Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Babu aliyebaka mjukuu kisa pombe akwaa kisiki

Muktasari:

  • Shangazi aliyetoa ushahidi katika kesi aliieleza mahakama alimsikia mwathirika wa tukio hilo akilalamika akisema: “Babu niache unaniumiza.” Alieleza alikimbilia kwenye dirisha, alipochungulia aliwaona akajikuta akisema: “Shindwa pepo mchafu.”

Arusha. Mahakama Kuu Masjala Ndogo Moshi, imebariki adhabu ya kifungo cha miaka 30 jela kwa babu aliyetiwa hatia kwa kumbaka mjukuu wake wa miaka 15.

Babu huyo (tunahifadhi jina kwa sababu za kimaadili na kisheria zinazotaka mwathirika asitambuliwe kwa namna yoyote), mkazi wa Ngungu Kilema, wilayani Moshi mkoani Kilimanjaro alitiwa hatiani kwa kitendo hicho alichotenda Mei 12, 2024.

Mahakama ya Wilaya Moshi iliyosikiliza kesi hiyo awali, ilimtia hatiani mshtakiwa huyo ambaye akijitetea alidai hajui alichofanya kwani alikuwa amekunywa pombe.

Hakuridhika na hukumu hiyo akakata rufaa ya jinai  ya mwaka 2024 akipinga adhabu ya kifungo cha miaka 30 jela.

Katika hukumu ya rufaa iliyotolewa Julai Mosi, 2025 na Jaji Adrian Kilimi na nakala kuwekwa kwenye mtandao wa mahakama, baada ya kupitia mwenendo na kumbukumbu za rufaa alihitimisha kuwa upande wa mashtaka ulithibitisha kesi hiyo bila kuacha shaka kuwa babu ndiye alimbaka mjukuu wake.

Jaji ametupilia mbali rufaa na kubariki adhabu iliyotolewa na mahakama ya chini.


Ilivyokuwa

Katika usikilizaji wa kesi ya msingi, upande wa mashtaka ulikuwa na mashahidi wanne na kielelezo kimoja ambacho ni ripoti ya uchunguzi wa matibabu.

Mjukuu aliieleza mahakama kuwa aliishi na babu yake kwa muda wa miaka miwili. Siku ya tukio, jioni babu yake alimwita chumbani akamuuliza kama bado anahitaji pesa kwa ajili ya ziara ya shule.

Alieleza babu yake alimwambia hadi ambake kwanza ndipo ampe fedha alizoomba, hivyo alimvua nguo kisha akainama na kuanza kumbaka.

Kutokana na maumivu aliyopata wakati akifanyiwa kitendo hicho alipiga kelele, shangazi yake aliyekuwa akipita jirani akasikia.

Shangazi aliyekuwa shahidi katika kesi hiyo aliieleza mahakama alimsikia mwathirika wa tukio hilo akilalamika akisema: “Babu niache unaniumiza.”

Alieleza alikimbilia kwenye dirisha, alipochungulia aliwaona akajikuta akisema: “Shindwa pepo mchafu.”

Alieleza mrufani aliuliza nani aliye dirishani, kisha akatoka nje.

Kutokana na hofu, shangazi alieleza alijificha wakati mrufani akitoka nje.

Shangazi alieleza alipoingia ndani alimuuliza binti kuna nini, akamweleza babu yake alimbaka.

Binti huyo alipelekwa Kituo cha Afya Himo alikochunguzwa na Dk Scholastica Taji aliyethibitisha kuwa kitu butu kilipenya sehemu zake za siri.


Babu alivyojitetea

Akijitetea babu alikana kutenda kosa hilo, akieleza amekuwa akiishi na mjukuu wake tangu akiwa na miaka miwili na kwamba, hata yeye alisikia uvumi kuwa amembaka mjukuu wake wakati si kweli.

Alieleza aliposomewa shtaka alikiri kutenda kosa lakini alifanya hivyo kwa sababu ya hofu.

Kuhusu rufaa

Baba katika rufaa alipinga hukumu ya kifungo cha miaka 30 jela alichohukumiwa akitoa sababu saba, ikiwamo hakimu alikosea kisheria kumtia hatiani na kumhukumu licha ya kwamba shtaka halijathibitishwa bila kuacha shaka yoyote.

Sababu nyingine ni hakimu alikosea kutumia ushahidi dhaifu wa mashtaka, wa ajabu na usiotegemewa kabisa kama msingi wa kesi na mashahidi muhimu wa upande wa mashtaka hawakuitwa kutoa ushahidi.

Vilevile, hakimu alijielekeza vibaya katika ushahidi wa shahidi wa kwanza na wa pili ambao haukuwa wa maana na ulijaa mashaka.

Wakati wa usikilizwaji wa rufaa babu hakuwa na uwakilishi wa wakili ila upande wa Jamhuri (mjibu rufaa) aliwakilishwa na Wakili Kambarage Samson.


Uamuzi jaji

Jaji Kilimi alisema amepitia kumbukumbu za mahakama iliyosikiliza kesi hiyo na mwenendo mzima wa shauri hilo, amebaini uamuzi wa mahakama ya awali ulitegemea zaidi ushahidi wa mwathirika wa tukio hilo, ambaye alimtambua vema kwani aliishi naye kwa muda mrefu.

Amesema swali pekee ni iwapo babu alimbaka mjukuu wake? Jaji alisema kulingana na ushahidi uliopo kwenye kumbukumbu na baada ya kutathmini ushahidi wa mwathirika wa tukio hilo anashikilia kwamba, ushahidi ulikuwa wa kuaminika.

“Baada ya kukagua ushahidi wa mwathirika wa tukio, mrufani hakuwahi kumuhoji mwathiriwa kuhusu madai hayo iwapo alimuita chumbani kwake, akamuuliza kuhusu pesa ya ziara ya shule au vinginevyo,” amesema na kuongeza:

“Hii inaashiria alikuwa anakubaliana na kile ambacho mwathiriwa alikuwa akishuhudia, ni sheria kwamba kushindwa kumchunguza shahidi juu ya mambo muhimu kunamaanisha kukubali ukweli au ushuhuda huo.”

Jaji amesema baada ya kutathmini upya ushahidi wa upande wa mashtaka na utetezi wa mshtakiwa; upande wa mashtaka ulithibitisha kesi bila kuacha shaka yoyote, hivyo kutupilia mbali sababu zote za rufaa na rufaa hiyo kutokana na kukosa mashiko.