Prime
HUKUMU MAUAJI YA MUUZA MADINI MTWARA:Kutoka mipango, mauaji mpaka kunyongwa askari Polisi – 5

Muktasari:
- Huu ni mwendelezo wa mapitio ya hukumu ya kesi ya mauaji iliyokuwa ikiwakabili maofisa na askari saba wa Jeshi la Polisi mkoani Mtwara.
Dar es Salaam. Katika sehemu hii ya mapitio ya hukumu hii, upande wa mashtaka unaendelea kuchambua ushahidi wake namna ulivyoweza kuthibitisha viini vitatu vya hatia ya kosa la mauaji dhidi ya washtakiwa.
Washtakiwa hao katika kesi hii ni aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi Wilaya ya Mtwara, Mrakibu wa Polisi, Gilibert Kalanje na aliyekuwa Mkuu wa Kituo Kikuu cha Polisi Mtwara, Mrakibu Msaidizi wa Polisi, Charles Onyango.
Wengine ni aliyekuwa Mkuu wa Intelijensia wa Wilaya ya Mtwara, Nicholous Kisinza; Mkaguzi Msaidizi wa Polisi, Marco Chigingozi, Mkaguzi wa Polisi, John Msuya, Inspekta msaidizi, Shirazi Mkupa na Koplo Salim Mbalu.
Wote walishtakiwa kwa kosa la kumuua kwa kukusudia, mfanyabiashara wa madini, Mussa Hamis, Mkazi wa Wilaya ya Nachingwea mkoani Lindi Januari 5, 2022, ndani ya kituo cha Polisi Mitengo, katika Wilaya ya Mtwara.
Katika sehemu iliyopita, upande wa Jamhuri ulichambua ushahidi wake na kuonesha imeweza kuthibitisha kifo cha Mussa hakikuwa cha kawaida.
Uhusika wa washtakiwa
Ili mshtakiwa wa kosa la mauaji apatikane na hatia ya kosa la mauaji ya kukusudia, ushahidi wa upande wa mashtaka unapaswa uthibitishe pasi na shaka kuwa ni mshtakiwa au washtakiwa ndio waliohusika kutenda kosa hilo na si mwingine.
Katika kesi hii Jamhuri ilianza kujenga hoja zake za msingi za ushiriki katika kosa la mauaji, ikirejea uamuzi wa Mahakama ya Rufani (iliyoketi Bukoba) katika rufaa baina ya Robert Berenado Steven dhidi ya Jamhuri, ilitoa msimamo kwamba:-
“Ni msingi thabiti wa kisheria kwamba kila mtu anayeshiriki kwa namna yoyote katika kusaidia, kuchochea, kushauri au kupanga kutendeka kwa kosa ni mtendaji mkuu wa kosa hilo kwa mujibu wa kifungu cha 22(1) cha Kanuni ya Adhabu…,”
Hivyo Jamhuri ilieleza kuwa kwa mujibu wa ushahidi wa mazingira, ushahidi wa washtakiwa wenza, kanuni ya mtu wa mwisho kuwa na marehemu, pamoja na ushahidi wa moja kwa moja uliotolewa, umeweza kuthibitisha kesi hiyo kikamilifu kwamba washtakiwa wote wanawajibika kwa kifo cha marehemu huyo.
Ushahidi wa mazingira
Ikizungumzia ushahidi wa mazingira katika kuthibitisha kosa, Jamhuri iliirejesha mahakama katika hukumu ya Mahakama ya Rufani kwenye hukumu yake ya rufaa baina ya Jamhuri dhidi ya Godson Laurent @ Mzaula & Wengine.
Katika hukumu hiyo, Mahakama ya Rufani ilisema kuwa ushahidi wa mazingira unaweza usiwe tu wa kuthibitisha, bali hata ukawa wa uthibitisho mkubwa kuliko ule wa shahidi wa macho aliyeshuhudia tukio la mauaji.
Jamhuri ilieleza kuwa ushahidi iliouwasilisha kupitia mashahidi wake, umeonyesha bila kuacha mashaka washtakiwa hao ndio wahusika wa mauaji hayo.
Katika hoja hiyo, Jamhuri imerejea ushahidi wa mashahidi wake walioelezea matukio mbalimbali kabla, wakati na baada ya kumkamata Mussa mpaka mauaji yake na kuyataja matukio hayo kuwa ni pamoja na:
Washtakiwa kumkamata Mussa katika lodge (nyumba ya kulala wageni) aliyokuwa amefikia mjini Mtwara, kwenda nyumbani kwao kijijini kufanya upekuzi, wakachukua pesa zake ambazo ilielezwa kuwa mpaka sasa ni washtakiwa tu ndio wanaofahamu mahali zilipo, ushahidi ulioungwa mkono na mshtakiwa wa tatu, wa nne, wa sita na wa saba.
Pia washtakiwa kumkamata Mussa kwa kumbukumbu ya namba ya kesi (RB) ya uongo ya tuhuma za wizi wa pikipiki, lakini RB waliyotoa wenyewe inahusiana na uvunjaji na wizi, kutomfungulia kesi na kugawana pesa zake kama nyara.
Aidha kumwachia kwa dhamana bila wadhamini, kumtaka asirudi tena kituoni hapo na wala asidai fedha zake walizozichukua, kumuita kituoni hapo baada ya kusikia malalamiko yake dhidi yao kuhusu pesa na mali zake walizomchukulia.
Pia ushahidi wa mshtakiwa wa kwanza Kalanje kumfukuza mjomba wa Mussa aliyemsindikiza kituoni hapo, Januari 5, 2022 akimtishia kumpa kesi ya ugaidi.
Washtakiwa na machela
Siku hiyohiyo Januari 5, 2022 mshtakiwa wa kwanza, wa pili, wa tano na mshirika wao Inspekta Greyson Mahembe (marehemu kwa sasa) kuonekana wakiwasili Kituo cha Polisi Mitengo au Mikindani wakiwa na Mussa, walikoomba chumba na godoro kwa ajili ya mahojiano kisha wakamfungia chumbani humo na kuondoka.
Halikadhalika washtakiwa kuonekana wakirudi kituo cha Mitengo usiku wa siku hiyohiyo wakiwa na machela wakieleza kuwa walikwenda kumchukua mgonjwa, wakaingia kwenye chumba walichokitumia mchana kisha wakatoka wamebeba mwili kwenye machela, wakaondoka na gari lao kuelekea uelekeo wa Lindi.
Kutokana na matukio hayo, pia Jamhuri ilieleza kuwa baada ya malalamiko ya kupotea kwa Mussa, mshtakiwa wa tano, Msuya alifichua chanzo cha jambo hilo kwa shahidi wa tatu aliyekuwa RCO Mtwara, SSP Mgonja.
Pia ilieleza kuwa SSP Mgonja alipomuhoji Inspekta Mahembe aliyekuwa mshirika katika tukio hilo alikiri na kwenda kuonesha mahali walipotupa mwili, ambako walipata vipande vya mifupa ya binadamu.
Jamhuri ilieleza kuwa mifupa hiyo iliyofanyiwa uchunguzi wa vinasaba na kulinganishwa na vinasaba katika sampuli za mama wa Mussa ikathibitika kuwa ni ya marehemu Mussa.
“Mheshimiwa Jaji, ni mawasilisho yetu kwa unyenyekevu kuwa ukweli uliotajwa kutokana na mtiririko wa matukio hayo unakidhi mahitaji yote ya ushahidi wa mazingira unaowaelekeza washtakiwa katika hatia”, ilidai Jamhuri.
Mtu wa mwisho kuonekana kuwa na marehemu
Katika kuthibitisha uhusika wa washtakiwa, Jamhuri imetumia kanuni ya mtu wa mwisho kuonekana na mtu ambaye baadaye anapatikana akiwa marehemu.
Hii ni kanuni ya kisheria kwamba ikiwa mshtakiwa anadaiwa kuwa ndiye mtu wa mwisho kuonekana na marehemu, pasipo maelezo yanayokubalika kueleza mazingira yaliyosababisha kifo, atadhaniwa kuwa ndiye muuaji.
“Mheshimiwa Jaji, katika kesi hii, SP Kalanje na ASP Onyango ndio waliokuwa watu wa mwisho kuonekana na marehemu Januari 5, 2022”, ilidai Jamhuri.
“Na bado hawajatoa maelezo yoyote yanayokubalika katika utetezi wao juu ya aliko Mussa au hata kueleza mazingira yaliyopelekea kifo chake,”ulisisitiza.
Ushahidi wa mshtakiwa mwenzao
Jamhuri ilidai kuwa ushahidi wake huo wa mazingira wa uhusika wa washtakiwa katika mauaji hayo uliungwa mkono na ushahidi wa moja kwa moja mshtakiwa wa tano, Inspekta Msuya kama ilivyobainisha hapo juu.
Ilidai kuwa ushahidi huo ulioambatana na masharti ya kifungu cha 62(1)(a) cha Sheria ya Ushahidi, thamani yake ikisisitizwa na Mahakama ya Rufani katika kesi mbalimbali za rejea katika mazingira yanayofanana na hayo.
“Faida ya ushahidi wa moja kwa moja ni ushuhuda wa shahidi kuhusu jambo linalotakiwa kuthibitishwa, iwapo atasema ukweli, alilishuhudia likifanyika; na swali linalobaki ni kama anastahili kuaminiwa.”
Usikose mwendelezo wa simulizi ya kesi hii kesho.