Walimu walia kutengwa mchakato wa sera mpya ya elimu

Mwalimu akiwajibika darasani. Walimu wanasema hawashirikishwi ipasavyo katika mchakato unaoendelea wa utengenezaji wa sera mpya ya elimu.
Muktasari:
SERIKALI kupitia Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, imeanza mchakato wa kuifanyia marekebisho sera ya elimu ya mwaka 1995.
SERIKALI kupitia Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, imeanza mchakato wa kuifanyia marekebisho sera ya elimu ya mwaka 1995.
Kwa muda mrefu wadau wa elimu nchini wamekuwa wakiikosoa sera hiyo wakisema pamoja na mambo mengine inachangia kurudisha nyuma kiwango cha elimu nchini.
Kukubali kwa Serikali kuifanyia uboreshaji sera hiyo ni faraja kubwa kwa wadau hao kwa kuwa hiyo ndio nguzo muhimu kuelekea katika mafanikio ya kweli ya sekta ya elimu.
Hata hivyo, pamoja na kuwa sera ni jambo linalowahusu wadau wengi wakiwamo walimu, mchakato wa marekebisho ya sera mpya unadaiwa kuwapa kisogo walimu wanaosema ushiriki wao ni muhimu kwa mafanikio ya sera husika.
Rais wa Chama cha Walimu (CWT), Gratian Mukoba, anasema kuwa tangu kuanza kwa mchakato wa utungwaji wa sera mpya,walimu hawashirikishwi ipasavyo katika kutoa maoni yao.Ni mara moja tu anasema CWT kilialikwa, lakini sasa hawajui kinachoendelea.
“Kuitwa kwenyewe ilikuwa tunakwenda kusikiliza waliyopendekeza wao, siyo kwamba tunakaa meza moja tunasema hili liingie likae hivi na ili liwe vile, kwa hiyo siwezi kusema kuwa tunashirikishwa. Wao ndio wanakuja na mambo yao ambayo wanataka yaendelee kuwepo kwenye sera hii,”anafafanua.
Kwa sababu hiyo anasema ana wasiwasi kama sera hiyo italeta mabadiliko ya kweli katika sekta ya elimu pale itakapopitishwa, kwa kuwa walimu ambao ndio watekelezaji wa sera hiyo hawajashiriki kuitengeneza.
Aidha, akitoa mfano wa mambo yanayopaswa kuwapo katika sera mpya, Mukoba anasema sera mpya lazima ieleze namna ya kumjenga mwanafunzi tangu akiwa ngazi za chini za elimu.Anasema:
“Mtoto ajengeke kwenye nyanja zote, kuanzia awali kabisa lazima apatiwe msingi imara. Watekelezaji wa sera ambao ni walimu wanajua nini kikifanyika hili litawezekana.”
Kwa upande wake, Mwalimu Golden Kihahi anayefundisha Shule ya Msingi Ulinji iliyopo Kata wilayani Sumbawanga, anasema hajui kinachoendelea kuhusu mabadiliko ya sera.
Hata hivyo, angependelea sera hiyo mpya ikaruhusu mwanafunzi anayepata ujauzito kuendelea na masomo baada ya kujifungua.
Kwa kufanya hivyo, anasema kutawapa fursa ya wanafunzi kujenga maisha yao na watoto wanaowazaa, kwa kuwa kuwanyima fursa ya kuendelea na elimu, kunaendeleza umaskini na ongezeko la watu wasio na elimu.
Naye mhadhiri wa Shule Kuu ya Elimu katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Kitila Mkumbo anasema kuwa sera hiyo haitokuwa na tija kama walimu hawatashirikishwa kikamilifu katika uandikwaji wake.
“Lengo lilikuwa ni kuwashirikisha walimu, kama hawatashirikishwa haitakuwa na maana. Lazima wadau wa elimu washiriki vya kutosha,” anasema.
Kwa upande wake anapendekeza sera mpya kufafanua kuhusu lugha inayofaa kuwafundishia wanafunzi shuleni,kama anavyosema:
“ Lazima tuhakikishe watoto wetu wanajua lugha ya Kiswahili pamoja na Kiingereza. Kuwepo na msisitizo watoto waweze kuzifahamu vema lugha hizi. ”
Ukitoa walimu, wadau wengine wa elimu kama asasi za kiraia zinasema ushirikishwaji wao katika mchakato haujawa wa kuridhisha.
“Sisi tunashirikishwa kupitia TenMet, (Mtandao wa Elimu Tanzania), lakini bado ushirikishwaji huu hauridhishi kwa sababu wakati mwingine mwaliko unakuja kwa kuchelewa sana, hivyo inakuwa vigumu kujipanga na hata kusoma makarabrasha wanayoleta,” anasema Meneja wa Idara ya Utafiti na Uchambuzi wa Sera kutoka shirika la HakiElimu, Boniventure Godfrey.
Pamoja na kutoshirikishwa huko, anasema kuwa sera mpya ya elimu haitokuwa na maana yoyote endapo haitoainisha mikakati ya kukuza elimu kuanzia ile ya awali.
Anasema kuwa, licha ya kuwa elimu ya awali inazungumziwa katika sera iliyopo , utekelezaji wake haujafafanuliwa, jambo linalofanya chanzo cha bajeti yake kisieleweke.
“Hili suala lipo kisiasa sana, wanasema tu kila shule iwe na darasa la awali, lakini hakuna bajeti inayotengwa kwa ajili ya madarasa ya awali na wala haijulikani ni ni nani anatakiwa afuatilie utekelezaji wake,” anaeleza na kuongeza:
“ Bila kujenga msingi wa madarasa haya, hakutakuwa na mabadiliko ya elimu kama tutaanza kutilia mkazo wa watoto wa kuanzia darasa la kwanza.’’
Aidha, anapendekeza sera mpya kuangalia suala la shule kupewa mamlaka ya kuwafukuza wanafunzi wanaotoroka shule kwa siku 90 bila kujali sababu inayowafanya kuwa watoro.Kwa mtazamo wake, anasema uamuzi huo unawanyima wanafunzi hao haki yao ya kupata elimu.
“Waangalie ni kwa nini huyu mwanafunzi amekaa nyumbani kwa kipindi hicho, alikuwa anaumwa ama alikuwa na shida gani, siyo tu kuwafukuza shule,” anasema.
Kauli ya Serikali
Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Philip Mulugo, anasema hawajawatenga wadau wa elimu na kwamba hivi sasa wameanza kukutana na taasisi za ndani kabla ya kukutana na wadau wengine baadaye.
“Juzijuzi tu hapa tulikutana na taasisi za ndani kama Necta (Baraza la Mitihani la Taifa) na TCU (Tume ya Vyuo Vikuu). Sasa hivi mapendekezo yao ndio yanapitiwa na kuwekwa vizuri kisha tutakwenda kwa wadau wengine,” anasema na kuongeza:
“Tutapanga namna ya kushirikisha maofisa elimu ambao ndio watekelezaji pamoja na walimu, tutakutana nao na kujadili ili mwishowe tupate kitu chenye manufaa.”
Anasema mchakato wote huo utafanyika kwa haraka, ili kuhakikisha kuwa utengenezaji wa sera hiyo unakamilika kwa haraka.