Ofisa Magereza Moshi apandishwa kizimbani kwa kesi ya ulawiti

Emmanuel Nyange (35) Ofisa wa Magereza, mkoani Kilimanjaro akiwa katika viunga vya mahakama ya Wilaya ya Moshi, akikabiliwa na shitaka la ulawiti.
Muktasari:
- Ofisa huyo amefikishwa mahakamani hapo leo Juni 24, 2025 mbele ya Hakimu Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Ruth Mkisi na kusomewa shitaka moja la ulawiti.
Moshi. Ofisa wa Magereza, Emmanuel Nyange (35), ameshtakiwa na kupandishwa kizimbani katika Mahakama ya Wilaya ya Moshi, mkoani Kilimanjaro, akikabiliwa na shtaka la kumlawiti mtoto wa miaka 13.
Ofisa huyo amefikishwa mahakamani hapo leo Juni 24, 2025 mbele ya Hakimu Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Ruth Mkisi na kusomewa shitaka moja la ulawiti.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Abel Mtagwa, alithibitisha kukamatwa kwa mtuhumiwa huyo na kueleza kuwa taratibu za kijeshi dhidi ya askari huyo zinaendelea.
Aliongeza kuwa hatua nyingine za kisheria zitachukuliwa mara tu taratibu hizo zitakapokamilika.
Akimsomea shitaka hilo, Mwendesha Mashitaka wa Serikali, Jesca Kamuhambwa ameeleza mahakama hiyo kuwa, mshitakiwa huyo alitenda kosa hilo Juni 5, 2025 katika eneo la Kijiji cha Rauya, Marangu, Wilaya ya Moshi.
"Mshitakiwa Emmanuel Nyange ambaye ni Ofisa wa Magereza anashitakiwa kwa tuhuma moja ya kumlawiti mvulana wa miaka 13, katika eneo la Rauya, Wilaya ya Moshi,"ameileza mahakama hiyo
Aidha, mwendesha mashitaka huyo wa Serikali amedai mahakama hapo kuwa, upelelezi wa kesi hiyo umekamilika na hivyo kuomba tarehe kwa ajili ya usikilizwaji wa maelezo ya awali (PH).

Emmanuel Nyange (35) Ofisa wa Magereza, mkoani Kilimanjaro (aliyevaa kofia nyeusi) akipelekwa katika chumba cha mahakama ya Wilaya ya Moshi, akikabiliwa na shitaka la ulawiti.
Hata hivyo, mshitakiwa huyo amekana shitaka hilo na kutokana na kwamba kesi yake ina dhamana alitakiwa kuwa na wadhamini wawili kila mmoja kuweka bondi ya Sh1 milioni ambapo mshitakiwa alikidhi masharti na kuachiliwa kwa dhamana.
Hata hivyo, Hakimu Mkisi ameahirisha kesi hiyo namba 15401/25, mpaka Julai 9, mwaka huu kwa ajili ya usikilizwaji wa maelezo ya awali.