Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Nondo za Aunt Leila kwa wanandoa, wenza

Muktasari:

  • Ni mwanamama mtaalamu wa saikolojia na afya ya akili, aliyejizolea umaarufu mkubwa katika mitandao ya kijamii akitoa ushauri kuhusu masuala ya uhusiano.

Dar es Salaam. Katika ulimwengu wa kisasa unaoendeshwa na teknolojia, mitandao ya kijamii na majukwaa ya kidijitali yamekuwa sehemu muhimu ya maisha ya kila siku.

Sambamba na ukuaji huo, changamoto mbalimbali za kijamii zinazowakumba watu zinawafanya kuhitaji msaada na ushauri ili kukabiliana nayo.

Hapa ndipo watoa nasaha kupitia mitandaoni wanapochukua nafasi muhimu kwa kutoa miongozo, msaada wa kisaikolojia na ushauri kwa watu wanaopitia changamoto mbalimbali.

Kama ni mfuatiliaji wa mada mbalimbali zinazotolewa na wanasaikolojia pamoja na washauri mitandaoni  kuhusu uhusiano, jina la Madam Leila Abubakar litakuwa si geni kwako.

Huyu ni mtaalamu wa saikolojia na malezi ambaye amejizoelea umaarufu katika mitandao mbalimbali ya kijamii hasa Instagram na Tiktok,  kwa kuzungumzia masuala ya uhusiano na ndoa, afya ya akili pamoja na malezi.

Mwananchi limefanya mahojiano na mtaalamu huyu kufahamu nini hasa kilichomsukuma kutumia mitandao ya kijamii kuhubiri kuhusu masuala ya ndoa na malezi.


Swali:  Nini kimekusukuma kuzungumzia habari za ndoa na uhusiano?

Jibu: Kilichonisukuma kuzungumzia habari za uhusiano na ndoa ni kutokana na mambo hayo kuwasumbua watu wengi hasa nyakati za sasa.

Kupitia uzoefu wangu wa kufanya kazi katika upande wa saikolojia na afya ya akili,  nimeona eneo hilo ndilo linaongoza kwa kuwasumbua watu wengi na kusababisha changamoto mbalimbali za afya ya akili.

Kwa asilimia karibu 60, suala la mapenzi na uhusiano linachangia watu kuingia katika changamoto ya afya ya akili.

Leila Abubakar

Pia kuna uporomokaji wa  maadili katika jamii,  hivyo vimenisukuma kama mtaalamu, mdau wa masuala ya kijamii kuona haja ya kuyaongelea mambo haya na kuisaidia jamii inayonizunguka na kunisikiliza.


Swali: Jamii inayapokeaje mawazo yako?

Jibu: Jamii inayonizunguka imenipokea vizuri na inaniunga mkono kwa sababu mambo ninayoyazungumza yapo yapo ndani ya utamaduni na yanajitokeza katika maisha yetu ya kila siku.

Watu wa hapa nchini na mabara mbalimbali kama vile Asia, Ulaya na Marekani, huwa wananipigia simu na kunipongeza kuwa ninafanya jambo zuri kwa jamii.

Familia yangu kwa ujumla wanajivunia, wamelipokea kwa mikono miwili na wamekuwa wakinipa ushirikiano mkubwa.

Wao ndio sababu ya mimi kutoa nasaha zangu mtandaoni. Walinishauri kuwa kwa kufanya hivyo kazi zangu zitawafikia watu wengi, nikafanyia kazi ushauri wao ambao umenisaidia kwa kiasi kikubwa kufikia hapa.


Swali:  Kwa mtazamo wako, unadhani nini kinakwaza wanandoa wengi kutodumu katika ndoa?

Jibu: Wanandoa kutodumu katika ndoa kunasababishwa na  wenza kuingia kwenye ndoa bila ya kufahamiana vizuri.

Unakuta mwenza hajui vizuri tabia za mwenzake, vipaumbele na malengo yao   hawawekeani bayana tangu mwanzoni, hivyo inakuwa ngumu kuelewana.

Mambo mengine yanayochangia ni pamoja na kukosekana kwa uvumilivu, malezi pamoja na vijana kuingia katika ndoa bila ya kuandaliwa kwa jambo hilo.  


Swali:  Je, ni sahihi kusema kuwa ndoa si jambo jepesi na watu wasikurupuke?

Jibu: Ni sahihi ndoa si jambo jepesi hata katika imani yangu ya Kiislamu, imebainishwa bayana kuwa ndoa ni ibada.

Ibada yoyote inahitaji uifahamu vyema na uwe na  utulivu. Si jambo ambalo unafanya tu kwa sababu wengine wanafanya.

Hivyo hivyo katika ndoa, usiingie eti kwa sababu wengine wanaolewa au umri wako umekwenda, inahitaji fikra yakinifu na utulivu katika kufanya uamuzi katika mambo hayo.


Swali:Unadhani ni mambo gani yanastawisha ndoa?

Jibu: Ili ni ndoa iweze kustawi kwanza wanandoa wanatakiwa kumtanguliza Mungu mbele katika maisha yao na kuwa na mapenzi na maelewano baina yao.

Pia kuwa na mtu  anayekuhitaji, usipende kulazimisha kuwa na mtu ambaye yeye hakuhitaji katika maisha yake kwani madhara yake hapo baadaye ni makubwa.

Baadhi yao hujipa matumaini kuwa mwenza wake atabadilika hapo baadaye, isipotokea hivyo inaweza ikamuumiza.


 Swali:Unazungumziaje mtindo wa sasa wa baadhi ya wanawake kutaka kulea mtoto au watoto bila baba?

 Jibu: Sidhani kama ni sahihi, kama hakuna changamoto yoyote ningesisitiza watoto walelewe na wazazi wote wawili.

Hivi sasa changamoto nyingi za saikolojia na malezi zilizopo, ni pamoja na mtoto kulelewa na mzazi mmoja. Kama hakuna sababu ya msingi ya kufanya hivyo, ni vyema wazazi kushirikiana kwa pamoja katika suala la malezi.


Swali: Inawezekana kuwa na usawa katika ndoa kati ya mume na mke?

Jibu: Haiwezekani kuwa na usawa katika ndoa kati ya mwanamke na mwanaume, imeelezwa siku zote mwanamke atatii na mwanaume atapenda.

Pia hata katika vitabu vya dini imewekwa bayana kuwa mwanaume atatafuta kwa jasho na mwanamke atazaa kwa uchungu. Pia hata katika jamii zetu inaelezwa kuwa mwanaume ni kichwa cha familia na mwanaume ni shingo.

Hiyo ina maana kuwa kuna baadhi ya majukumu ya mwanaume mwanamke hawezi kuyafanya. Pia kuna yale ya mwanamke ambayo mwanaume hawezi kuyafanya.


Swali:Upi wito wako kwa watu wanaotarajia kuingia katika ndoa?

Jibu: Kwanza kumtanguliza Mungu ili aweze kuwaongoza katika maisha hayo ya ndoa. Pia hakikisha unamfahamu vyema mwenza anayetaka kuingia naye katika ndoa na kutopuuzia tabia zozote ovu zinazojitokeza kipindi cha uchumba.

Wasilazimuishe ndoa na watu walionyesha bayana kutowahitaji katika maisha yao. Vilevile wanapochagua wenza watangulize utu na kuacha kuweka tamaa ya pesa mbele.


Swali:Unaweza kutueleza kwa ufupi kuhusu historia yako?

Jibu: Mimi ni mzaliwa wa sita katika familia ya watoto 11. Katika upande wa taaluma mimi ni mwalimu, mtaalamu wa masuala ya afya ya akili, saikolojia na malezi.

Nimefanikiwa kufungua kampuni yangu ambayo inashughulika na masuala ya afya ya akili na ushauri nasaha.

Kupitia kampuni hiyo nimefanikiwa kutoa mafunzo na ushauri kwa watu katika maeneo.