vya utovu wa nidhamu na ushirikina.

Binafasi nimefurahishwa na hatua hiyo kwa sababu itachochea wachezaji na viongozi kuwa na nidhamu kwenye soka.

Siku zote mchezo wa soka, mbali na kubebwa zaidi na kipaji au vipaji vya wachezaji, lakini pia suala la nidhamu lina nafasi kubwa katika kuufanya mchezo wa soka kuwa wa amani na upendo.

Kwa siku za karibuni, tumekuwa tukishuhudia mechi mbalimbali za Ligi Kuu zikimalizika katika hali ya malalamiko, jambo ambalo limesababisha baadhi kufanya matendo yasiyo na utashi wa mchezo wa soka.

Kwa mfano, viongozi kuwalaumu waamuzi, wachezaji kupigana uwanjani makocha kutoa kauli zisizosaidia hata kidogo kulinda nidhamu ya soka.

Matukio kama haya, siyo tu yanaharibu soka bali pia yanatia aibu soka letu kiasi cha kuonekana kubeba taswira ya uhuni na kukosekana kwa ustaarabu. Katika mchezo wa soka, nidhamu ni jambo muhimu sana. Hata kama mchezaji atakuwa na kipaji kizuri kiasi gani, bado atalazimika kuonyesha nidhamu ili aweze kulinda kapaji chake.

Adhabu zilizotolewa ziwe chachu na fundisho kwa wachezaji, viongozi au timu nyingine zitakazokwenda kinyume. Naipongeza TFF kwa adhabu walizotoa, lakini ni vizuri pia viongozi wakajenga ushindani kwa kuziandaa timu zao kufanya vizuri badala ya kutegemea ushirikina. Wachezaji nao waheshimu nidhamu ya soka kwa faida yao na kizazi kijacho.