Prime
Kutoka mipango, mauaji mpaka askari kunyongwa– 3

Muktasari:
- Inspekta Msuya alipinga mpango huo, akamshauri Kalanje na wakakubaliana, amchome Mussa sindano ya dawa ya usingizi, ambayo ingemfanya baada ya kuzinduka aeleza yote waliyoyataka. Kilichoendelea, fuatilia sehemu hii ya tatu.
Dar es Salaam. Jana simulizi hii iliishia Gilbert Kalanje aliyekuwa Mrakibu wa Polisi na Mkuu wa Upelelezi wa Wilaya ya Mtwara, akimtaka Mkaguzi na Mganga Mkuu wa Zahanati ya Polisi Mtwara, John Msuya awasaidie kumuua Mussa Hamis kwa kumdunga sindano ya sumu, akidai hataki kutoa taarifa za uhalifu wa wizi wa pikipiki unaofanyika mikoa ya Dar es Salaam, Lindi na Mtwara.
Inspekta Msuya alipinga mpango huo, akamshauri Kalanje na wakakubaliana, amchome Mussa sindano ya dawa ya usingizi, ambayo ingemfanya baada ya kuzinduka aeleza yote waliyoyataka. Kilichoendelea, fuatilia sehemu hii ya tatu.
Mauaji ndani ya kituo cha polisi
Mussa baada ya kudungwa sindano ya usingizi, wakati anakaribia kupoteza fahamu, Kalanje alibadili msimamo, akaamua kuendelea na azma yake ya awali, kumuondoa duniani tofauti kabisa na alichokuwa amemueleza Msuya.
Alimweleza Inspekta Msuya kuwa mpango wake huo wa kumdunga dawa ya kumfanya aeleze mambo yote baada ya kurejewa na fahamu ungewachelewesha sana, hivyo akaamua kutekeleza mauaji ya Mussa.
Hivyo, Kalanje alichukua nguo na kumziba Mussa pua na mdomo hadi akazimia, mbele ya macho ya Charles Onyango, Mrakibu Msaidizi wa Polisi na Mkuu wa Kituo Kikuu cha Polisi Mtwara na Inspekta Msaidizi Grayson Mahembe.
Kwa mujibu wa Inspekta Msuya, alipatwa na mshtuko kwa uamuzi aliouchukua Kalanje kwa kuwa ,hayo hayakuwa makubaliano yao hivyo aliamua kuondoka na kwenda kusimama nje ya chumba hicho.
Baada ya hapo, Kalanje, Onyango na Inspekta Mahembe walikaa ndani ya chumba hicho kwa muda wa takribani dakika 45, kisha walitoka nje wakaufungia mwili wa Mussa ndani ya chumba hicho kwa kufuli.
Wote wakaondoka kituoni hapo (Mitengo) kwa pamoja wakitumia gari moja.
Mwili ulivyotupwa porini
Usiku huohuo, Mahembe alionekana akichukua machela kutoka Kituo Kikuu cha Polisi Mtwara na kuipakia kwenye sehemu ya nyuma ya gari lenye namba za usajili PT 1918 aina ya Toyota Land Cruiser.
Dereva wa gari hilo alikuwa ni Kalanje na mbele upande wa abiria alikaa Onyango na nyuma ya gari hilo alikaa Mahembe na alimkuta askari mwingine.
Kalanje aliendesha gari hilo hadi Kituo cha Polisi Mitengo na wote waliokuwamo ndani ya gari hilo, walishuka wakiwa na machela na kuelekea chumba walichokuwa wameufungia mwili wa Mussa.
Kalanje aliwaeleza askari wa vyeo vya chini waliokuwa doria katika Kituo cha Polisi Mitengo, kwamba, walikwenda hapo kituoni kumchukua mgonjwa.
Waliuweka mwili wa Mussa juu ya machela hiyo na kuubeba hadi nyuma ya gari la polisi walilokwenda nalo kituoni hapo kisha waliingia ndani ya gari lao wakaondoka.
Walikwenda mpaka kwenye msitu wa Kijiji cha Hiari wilayani Mtwara na kuutupa mwili wa Mussa na wakarejea Kituo Kikuu cha Polisi Mtwara.
Mama, mjomba waanza kufuatilia
Januari 7, 2022, mama wa marehemu Mussa (Hawa Ally )na mjomba wake walianza kulalamikia kutoweka kwake na mara ya mwisho alionekana katika Kituo Kikuu cha Polisi Mtwara.
Waliripoti madai yao kwa Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Mtwara na Kamishna Msaidizi wa Polisi Yustino Mgonja aliyeahidi kulifanyia uchunguzi suala hilo.
Uchunguzi juu ya mahali alipo Mussa ulianza, mshitakiwa wa tano ambaye ni Inspekta Msuya alikubali kuzungumza na kuweka mambo wazi, alisimulia tukio zima lililotokea Januari 5, 2022 na kufichua ushiriki wa Mahembe.
Januari 21, 2022, baada ya kuhojiwa, Mahembe naye alitoa maelezo kamili jinsi Mussa alivyouawa na washirika wake katika uhalifu huo.
Aliwaongoza polisi hadi katika Msitu wa Hiari eneo ambako mwili huo wa marehemu Mussa ulitupwa.
Mifupa ya Mussa na DNA
Katika eneo la tukio msituni, polisi walipata mabaki ya mifupa 10 ya binadamu, ramani ya eneo la tukio ilichorwa na picha za tukio zilipigwa.
Baada ya maelezo hayo, siku hiyo hiyo, Januari 21, 2022, Mkaguzi Msaidizi wa Polisi, Mahembe alikamatwa na kuwekwa mahabusu na usiku huohuo, taarifa zilisambaa kwamba alijinyonga akiwa mahabusu.
Mifupa ile ya binadamu iliyopatikana eneo la tukio ulikotupwa mwili wa Mussa ilipelekwa Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali kwa ajili ya uchunguzi wa vinasaba (DNA).
Januari 24, 2022, mama wa marehemu Mussa alipelekwa Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali na alichukuliwa sampuli kwa ajili ya kulinganisha na mifupa iliyopatikana Msitu wa Hiari.
Ripoti ya uchunguzi wa vinasaba ilithibitisha kuwa mifupa iliyopatikana msituni ilikuwa ya mtu mwenye uhusiano wa damu na Hawa Ally, mama wa marehemu Mussa.
Washitakiwa wapandishwa kizimbani
Baada ya uchunguzi wa kina, Januari 25, 2022 washitakiwa walipelekwa mahakamani.
Walipandishwa kizimbani katika Mahakama Kuu, Masjala Ndogo Mtwara, wakasomewa, shtaka hilo moja la kumuua Mussa kwa makusudi kinyume na vifungu namba 196 na 197 vya Sheria ya Kanuni ya Adhabu, Sura 16, Marejeo ya Mwaka 2022.
Walipoitwa kujibu mashitaka hayo, washitakiwa wote walikana mashtaka.
Upande wa mashtaka katika kutekeleza wajibu wake wa kuthibitisha mashtaka dhidi yao, ulilazimika kuwaita mashahidi 28 na vielelezo 16 kuthibitisha kesi yao.
Kwa upande wao, washitakiwa walijitetea na kuwasilisha vielelezo vitatu.
Awali, kesi ilisikilizwa na Jaji Edwin Kakolaki wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dar es Salaam (wakati huo), kabla ya kuhamishiwa kwa Jaji Hamidu Mwanga kutokea Dar es Salaam, ambaye ndiye aliyetoa hukumu hiyo.
Katika nyakati tofauti, Jamhuri iliwakilishwa na mawakili wa Serikali, Matenusi Marandu, Paschal Marungu, Joseph Maugo na Chivanenda Luwogo, Farida Kiobya, Jaggad Jilala na Karangi Joels.
Wengine ni mawakili wa Serikali waandamizi ambao ni Kassim Nassir, Ignas Mwinuka.
Upande wa utetezi (washtakiwa) uliwakilishwa na mawakili wa kujitegemea Majura Magafu, Fredrick Ododa, Nehemia Nkoko, Allex Msalenge, Felister Awasi, Steven Lekei na Emmanuel Ngongi.
Baada ya kumalizika kwa usikilizwaji wa ushahidi wa upande wa utetezi, pande zote mbili ziliomba kuwasilisha hoja zao za mwisho, maombi yaliyoruhusiwa kwa heshima.
Upande wa mashtaka katika hoja zao ulijenga hoja kuishawishi Mahakama kuwa umeweza kuthibitisha hatia dhidi ya washtakiwa huku ukichambua namna ushahidi huo uliweza kumgusa kila mshtakiwa.
Je nini kilitokea, fuatilia Mwananchi kesho Alhamisi