Jela mwezi mmoja kwa kuiba 'fire extinguisher' kwenye boti
Muktasari:
- Hamad anadaiwa kutenda kosa hilo Juni 25, 2026 eneo la feri Kigamboni, wilaya ya Kigamboni.
Dar es Salaam. Mahakama ya Mwanzo Kariakoo jijini Dar es Salaam, imemhukumu mvuvi wa samaki, Salmin Hamad (34), kifungo cha mwezi mmoja gerezani baada ya kupatikana na hatia ya kuiba kifaa cha kuzimia moto (fire extinguisher) ndani ya boti ya Kampuni ya Azam Marine.
Mbali na kifungo hicho, mahakama imeamuru kifaa hicho chenye thamani ya Sh120,000, kirudishwe kwa mmiliki wake.
Hukumu hiyo imetolewa leo Ijumaa, Juni 26, 2026 na Hakimu Mkazi Mpoki Mwabela, baada ya mahakama kuridhika kuwa upande wa mashtaka umethibitisha shtaka hilo pasipo kuacha shaka.
"Mahakama imeridhika na ushahidi uliotolewa na mashahidi wawili wa upande wa mashtaka pamoja na kielelezo kimoja, ambacho ni fire extinguisher. Hivyo, mahakama inamtia hatiani mshtakiwa kama alivyoshtakiwa," amesema Hakimu Mwabela.
Akichambua ushahidi uliowasilishwa mahakamani, Hakimu Mwabela alisema shahidi mmoja wa upande wa mashtaka, baharia Usama Hamad, amesema akiwa ndani ya boti akitekeleza majukumu yake ya kufunga mlango, alipewa taarifa na mmoja wa abiria kwamba kulikuwa na mtu aliyekuwa ameondoka na kifaa cha kuzimia moto.
Kwa mujibu wa ushahidi huo, wahudumu wa boti walimfuatilia mtuhumiwa, wakamkamata akiwa na kifaa hicho na baadaye kumfikisha katika Kituo cha Polisi. Baada ya upelelezi kukamilika, alifikishwa mahakamani kujibu shtaka moja la wizi.
Katika utetezi wake, Hamad amedai kuwa wakati akivuka kuelekea upande wa pili wa kivuko, alishangaa akifuatwa na watu waliomkamata, kumvuta kwa nguvu na kumpiga kabla ya kumrudisha ndani ya boti na baadaye kumfikisha kituo cha polisi.
Hata hivyo, baada ya kupitia ushahidi wa pande zote mbili, mahakama imeeleza kuwa upande wa Jamhuri umefanikiwa kuthibitisha shtaka dhidi ya mshtakiwa, hivyo ikamhukumu kifungo cha mwezi mmoja gerezani na kuagiza kifaa hicho kirudishwe kwa mwenye mali.
Kwa mujibu wa hati ya mashtaka, Hamad anatuhumiwa kutenda kosa hilo usiku wa Juni 25, 2026 katika eneo la Kivuko cha Kigamboni, wilayani Kigamboni, ambapo alidaiwa kuiba kifaa cha kuzimia moto mali ya Kampuni ya Azam Marine chenye thamani ya Sh120,000.