Nyerere alivyoimarisha uhusiano wa kimataifa

Mwalimu Nyerere akiwa na kiongozi wa Cuba, Fidel Catsro. Picha ya Maktaba
Muktasari:
- Hatimaye mwana wa Afrika alivuka mipaka na kuingia Marekani akiitika wito wa mwenyeji wake, Rais John F. Kennedy. Ziara hii aliifanya siku chache tu baada ya kutoka Mtwara. Wawili hawa walishibana kiasi cha kuitwa marafiki wa chanda na pete. Kila mmoja alimtosha mwenzake. Ulikuwa ujumbe wa kwanza kutoka Afrika katika ikulu ya Marekani.
Kiangazi kinapuliza na Mwalimu Nyerere amemaliza mkutano wake wa Halmashauri Kuu ya Chama cha Tanu uliofanyika mkoani Mtwara.
Hatimaye mwana wa Afrika alivuka mipaka na kuingia Marekani akiitika wito wa mwenyeji wake, Rais John F. Kennedy. Ziara hii aliifanya siku chache tu baada ya kutoka Mtwara. Wawili hawa walishibana kiasi cha kuitwa marafiki wa chanda na pete. Kila mmoja alimtosha mwenzake. Ulikuwa ujumbe wa kwanza kutoka Afrika katika ikulu ya Marekani.
Ingawa vuguvugu la ukombozi barani Afrika lilikuwa juu, lakini ziara ya Mwalimu Nyerere ilitegua kitendawili kilichohusu uhusiano wa Marekani na mataifa ya Afrika na namna Ulaya ilivyokuwa ikicheza na siasa za Afrika.
Katika dhifa ya Taifa ambayo Rais Kennedy alimwandalia mgeni wake katika Ikulu ya White House, Mwalimu Nyerere alitoa hotuba iliyojaa mitego lakini yenye wingi wa maneno yenye nasaha za kidiplomasia.
Ikitazamwa kuwa ni miaka miwili tu imepita tangu Tanganyika kupata uhuru wake kutoka Uingereza ulimwengu ulistaajabishwa na ziara hiyo. Ulishangaa kuona inawezekanaje mkubwa na mdogo wakala katika meza moja. Tena walipata hofu kuona wawili hawa waliweza kupiga soga na kugongeana mikono.
Haikufahamika ni lini wawili hao walianza kujenga urafiki wao na kwa namna gani walianza kuaminiana, lakini Mwalimu Nyerere alipokanyaga kwa mara ya kwanza katika Ikulu ya White House Julai 14,1963 aliisifu Marekani.
Nyerere alimwambia mwenyeji wake, Tanzania kama ilivyo Marekani ni Taifa lenye mchanganyiko wa watu, kuanzia wale wazawa mpaka wahamiaji. Lakini, alisisitiza kuwa ingawa watu hao wana asili tofauti jukumu analoliona mbele ni kuhakikisha anaendeleza mapambano ya kuwaendeleza na kuwajenga kiuchumi.
Alidai ingawa mapambano ya kudai uhuru yamekamilika, lakini itakuwa haina maana kama ataendelea kubweteka na kuacha matabaka yakichipua. Mtu wa kwanza kuhutubia kwenye hafla hiyo alikuwa Rais Kennedy.
Hotuba yake ilijaa maneno yenye sifa na heshima iliyomwendea Mwalimu Nyerere. Kennedy anayetajwa kupendwa zaidi katika historia ya marais wa Marekani alimtaja Nyerere kama mtoto wa kweli wa Tanganyika na Afrika.
Aliusifu uongozi wake alioutaja kuwa wenye kuzingatia misingi ya haki na usawa. Suala la Jumuiya ya Afrika Mashariki, harakati za ukombozi wa bara la Afrika lilijitokeza pia katika hotuba yake. Alimwelezea Nyerere kama kiongozi aliyekuwa mstari wa mbele kufanikisha yote hayo.
Aligusia pia namna viongozi wa nyuma wa Marekani walivyovutiwa na juhudi zake kiasi cha kukumbusha historia ya Marekani ambayo wakati fulani ilitawaliwa na itikadi za ubaguzi na utesaji wa makundi ya wachache.
“Juhudi zako za kupigania haki na kuleta usawa kwa wananchi wa Tanganyika na Afrika zinakumbusha namna pia waasisi wetu hapa Marekani walivyohangaika kuleta umoja na usawa hapa nchini,” jinsi ilivyokuwa sehemu ya hotuba yake.
Ziara hii ilifungua enzi mpya ya uhusiano kati ya mataifa haya mawili na kikubwa zaidi ilikuwa kama mlango kwa nchi za Afrika kwa Marekani.
Ingawa wakati huo wanaharakati wengi wa Afrika walipata ufadhili na kuingia nchini humo kwa ajili ya masomo, lakini hata hivyo, Marekani iliendelea kufanya kile kinachoitwa ‘kuuma na kupuliza’ kuhusu nafasi ya Afrika katika siasa za kimataifa.
Lakini, kishindo kikubwa kilijitokeza wakati Mwalimu Nyerere aliporejea tena Marekani kwa ziara ya pili ya kiserikali aliyoifanya mwaka 1977, akialikwa na mwenyeji wake, Rais Jimmy Carter.
Upepo wa siasa za dunia ulikuwa umebadilika huku mvutano kati ya madola ya magharibi umepevuka. Nguu za Urusi ya zamani (USSR), kujaribiwa kwa nguvu za Umoja wa Mataifa (UN), kuimarika kwa kile kilichofahamika Mataifa Yasiyofungamana na Upande Wowote, kupanuka kwa Siasa za Ukombozi Kusini mwa Afrika, ni baadhi ya mambo yaliyoifanya ziara ya Mwalimu Nyerere ifuatiliwe na wengi.
Nyerere alifanikiwa kuchanga vyema karata zake. Hotuba yake ilijaa sifa namna dunia inavyoionea gere Marekani kwa kuwa taifa lenye ushawishi mkubwa duniani. Alisema watu wengi duniani wangependa kushiriki katika uchaguzi wa rais wa Marekani lakini bahati mbaya hilo haliwezekani.
Ingawa hakutaka kufichua mengi kwenye hotuba yake hiyo, Mwalimu Nyerere alimalizia kwa kuelezea matumaini yake namna atakavyojadiliana na mwenyeji wake kuhusu ukombozi wa kusini mwa Afrika.
Ziara hii ambayo aliifanya miaka 14 baadaye baada ya kufanya ziara ya kwanza ilisaidia kuishawishi Marekani kuwabana watala wa wakati huo nchini Zimbabwe, Namibia na utawala wa kibaguzi wa Afrika Kusini. Akiwa kiongozi wa nchi zilizoko mstari wa mbele, Mwalimu Nyerere alikuwa na ujumbe mwingine unaokaribiana na huo wakati alipofanya ziara ya kwanza ya kiserikali nchini Uingereza mwaka 1975.
Licha kwamba Mwalimu Nyerere wakati fulani alitibuana na baadhi ya mataifa ya magharibi, lakini ajenda yake ya kuikomboa Afrika na kukaribisha maendeleo nchini mwake ilihamishia katika mataifa ya Asia. Ni wakati ndipo taifa kama China lilianza kupata marafiki wapya barani Afrika.