Rasimu ya Katiba inataja Tunu za Taifa: Ni nani kati yetu anayezijua!
Muktasari:
Ni dhahiri, ndiyo maana hata wakati wa kuandika au kutunga kanuni zinazosimamia Bunge hilo, wengi walipinga kwa mfano uamuzi wa mambo kufanyika kwa njia ya kura ya wazi,waking’ang’ania usiri, ambao hakuna shaka ndiyo unaozaa maovu ambayo baadhi ya wanaCCM wakiwamo viongozi wanatuhumiwa nao.
NImeamua leo nianze kwa kueleza kitu kinachoitwa tunu. Tunaambiwa na wataalamu wa Kiswahili kuwa tunu ni kitu anachopewa mtu na mwingine kuwa ni ishara ya mapenzi, hidaya, zawadi, adia, hiba, azizi.
Tafsiri nyingine ya Kiswahili ya tunu inaeleza kuwa ni kitu ambacho ni adimu kupatikana na chenye kutumika kwa nadra.
Nimetumia maneno tunu baada ya kusoma rasimu ya pili ya Katiba na randama yake na kukutana na neno hili ‘Tunu za Taifa’.
Nimebaini kumbe kuwa Tunu za Taifa ni baadhi ya mambo ambayo yalijadiliwa siku nyingi, yalishapita baada ya kuwa yamejadiliwa na wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba kule Dodoma, lakini bila kufikia mwafaka.
Kumbe, nimebaini kuwa mgawanyiko ndani ya Bunge hili ambalo mara zote nimesema kuwa limegawanyika na kubakia vipande, mgawanyiko wake ulianzia hapo.
Hivyo, nimeamua nikumegee msomaji leo japo kidogo kile kilichoandikwa ndani ya rasimu, kuhusu tunu hizi za Taifa, kitu ambacho huenda wapo baadhi yenu ambao hamjawahi kukiona au hata kukisoma.
Kifungu hiki kinatoka Sura ya Kwanza ya Rasimu, Ibara ya 5: Tunu za Taifa. Sehemu A- inazungumzia Maudhui ya Ibara. Kifungu hiki kinasomeka:
Ibara hii ya Rasimu ya Katiba inapendekeza kuwa Utu, Uzalendo, Uadilifu, Umoja, Uwazi, Uwajibikaji na Lugha ya Kiswahili ambayo ni lugha rasmi ya Taifa, ziwekwe katika Katiba kuwa ndizo Tunu za Taifa.
Binafsi, sina ubishi wowote kuhusu azma nzuri ambayo Tume ya Mabadiliko ya Katiba, chini ya Jaji Joseph Warioba iliiona wakati ule wa kuandika mambo haya ambayo yameandikwa na kuitwa Tunu za Taifa kwamba yana manufaa.
Haya ndiyo yameandikwa kwenye rasimu ya pili na ambayo inajadiliwa kwa sasa ndani ya Bunge hili ambalo hakuna shaka limemeguka na kubakia vipande, halina tena mshikamano, sifa kuu ambayo imewatambulisha na kuwabeba kwa miaka mingi Watanzania.
Nimesikia kutoka kwa baadhi ya watu waliokuwamo ndani ya Bunge hilo kuwa wakati wa kujadili sura hii ya kwanza ya rasimu, ambako nimeambiwa kuwa wajumbe waligawanyika kwa kiasi kikubwa.
Kwa bahati nzuri, wakati ule, wajumbe wale wanaounda kundi la Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) walikuwa bado ndani ya kikao hiki, nimeambiwa kuwa suala la Tunu za Taifa liliwachanganya wengi, kisha likawagawa. Kwa ufupi, hawakukubaliana.
Ukawa, neno ambalo ni ubunifu uliofanyika ndani ya ukumbi ule wa kisasa wa Bunge, limegeuka msamiati maarufu masikioni mwa Watanzania, limezoeleka kwa kiasi kikubwa katika jamii.
Kitu cha kushangaza, ni pale ambako wajumbe wa Bunge hilo wakiwamo wa chama tawala, CCM eti walifika mahali pa kukataa kuzitambua tunu hizi kama zilivyopendekezwa na Tume ya Jaji Warioba.
Nimeambiwa kuwa wajumbe hao wenye fungamano na CCM walipinga dhana zaidi tunu hizi zinazohusu Uwazi, Uwajibikaji na Uadilifu kuchukuliwa kama Tunu za Taifa. Ni kwa nini?
Hakuna shaka kwamba wajumbe hao ambao hadi leo wamo ndani ya ukumbi hao, wamegawanyika, wamo mawaziri, naibu mawaziri na makada wengine maarufu wa chama hiki kikongwe ambacho tangu mwaka 1977 kipo madarakani, kwa nini hawaoni sababu au mantiki ya kuchukuliwa kwa mambo hayo matatu na kuyaenzi?
Je, wanaogopa nini? Ni dhahiri, wengi wao wanasutwa na dhamira, nafsi zao kwani wamekosa uadilifu, hawaoni sababu ya kuenzi uwazi, kaulimbiu ambayo mwenyekiti wao mstaafu, Rais Benjamin Mkapa alieleza mchana kweupe kwamba ni, ‘zama za uwazi na ukweli’.
Hakuna shaka wanaCCM hao wanakinzana na mtazamo huu wa Mzee Mkapa ambaye aliamini katika uwazi na ukweli, kiasi kwamba vipo baadhi ya vyombo kadhaa ya habari hasa vya umma vimeona viige kaulimbiu hiyo na kuitumia hata kama haviendeshwi kwa kuiishi kauli hii kwa vitendo.
Ni wazi kuwa kukataa kwa wajumbe hao wenye fungamano na CCM ambao hawataki kuamini katika uwazi, uwajibikaji na uadilifu, bila shaka wanataka kuhalalisha vitendo vyao viovu, ambavyo vimekuwa kwa muda mrefu vikiendelea kwa miaka mingi, lakini hakuna anayejali au kudiriki kuvikemea.
Ni dhahiri, ndiyo maana hata wakati wa kuandika au kutunga kanuni zinazosimamia Bunge hilo, wengi walipinga kwa mfano uamuzi wa mambo kufanyika kwa njia ya kura ya wazi, waking’ang’ania usiri, ambao hakuna shaka ndiyo unaozaa maovu ambayo baadhi ya wanaCCM wakiwamo viongozi wanatuhumiwa nao.
Ndiyo maana, kumbe wajumbe hao wameng’ang’ania kubaki kwenye Bunge hili licha ya kelele nyingi, vilio vya wadau wa masuala ya siasa, wanaharakati wanaoamini kuwa inafaa mchakato huu kuandika Katiba Mpya uahirishwe kwanza, ili pawepo kwanza maridhiano.
Kukosekana kwa uwazi, uadilifu ndiko kumefanya Bunge hili liendelee kutumia kiasi kikubwa cha fedha za walipakodi kama posho au hata katika kugharimia mambo mengine yasiyo na tija, kama ya kuazima vinasa sauti na kuvilipia mamilioni kwa siku.
Ni wazi Bunge hili mijadala yake imekosa hoja, akidi ya kutosha kutokana na kutokuwamo ndani ya jumba hilo kwa wajumbe wa Ukawa, hoja zake pia zimepwaya, lakini hakuna anayejali.
Kama viongozi wa dini na watu wengine maarufu wameshauri dawa kuwa ni kuwapo kwa maridhiano baina ya pande hizi mbili zinazokinzana kimtazamo, kwanini ushauri wao umekataliwa?
Najiuliza, iko wapi sababu ya msingi ya kuendelea kwa CCM kujiita chama sikivu, kinachowajali watu kama kinashindwa kuona mbele na kuamua kusitisha kwa muda Bunge hili ili kwanza yafikiwe maridhiano ili pande hizi mbili zikutane, zimalize tofauti ili Bunge hili lijadili na kupitisha Katiba ambayo itakuwa ya Watanzania wote?