Takukuru yamnasa mtuhumiwa aliyekwepa hukumu ya miaka 20 jela
Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Arusha, Zawadi Ngailo, akizungumza na waandishi wa habari jijini Arusha.
Muktasari:
- Alitoroka January mwaka huu wa 2026, kabla ya siku ya kutolewa hukumu yake ya shauri la jinai namba 000011512/2024 aliyoshtakiwa kwa makosa sita, yakiwemo manne ya kutumia nyaraka kwa lengo la kumdanganya mwajiri kinyume cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa katika Mahakama ya Wilaya ya Arusha.
Arusha. Aliyekuwa Mratibu wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (Tasaf) katika Halmashauri ya Jiji la Arusha, Amani Mlay, amekamatwa mkoani Mtwara baada ya kudaiwa kutoroka na kujificha kwa zaidi ya miezi mitano ili kukwepa kutumikia kifungo cha miaka 20 jela.
Mlay alikuwa akikabiliwa na Shauri la Jinai Na. 000011512/2024 katika Mahakama ya Wilaya ya Arusha.
Alishtakiwa kwa makosa sita, yakiwamo manne ya kutumia nyaraka kwa lengo la kumdanganya mwajiri, kinyume cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Juni 24, 2026 jijini Arusha, Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Mkoa wa Arusha, Zawadi Ngailo amesema mtuhumiwa huyo alikamatwa Juni 21, 2026 katika eneo la Mangaka, Wilaya ya Nanyumbu mkoani Mtwara.
Amesema Mlay alikuwa mafichoni tangu Januari mwaka huu, baada ya kutoroka kabla ya siku ya kutolewa hukumu katika shauri hilo.
“Mlay alikuwa akikabiliwa na Shauri la Jinai Na. 000011512/2024 katika Mahakama ya Wilaya ya Arusha, ambapo alishtakiwa kwa makosa sita, yakiwamo manne ya kutumia nyaraka kwa lengo la kumdanganya mwajiri kinyume cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa,” amesema Ngailo.
Kwa mujibu wa Ngailo, baada ya kusikiliza ushahidi wa upande wa Jamhuri pamoja na utetezi wa mshtakiwa, mahakama ilibaini kuwa akiwa Mratibu wa Tasaf katika Halmashauri ya Jiji la Arusha, Mlay aliandaa nyaraka zenye taarifa za uongo katika vipindi tofauti kati ya Mei na Desemba 2023.
Amesema nyaraka hizo zilionyesha kuwa mzabuni alikuwa amewasilisha vifaa vya ujenzi kwa ajili ya mradi wa ujenzi wa uzio katika Shule ya Msingi Shangarao iliyopo jijini Arusha, ilhali hali halisi ilikuwa tofauti.
“Thamani ya vifaa vilivyohusika katika shauri hilo ilikuwa Sh64.2 milioni,” amesema.
Ngailo amesema Mahakama ya Wilaya ya Arusha ilitoa hukumu Januari 16, 2026 na kumtia hatiani Mlay katika makosa manne kati ya sita yaliyokuwa yanamkabili na kumhukumu kifungo cha miaka 20 jela.
“Hata hivyo, mshtakiwa alitoroka siku ya kutolewa hukumu kabla ya kuanza kutumikia adhabu yake, jambo lililoifanya mahakama kutoa hati ya kukamatwa kwake ili aanze kutumikia kifungo hicho mara atakapopatikana,” amesema.
Amesema baada ya kukamatwa kwake, taratibu za kumfikisha mahakamani zinaendelea ili asomewe hukumu hiyo na kuanza rasmi kutumikia adhabu aliyopewa.
Ngailo amewataka wananchi kuendelea kushirikiana na Takukuru kutoa taarifa za vitendo vya rushwa na uhujumu wa uchumi ili kuwasaidia wahusika kuchukuliwa hatua za kisheria.
“Tunaendelea kusisitiza kuwa hakuna mhalifu atakayekuwa salama popote atakapojificha, iwe ndani au nje ya nchi. Takukuru itaendelea kuwafuatilia na kuhakikisha wanakamatwa ili wakabiliane na mkono wa sheria,” amesema.
Akizungumzia tukio hilo, mkazi wa Arusha, Abdul Rajabu amesema wananchi wanafurahishwa na jitihada za Takukuru katika kuwabaini na kuwachukulia hatua watuhumiwa wa vitendo vya rushwa.
“Hii itasaidia watu kutafuta kipato kwa njia halali na kuachana na vitendo vya rushwa katika utoaji wa huduma. Sisi wananchi tunafarijika kuona hatua hizi zikichukuliwa,” amesema.