Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Nikki wa Pili: Mikakati ni mingi baada ya PhD

Nikki wa Pili

Muktasari:

  • Hivi karibuni Nikki wa Pili ambaye jina lake halisi ni Nickson Simon alitangaza uamuzi wake wa kusoma PhD na tayari ameanza masomo katika Chuo Kikuu ch Dar es Salaam(UDSM) katika masuala ya maendeleo(Development Studies.

Rapa Nikki wa Pili kutoka Kampuni ya Weusi ameweka wazi mikakati yake na kile atakachofanya baada ya kumaliza Shahada yake ya Uzamuvu (PhD).

Hivi karibuni Nikki wa Pili ambaye jina lake halisi ni Nickson Simon alitangaza uamuzi wake wa kusoma PhD na tayari ameanza masomo katika Chuo Kikuu ch Dar es Salaam(UDSM) katika masuala ya maendeleo(Development Studies.

 Kupitia mahojiano yafuatayo, pamoja na mambo mengine Nikki wa Pili anaweka wazi anayotarajia kuyafanya katika muziki wa Bongo Fleva baada ya kumaliza elimu PhD.

Starehe: Kuna uhusiano gani wa elimu na sanaa yako?

Nikki wa Pili: Uhusiano unaweza usionekane moja kwa moja, lakini elimu inaweza kunisaidia kwa mambo mengi katika safari yangu ya muziki na maisha nje ya muziki.

Starehe: Mpaka sasa kuna mchango gani uliotoa kutumia elimu yako katika kuendeleza moto za Bongo Fleva?

Nikki wa Pili: Nimejaribu kufanya kwa kiwango fulani katika ushawishi. Kwanza, nimeshiriki harakati za kuishawishi Serikali itambue kikatiba umuhimu wa sekta ya sanaa.

Pili, nimeshiriki nikiwa mstari wa mbele kama mfano, kupinga unyonyaji unaofanywa kupitia milio ya simu. Nilitangaza kujiondoa Kampuni ya Spice VAS Africa na Push Mobile mwaka jana na  baadhi wakafuata baada ya kuelimisha kuhusu unyonyaji huo.

Wasanii wengi bado hawafahamu hata makadirio ya faida au mapato yanayoingia kupitia milio ya nyimbo zao.

Hiyo ni hatari sana. Kampuni za simu zinachukua asilimia 60, mzalishaji anachukua 31 na mpaka hatua ya mwisho msanii anapata asilimia 2 hadi 6.

Harakati za kujiondoa huko zinaathiriwa na mfumo, inahitaji safari ndefu ya ushiriki wa Serikali na uamuzi wa wasanii wenyewe. Kwa hivyo, nikimaliza PhD nitakuwa na nafasi nzuri zaidi ya kuendeleza harakati hizo, ili siku moja tuone muziki wetu unaondolewa mizizi ya unyonyaji.

Mbali na harakati hizo, nimekuwa muelimishaji wa fursa za ajira kupitia semina iliyoandaliwa na Clouds Media Group.

Semina hiyo iliitwa Fursa, pia mimi ni Balozi wa Kupinga Rushwa, mtetezi wa haki za binadamu na mwanaharakati wa ulinzi wa mtoto dhidi ya unyanyasaji.

Starehe: Harakati hizo umezifanya wapi na kwa muda gani?

Nikki wa Pili: Baada ya kumaliza Shahada yangu ya Uzamili, nilipata nafasi ya kufanya kazi katika Shirika la Kimataifa linalojihusisha na Ulinzi wa Mtoto Dhidi ya Unyanyasaji na Utelekezwaji barani Afrika (African Networking for Prevention and Protection Against Childrens).

Nimefanya kwa kipindi cha mwaka 2011 mpaka 2012, nikiwa mshauri. Kwa hapa nchini ofisi zao zilikuwa Kijitonyama.

Hivyo, nina uzoefu na ninaguswa na harakati hizo.Shirika hilo linafanya kazi kwenye nchi 23 barani Afrika na limekuwa na harakati hizo kwa miaka mingi.

Starehe: Kwa maana hiyo ikitokea leo hii tumesikia umeacha muziki, tutarajie utakuwa kwenye ofisi gani baada ya PhD?

Nikki wa Pili: Eee..., ikitokea hivyo, basi nitafanya kazi kwenye ofisi za uandaaji wa sera, utafiti au uendeshaji wa miradi mbalimbali ya kijamii.

Starehe: Utawezaje kulinda ratiba yako ya masomo na muziki?

Nikki wa Pili: Ratiba haiwezi kuathiri hata kidogo, nimefanikiwa kusoma tangu shahada ya kwanza mpaka sasa nikiwa kwenye muziki, hivyo, haiwezi kunipa shida, sitoacha muziki.

Starehe: Uamuzi wa kurudi kwenye masomo inaweza kuwa changamoto yoyote kwa wasanii wenzako?

Nikki wa Pili: Wasanii kwa sasa wameamka, watambua umuhimu wa elimu siyo kama ilivyokuwa mwanzoni. Mimi nimetumia nafasi yangu, ila naamini kuna wasanii wanaotamani kurudi shuleni, lakini wamebanwa na ratiba tu za muziki.