Ligi Kuu Bora : Bundesliga ligi inayoendelea kutesa duniani

Wachezaji wa timu ya FSV Mainz 05 wakishangilia baada ya kumalizika mechi ya Ligi Kuu ya Ujerumani “Bundesliga’ dhidi ya VfL Wolfsburg huko Mainz wiki iliyopita. Picha na AFP.
Muktasari:
- Kutokana na utafiti huo, Ligi Kuu ya Ujerumani ‘ Bundesliga’ ilipata pointi 60, Ligi Kuu ya England ilipata pointi 55, Ligi Kuu ya Hispania ‘La Liga’ ilipata pointi 46. Jarida la World Soccer linasema katika miaka kadhaa iliyopita Ligi Kuu ya England ilikuwa ikiongoza ikifuatiwa na La Liga halafu Ligi Kuu ya Italia ‘Serie A’.
Ligi Kuu ya Ujerumani ndiyo ligi bora duniani ya soka.
London, England
Utafiti uliofanywa hivi karibuni na Jarida la World Soccer unaonyesha kwamba Ligi Kuu ya Ujerumani ‘Bundesliga’ ndiyo Ligi Kuu bora duniani ya soka kuliko ligi ya England au Ligi ya Hispania ‘La Liga’.
Kwa mujibu wa Jarida la World Soccer, utafiti huo umefanywa kwa kuangalia mambo mbalimbali ili kutambua Ligi Kuu bora ya dunia. Mambo hayo ni kuangalia mahudhurio ya watazamaji viwanjani, masuala ya fedha, mabao yanayofungwa na ushindani wa soka uwanjani katika lig husika na mashindano ya klabu barani Ulaya.
Pia utafiti huo umeangalia umahiri wa makocha wa klabu za ligi mbalimbali, ubora wa viwanja na wachezaji waliowakilisha timu zao za taifa katika Fainali za Kombe la Dunia zilizofanyika Afrika Kusini 2010.
Kutokana na utafiti huo, Ligi Kuu ya Ujerumani ‘ Bundesliga’ ilipata pointi 60, Ligi Kuu ya England ilipata pointi 55, Ligi Kuu ya Hispania ‘La Liga’ ilipata pointi 46. Jarida la World Soccer linasema katika miaka kadhaa iliyopita Ligi Kuu ya England ilikuwa ikiongoza ikifuatiwa na La Liga halafu Ligi Kuu ya Italia ‘Serie A’.
Ligi Kuu ya Ujerumani ambayo kwa msimu huu imeanza 9 Agosti 2013 na inatarajiwa kumalizika 10 Mei 2014, imechaguliwa na Jarida la World Soccer kutokana na kuwa na mambo yote yaliyoangaliwa kama viigezo. Ligi hiyo ina ushindani kwani kila timu katika ligi hiyo msimu uliopita mpaka msimu huu ina uwezo wa kuifunga timu nyingine katika ligi, tofauti ipo kidogo kwa timu zikikutana na Bayern Munich au Borussia Dortmund, lakini timu nyingine zina uwezo wa kufungana.
Pia kwa mujibu wa jarida la World Soccer, Ligi Kuu ya Ujerumani ni bora kuliko ligi nyingine duniani kwa sababu inavutia pia kuitazama kuitazama katika televisheni.
Nguvu nyingine inayoipa ubora Ligi Kuu ya Ujerumani ni mahudhurio ya mashabiki viwanjani kila wiki. Ligi Kuu ya Ujerumani ina wastani wa mahudhurio ya mashabiki 45,179 karibu kila mechi wakati Ligi Kuu ya England ina wastani wa mahudhurio ya mashabiki 35,278 karibu kila mechi huku Ligi Kuu ya England ikiwa na mahudhurio ya wastani wa mashabiki 28,291 na Ligi Kuu ya Italia ‘Serie A’ ikiwa na wastani wa mashabiki 24,363.
Uwanja wa klabu ya Borussia Dortmund unaoitwa Signal Iduna Park unachukua mashabiki 80,000 na kila wiki tiketi zote za mechi huuzwa. Jukwaa la Sudtribune au ‘South Stand’ peke yake linachukua mashabiki 25,000, jukwaa hilo kukaa mashabiki wa damu wa Dortmund. Katika jukwaa hilo mashabiki hushangilia kwa nguvu muda wote, huzomea, hupiga miluzi, huwa na vitu mbalimbali vya kushangilia vyenye rangi za klabu hiyo na hivyo kufanya jukwaa hilo kuwa la kuvutia muda wote.
Pia klabu ya Bayern Munich inatumia uwanja wa Allianz Arena, ambapo mashabiki 76,000 kila wiki huujaza uwanja huo.
Ushindani mwingine unaoonekana katika Ligi Kuu ya Ujerumani ni kwamba tangu mwaka 2006 kumekuwa na mabingwa wanne tofauti wa Bundesliga tofauti na ilivyo katika Ligi Kuu nyingine hasa za Ulaya.
Katika Ligi Kuu ya Ujerumani hakuna suala la timu nne bora ‘Big Four’ au timu mbili bora ‘Big Two’ zinazowania ubingwa kila mwaka. Katika Ligi Kuu ya Ujerumani kila mwaka timu tofauti hushika nafasi nafasi za juu na nyingine hushuka chini, Ligi Kuu ya Ujerumani haitabiriki na inavutia msimu mzima.
Ligi Kuu ya Ujerumani pia ina ushindani na mvuto kwa sababu ya mfumo mzuri wa kuibua vipaji uliopo kwa klabu za Ligi Kuu. Katika Ligi Kuu za Hispania na England klabu zina akademia katika ngazi za juu tofauti na klabu za Ujerumani, ambapo klabu zina akademia tangu ngazi za chini kabisa zinazochukuwa watoto bila kuangalia idadi.
Ndiyo maana klabu za Ujerumani zinaweza kuibua wachezaji wengi kila mwaka kama Mario Gotze, Marco Reus, Mesut Ozil, Sami Khedira, Toni Kroos, Thomas Muller, Ilkay Gundogan, Julian Draxler, Leon Goretzka, Mats Hummels, Andre Schürrle, Lewis Holtby, Mesut Ozil na wengine wengi wanaofanya vizuri katika soka hivi sasa duniani.
Suala lingine linaloifanya Ligi Kuu ya Ujerumani kuwa bora na kuendelea kutesa ni kutokana na klabu za ligi hiyo kukosa madeni. Klabu za nchi nyingi zina madeni. Klabu kama Chelsea, Manchester City, Juventus, Valencia na Malaga zote za England, Italia na Hispania zimekuwa zikikabiliwa na madeni kwa miaka mingi sasa huku zikiwa zinakosa njia sahihi za kumaliza madeni hayo. Hata hivyo klabu zenye madeni makubwa zaidi ni klabu za Malaga na Valencia za Hispania.
Lakini klabu za Ujerumani hazina madeni kwa sababu mfumo wa uendeshaji wa klabu hizo hauruhusu. Klabu za Ujerumani zimejifunza kuepuka kusajili kwa gharama kubwa wakati wa kipindi cha usajili na badala yake zinategemea zaidi mfumo wao wa kuibua wachezaji vijana ambao wameujenga kwa muda mrefu kupitia mfumo wa akademia.
Zifuatazo ni Ligi Kuu 25 bora duniani kuanzia namba 25 mpaka namba 1:
25. Uruguay | Primera Division
25. Afrika Kusini | Premier Soccer League
25. Scotland | Premier League
25. Paraguay | Primera Division
23. UAE | Pro League
23. Ecuador | Serie A
20. Poland | Ekstraklasa
20. Colombia | Primera A
20. Australia | A-League
19. Switzerland | Super League
18. Sweden | Allsvenskan
15. Ukraine | Premier League
15. Uturuki | Super League
15. Ubelgiji | Pro League
14. China | Super League
13. Russia | Premier League
11. Ureno | Primeira Liga
11. Japan | J1 League
10. Argentina | Primera Division
9. Ufaransa | Ligue 1
8. Uholanzi | Eredivisie
7. Marekani | MLS
6. Mexico | Liga MX
5. Brazil | Serie A
4. Italia | Serie A
3. Hispania | La Liga
2. England | Premier League
1. Ujerumani | Bundesliga